Misuguano ya uchaguzi isivyoacha watu salama

Sehemu ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na wageni waliohudhuria hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa hilo. Picha na Maktaba

Moshi/Dar. Kuna usemi kuwa siku zote uchaguzi hauwezi kumwacha mtu salama. Ndivyo unavyoweza kuelezea masuala yatokanayo na uchaguzi katika ngazi mbalimbali nchini – ziwe za kisiasa au za kidini.

Hali hiyo ndiyo iliyotokea wiki iliyopita baada ya uchaguzi wa mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ulioibua manung’uniko na mijadala katika mitandao ya kijamii.

Hali kama hiyo imekuwa ikionekana pia katika madhehebu mbalimbali na katika vyama vya siasa nchini.

Kiini cha manung’uniko hayo kinachambuliwa na viongozi wa dini na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wakisema sababu ni uchaguzi kuendeshwa bila kufuata misingi ya taasisi na kukosekana uwazi kwenye uchaguzi husika.

Uchaguzi KKKT

Katika uchaguzi wa KKKT uliofanyika Alhamisi ya Agosti 24 mwaka huu, Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani alichaguliwa kuwa mkuu wa kanisa kwa kura 167 dhidi ya 73 alizozipata Askofu Abednego Keshomshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.

Uchaguzi huo unaweza kuwa ndio uliojadiliwa zaidi katika mitandao ya kijamii, washarika wa KKKT na hata waumini wa madhehebu mengine.

Baada ya uchaguzi huo, mjadala umejikita kwenye manung’uniko si tu kwenye mitandao ya kijamii, bali hata kwa baadhi ya washarika na maaskofu wenyewe.

Miongoni mwa waliojadili yatokanayo na uchaguzi huo ndani ya kanisa ni Askofu Benson Bagonza wa Karagwe, akiungwa mkono na Stephen Munga, askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Askofu Bagonza aliandika ujumbe wa kifalsafa, wenye uhusiano wa moja kwa moja na uchaguzi huo, akieleza wazi kwamba amejizuia sana kuandika au kusema chochote hadi aliposongwa sana.

Kwa upande wake Munga, katika andiko lake ambalo alilithibitishia gazeti hili kuwa ni lake, alionekana kuunga mkono kile alichokisema Askofu Bagonza, akimtia moyo kuwa japo hakuwa mgombea mkutano mkuu, bado alipigiwa kura na wajumbe.

“Sitaki kuingilia mipango na makusudi ya Mungu, lakini naomboleza kwako Askofu Bagonza kwa kufanyiwa dhuluma ili jina lako lisiteuliwe upigiwe kura na wajumbe wa sinodi ya kanisa. Moyo wangu unaugua. Nimehuzunika sana kwa ajili yako”

Askofu Shoo autetea

Hata hivyo, mkuu wa Kanisa hilo anayemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo alijitokeza na kuzungumzia uchaguzi huo: “Tunamshukuru sana Mungu mkutano mkuu ulienda na kumalizika salama kabisa. Uchaguzi ulienda vizuri kwa kufuata Katiba.

“Maaskofu wote walioko kazini isipokuwa mkuu anayemaliza muda wake walipigiwa kura na halmashauri kuu kupata majina matatu ya kupeleka kwenye mkutano mkuu kupigiwa kura, ndipo Dk Malasusa akaibuka kidedea,” alisisitiza.

“Ninajua ni kawaida watu kuzungumza mengi baada ya uchaguzi kama huu. Muhimu na wito wangu kwa wanakanisa wote ni kukubali matokeo na kumwombea sana mkuu aliyechaguliwa,” alisema Askofu Shoo Jumamosi iliyopita.

Chaguzi nyingine

Mwaka jana, ulishuhudiwa mgogoro katika Dayosisi ya Konde ya KKKT mkoani Mbeya kuhusiana na masuala ya uchaguzi ambapo Askofu Edward Mwaikali aliyeondolewa madarakani, alikimbilia mahakamani kupinga uchaguzi huo, lakini kesi hiyo ikatupwa.

