Mikasa nyumba za kupanga, hatari ya kuzeeka mapema

Muktasari:

  • Mazingira yenye usumbufu, kudaiwa kodi za nyumba mara kwa mara, kupanga nyumba zilizo kwenye maeneo yenye viwango vya juu vya uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha kuzeeka mapema.

Dar es Salaam. Maisha ya kila siku kwenye nyumba za kupanga yamegubikwa na matukio kadhaa yaliyojaa visa na mikasa, ikielezwa yanachangia watu kuzeeka mapema.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital kwa takribani wiki moja umebaini matukio hayo yanayohusisha majirani, chanzo ni matumizi ya maji, umeme na suala la usafi.

Si hayo pekee, ipo migogoro inayojitokeza kwa mmoja wa majirani kuomba mboga kwa mwingine, kuibiana vyombo na hata kujazana sebuleni kwa jirani kuangalia tamthilia kwenye runinga.

Tembea uone mambo, ndivyo Waswahili husema: Wapo wapangaji wanaoingia kwenye ugomvi kutokana na kuchukizwa na tabia za ama mwanaume au mwanamke kuwa na mahusiano na watu mbalimbali ambao kwa nyakati tofauti hupishana ndani ya chumba chake.

Si hivyo pekee, wapo wanaochukizwa na nyendo za wenye mahusiano hao wawapo bafuni au maeneo mengine wanaposhindwa kuwa na staha.

Changamoto nyingine inayozua migogoro ni kwa wale wanaopeleka waganga wa jadi ndani ya nyumba au vyumba vyao.


Ununuzi wa umeme

Kwa wapangaji wanaochangia mita za umeme (Luku) wengi huwekeana utaratibu wa kununua kwa mzunguko wa siku, wiki au mwezi kulingana na vipato au hadhi ya wakazi wa nyumba husika.

Mgogoro huibuka pale in apofika zamu ya mmoja wapo akachelewa kununua kisha akakumbushwa kutekeleza wajibu wake.

Hapo huibuka zogo la wengine kudai hawana matumizi makubwa isipokuwa mtu fulani, yupo atakayesema anatumia taa pakee, mwingine akielezwa ana jokofu, redio na runinga hivyo anatumia umeme mwingi.

Itaelezwa huyu anatumia pasi kwa kificho, ama birika ya kuchemsha maji au jiko la kupikia la umeme.

Si ajabu kwa baadhi ya nyumba kukuta wakilala giza kwa sababu tu mwingine kakataa kununua umeme zamu yake. Asipotokea wa kuokoa jahazi, kinachofuata ni malumbano.


Usafi wa mazingira

Kila wapangaji hujiwekea utaratibu wao, kwa wanaume ambao hawajaoa kwenye nyumba zingine hupewa jukumu la kununua vifaa vya usafi kama vile dawa, sabuni na ufagio.

Kwenye nyumba zingine hulazimika kuwalipa walio tayari kufanya usafi kwenye zamu zao.

Hata hivyo, migogoro huibuka pale mtu anapoingia msalani baada ya usafi kufanyika halafu akatoka na kuacha mazingira yakiwa machafu.


Changamoto ya akili

Akizungumza na Mwananchi, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, Dk Said Kuganda amesema migogoro kwenye nyumba za kupanga ipo katika sura mbili, mosi kushuhudia wapangaji wenzako wakizozana; pili kuwa sehemu ya mgogoro huo.

“Sasa wewe unapokuwa sehemu ya kugombana na majirani utakuwa unaishi maisha eneo ambalo amani haipo, kuna mtu anakupotezea amani hii ndiyo tunaita changamoto kwenye akili kwa sababu akili yako inakosa utulivu kwa muda mrefu,” amesema.

Amesema mtu anapokosa utulivu kwa muda mrefu hupata msongo ambao humshinda na tabia za mtu husika huanza kubadilika.

“Mfano mhusika (anayepitia migogoro kwenye nyumba za kupanga) anapoenda kumsalimia ndugu yake lazima ataonekana tabia zake zimebadilika na ataulizwa mbona umebadilika kwa nini unakuwa mkali, hivyo kumbe ameyatoa huko alipotoka kutokana na ugomvi wa muda mrefu,” amesema.

