Mitihani ya kidato cha sita kuanza kesho

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk Said Mohamed akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Watahiniwa 113,504 wa kidato cha sita na ualimu ngazi ya cheti na stashahada wanatarajiwa kuanza mitihani yao kesho Mei 6 mwaka 2024.

Dar es Salaam.  Jumla ya watahiniwa 113,504 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, kuanzia kesho Mei 6 mwaka huu huku ikitarajiwa kumalizika Mei 24.

Mtihani huo wa kidato cha sita, utafanyika kwenye jumla ya shule 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 258.

Pamoja na hayo, mitihani ya ualimu ngazi ya cheti na stashahada inatarajiwa kuanza rasmi Mei 6 Tanzania Bara na Zanzibar na inatarajiwa kumalizika Mei 20 mwaka huu, ikifanyika katika vyuo vya ualimu 99.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Mei 5, 2024 na Katibu Mkuu Mtendaji wa Necta Dk Said Mohamed alipokuwa akitangaza kuanza kwa mitihani hiyo.

Dk Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 113,504 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita 2024, ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 104,449 na watahiniwa wa kujitegemea  ni 9,055.

"Mwaka 2023 idadi ya watahiniwa shule za kujitegemea na waliosajiliwa walikuwa 106,883, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 6,621 sawa na asilimia 6.19 kwa mwaka 2024, ukilinganisha na mwaka 2023," amesema Dk Mohamed.

Akizungumzia maandalizi ya mitihani ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2024, amesema yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani husika, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani hiyo.

“Kamati zote za mikoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu kwa kutoa semina kwa wasimamizi wa mitihani pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,” amesema Dk Mohamed.

Akitoa wito kwa kamati za mitihani, wasambazaji na waniliki wa shule na jamii, amesema pamoja na maandalizi yote muhimu yaliyofanyika kamati za mikoa na halmashaauri zihakikishe usalama wa vituo vya mitihani na unaimarishwa na vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Necta

 "Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mitihani kufanya kazi yao kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu na kuhakikisha wanafika kwa wakati katika vituo husika,” amesema.

Akitoa wito kwa watahiniwa amesema, wakuu wa shule wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kutekeleza kwa kuzingatia usimamizi uliotolewa na Baraza.

"Baraza linawaasa wamiliki wa shule kutambua ushirikiano unaotakiwa wakati wa uendeshaji wa mitihani, ili wote wafanye kazi katika hali ya utulivu," amesema.