Vilevile, masuala ya uchaguzi mara kadhaa yamewahi kuwa na migogoro ndani ya Kanisa la Anglikana kama ule wa Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay akichuana na Profesa Emmanule Mbenah uliopelekea waumini kufungua kesi mahakamani.

Pia uchaguzi wa Askofu wa Dayosisi ya Nyanza uliomweka madarakani Askofu Boniface Kwang ulikuwa na mzozo kwamba kampeni zilihusisha matumizi ya fedha.

Hata uchaguzi uliomweka madarakani Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani ulikuwa na mvutano kati ya upande wake na Canon Moses Matonya na kupelekea kura kurudiwa mara mbili, japokuwa ulimalizika salama.

Si tu upande wa makanisa hayo tu, ipo pia mifano ya upande mwingine, kama kitendo cha waumini wa msikiti wa Raudhwa uliopo jijini Mwanza walipoiomba Serikali kuingilia kati na kuzuia uchaguzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa msikiti huo, wakidai mchakato wake unakiuka Katiba.

Ukiacha uchaguzi wa kidini, kwenye siasa mambo ndiyo mazito zaidi na malalamiko yamekuwa yakiibuka kila uchaguzi unapofanyika na migogoro mingine huishia mahakamani.

Vilevile yamekuwepo matukio ya watu kujeruhiwa, kukamatwa na hata kupoteza maisha kutokana na mivutano ya kiuchaguzi.

Sababu za migogoro

Akizungumzia sababu za hali hiyo, Sheikh Khamis Mataka, mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), alisema manung’uniko hayo ni ishara ya uchaguzi kuendeshwa bila kuzingatia maadili ya dini na kuruhusu mambo yasiyofaa kuingilia dini, akitolea mfano kampeni chafu na utoaji wa rushwa.

“Uchaguzi wa dini unapofanywa kama wa kisiasa lazima ulete manung’uniko baada ya uchaguzi. Nasaha kubwa kwa waandaaji na wasimamizi wamuogope Mungu ili wafanye kazi yao kwa uadilifu.

Lakini kwa wanaoshindwa wakubali, wajue ule ulikuwa mtihani wa kutumikia watu, ukikosa endelea kutoa ushirikiano kwa sababu wewe ni sehemu ya watu hao,” alisema.

Kwa jicho la kisiasa, Dk Paul Loisulie, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma, alisema yanayotokea baada ya uchaguzi wa dini ni ishara kwamba “uchaguzi ni uchaguzi”.

Akifafanua, alisema kwenye uchaguzi upo uhuru wa kuamua na hali hiyo husababisha kuwepo kwa pande mbili zinazokinzana na ukinzani huo lazima ulete matokeo ya kukandamiza upande mmoja.

“Pamoja na yote kwenye uchaguzi huo watu ndio wanaoshiriki si malaika, hivyo lazima ubinadamu uonekane. Kwa binadamu kuna vionjo hisia.

Hivyo, alisema lazima kutokee vitu tofauti kwa kuwa hata kama uchaguzi umeendeshwa kwa uhuru na haki, aliyeshindwa kutokana na matarajio yake anakuwa na msongo wa mawazo, lazima kutakuwepo maneno.

Ili kuondoa malalamiko, alisema ni muhimu kwenye taasisi za dini kupunguzwa demokrasia.

Akijadili suala hilo, Abbas Mwalimu, mchambuzi wa masuala ya siasa, alisema taasisi za dini utofauti wake na nyingine ni kuongozwa kiroho.

“Wanaoongoza taasisi za kidini ni binadamu. Wana utashi, mtazamo, matamanio, mafungamano na hivi vyote ndivyo vinatoa upande, kwamba taasisi licha ya kuwa na taratibu za uchaguzi, wanaoshiriki licha ya kuwa viongozi wa dini, bado ni binadamu.

Kwa hiyo wanarudi kwenye mitizamo ya kibinadamu badala ya Kimungu na kuona kuna sehemu hawajatendewa haki,” alisema.

Alisema uchaguzi wowote lazima uache makovu, akisisitiza hata ngazi ya familia uchaguzi ukifanyika lazima watakuwepo watakaosema aliyechaguliwa hakustahili.

Nyongeza na Habel Chidawali