Mkandarasi Bwawa la Nyerere aigomea Tanesco miradi ya jamii nje ya mkataba

Muktasari:

  • Zaidi ya Sh262.34 bilioni zinazotakiwa kutolewa kwa miradi ya jamii kwa wananchi (CSR), hazijatolewa tangu Bwawa la Julius Nyerere lilipoanza kujengwa mwaka 2018, baada ya mkandarasi anayejenga bwawa hilo kukataa mapendekezo ya Tanesco.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limedaiwa kukwamisha utekelezaji wa miradi ya kijamii ya Sh262.34 bilioni tangu ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere ulipotiwa saini Desemba 12, 2018.

Hali hiyo imeelezwa kutokana na Tanesco kupendekeza miradi ambayo mkandarasi amesema haiendani na vigezo vilivyoainishwa katika mkataba baina ya pande hizo mbili.

Hayo yameelezwa na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2022/23.


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere


Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Aprili 16, 2024, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema suala hilo linaweza kujibiwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Felchesmi Mramba.

Mramba alipoulizwa naye alisema Tanesco wenyewe ndiyo wanaopaswa kulijibu kwa kuwa ndio waliokaguliwa na CAG.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamohanga alipoulizwa, alisema suala hilo bado linajadiliwa.

“Hilo siwezi kulijibu sasa hivi kwa sababu bado tunalijadili. Kama ulivyoona linatoka kwa CAG, kwa hiyo bado litajadiliwa pengine hata bungeni, sasa tulipe muda tusi pre-empt (kuwahisha kabla ya wahusika), tulipe muda kwanza,” amesema.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyokabidhiwa bungeni juzi, Tanesco ilitakiwa kusaini makubaliano ya kina kuhusu CSR ndani ya mwezi mmoja, baada ya kusaini mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere kwa mujibu wa kifungu cha 2.1.6 cha makubaliano hayo.

Kutokana na makubaliano hayo, mkandarasi alitakiwa kuanza utekelezaji wa miradi ya kijamii ndani ya mwezi mmoja baada ya kusaini makubaliano ya kina, na kuwa malipo ya awali yamelipwa chini ya mkataba wa mradi huo.

“Mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ulitiwa saini Desemba 12, 2018 na makubaliano ya kina ya miradi ya kijamii yalipaswa kutiwa saini Januari 13, 2019.

“Hata hivyo, hadi kufikia Juni 30, 2023 mkataba wa kina wa utekelezaji wa miradi ya kijamii ulikuwa bado haujatiwa saini, ikiwa ni ucheleweshwaji wa zaidi ya miaka minne,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa CAG, ucheleweshwaji huo umechangiwa na kuchelewa kuanzisha mazungumzo ya kusaini mkataba wa kina juu ya miradi ya kijamii.

“Ninaona kuchelewa kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuna hatari ya kushindwa kutekeleza miradi ya kijamii kwa wakati, ikizingatiwa kuwa mradi uko katika hatua ya kukamilika,” inaeleza ripoti ya CAG.  

Pia CAG anasema kuwa Desemba 16, 2019 kilifanyika kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo lakini pande hizo mbili hazikuafikiana.  

CAG anasema katika kikao hicho, pande hizo zilijadiliana kutekeleza miradi hiyo, hususani ujenzi wa uwanja wa michezo wa Dodoma na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Fuga hadi Bwawa la Julius Nyerere.

“Hata hivyo, makubaliano hayakutiwa saini kutokana na mkandarasi kueleza kuwa miradi iliyopendekezwa haiendani na vigezo vilivyoainishwa katika mkataba wa utekelezaji wa miradi ya kijamii, kwa kuzingatia aina na utaratibu wa utekelezaji,” anaeleza.

Kutokana na mazingira hayo, CAG anaitaka Tanesco  iwasiliane na Wizara ya Nishati kwa ajili ya kuhitimisha na kuchagua miradi itakayotekelezwa na mkandarasi, iwasilishwe kwa mkandarasi ili kuwezesha utiaji saini wa mkataba wa kina wa utekelezaji wa miradi ya kijamii.


Wasubiri bila mafanikio

Kutokana na mzozo huo, Mwananchi imezungumza na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Aboubakar Chobo ambaye amesema wamekuwa wakisubiri miradi ya jamii kutoka Bwawa la Julius Nyerere bila mafanikio.

“Tumeshalalamika sana kwa barua tuliyowaandikia Tanesco, lakini haijajibiwa hadi leo. Ieleweke kuwa CRS si zawadi, iko kisheria,” amesema.  

Amesema licha ya kuzungushwa, taarifa walizozipata ni kwamba wilaya hiyo itaambulia Sh10 bilioni tu.

“Tunasikia tutapewa Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali na Sh10 bilioni nyingine zitapelekwa Mkoa wa Morogoro na nyingine mikoa mingine. Tulitarajia kwamba tupate mgawo mkubwa kwa sababu ndio tuko karibu na mradi.

“Awali, tulishakaa na kupanga bajeti ya hizo fedha, kama kujenga barabara, vituo vya afya, masoko shule na hata haya mafuriko ya sasa zingetufaa, lakini tunaona mzigo wote umehamishwa,” alisema.

Kwa upande mwingine, wadau wa haki ardhi wamehoji sababu ya Tanesco kutaka ujenzi uwanja wa michezo mkoani Dodoma, ilihali wananchi wa Rufiji mkoani Pwani ndio wako karibu.

“Wanaotakiwa kufaidika na miradi ya jamii ni wale wananchi wanaoishi karibu na mradi, lakini kujenga uwanja wa michezo mkoani Dodoma, hakuna justification (uhalali),” amesema Bernard Baha, mdau wa haki za ardhi.

Ameongeza, “wananchi wa Rufiji na Kibiti ndio wahusika wa huo mradi kwa sababu wako chini, eneo maji yanakoelekea.”

Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi, Cuthbert Tomito amesema ucheleweshwaji miradi ya kijamii katika mradi huo, unaibua maswali mazito kuhusu fedha hizo.

“Maana ya CSR (miradi ya jamii) kama inavyofanywa kwenye kampuni za madini, kilimo na nyinginezo ni kufaidisha wanajamii walio karibu na mradi. Inaweza kuwa ni fedha moja kwa moja, au kuwajengea mradi au kutoa ajira kwa wanajamii.

“Bahati nzuri mkandarasi anafahamu, ndio maana amewakatalia Tanesco,” alisema.