Ameeleza, “Sehemu yoyote mtu anayoishi na hana amani, sehemu hiyo ina changamoto ya afya ya akili na eneo hilo linahitaji mtu anayeweza kukabiliana na mazingira hayo.”

Dk Kuganda amesema kama ugomvi huo utadumu kwa muda mrefu una waathiri watoto kiakili.


Kupungua umri wa kuishi

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Essex na Chuo Kikuu cha Adelaide nchini Australia umebainisha kukodi nyumba kutoka kwa mtu au kampuni binafsi kunaweza kumsababisha mtu kuzeeka haraka.

Mambo yaliyoainishwa katika utafiti huo yanayosababisha uzee kwa wapangaji wa nyumba binafsi ni kuwa kwenye mazingira yenye usumbufu, kudaiwa kodi za nyumba mara kwa mara, kupangisha nyumba zilizo kwenye maeneo yenye viwango vya juu vya uchafuzi wa mazingira.

Utafiti huo uliochapishwa mwaka 2023 kupitia jarida la Epidemiolojia na Afya ya Jamii unafafanua kuwa uzee husababishwa na msongo wa mawazo ambao ni chanzo cha mwili kuzeeka.

Utafiti huo uliendeshwa kwa kutumia taarifa za kiafya zilizokusanywa kwa watu 1,420 walioishi katika kaya mbalimbali nchini Uingereza.


Simulizi za wapangaji, wenye nyumba

Josephine Solomon, mkazi wa Tabata Kisiwani akizungumza na Mwananchi Digital amesema migogoro kwenye nyumba za kupanga baina ya majirani unatokana na uchafu na kudharauliana.

“Unakuta mtu anaenda uani akimaliza haja zake hasafishi, anaondoka unapokuta uchafu mara kwa mara huwezi kuvumilia, lazima useme watu wabadilike,” amesema.

Amesema tatizo lingine ni ankara za umeme na maji, akieleza wapo wapangaji wenye vifaa vya kielektroniki vinavyotumia umeme hivyo huwasha jokofu, runinga na pasi kwa pamoja kila siku anapoambiwa aongeze fedha kwa ajili ya malipo ya umeme hukataa.

Yusuph Juma, mkazi wa Mbezi amesema yanayochangia migogoro baina ya wapangaji ni tabia ya kuweka taka kwenye mfuko wa jirani yake.

“Mfano kwa hapa tunapoishi tuliwahi kuamua mgogoro wa mtu kuchukua taka zake na kuziweka kwenye mfuko wa mtu, taka hizo zilikuwa za kitimoto na aliyewekewa hali vitu hivyo, watu walitoleana maneno mabaya,” amesema.

Tukio lingine analosimulia ni mpangaji aliyewekewa taka kwenye mfuko wake na kwenda kuzimwaga barazani kwa aliyeziweka.

Akizungumzia zamu ya kufanya usafi, ikiwamo kufagia na kudeki vyoo, amesema mara nyingi vijana wa kiume hawafanyi bali huombwa kuchangia vifaa.

“Sasa anapoomba yeye asideki wala asifagie ananunua ufagio, sabuni na brashi kila inapofika zamu yake anaambiwa anunue nyingine, wengi hawakubali ndipo huibua mgogoro wakisema haiwezekani kununua kila mara, hapo huambiwa watekeleze zamu yao jambo ambalo kwao ni gumu,” amesema.

Yusuph amesema kelele za redio huwa kero kwa wengine na huchangia msuguano.

Amesema wapo watu hufungulia radio usiku hadi asubuhi na anapoambiwa apunguze sauti anadai amelipa kodi na yupo kwake.

Amir Nyoni, dalali mkazi wa Tabata amesema ‘Uswahili’ unachangia migogoro.

“Unakuta mtu anapika vizuri, anavaa vizuri mtu anaanza kumfuatilia na kumwekea vijembe, wengine mambo hayo hawewezi yakiwashinda wanahama. Kuna mpangaji aliwahi kuhama nyumba kutokana na jirani yake kumfanyia vitendo vya kishirikina kumharibia kazi yake,” amesema.

Philimon Hosea, mmiliki wa nyumba eneo la Tabata Kisiwani amesema mwaka 2019 alilazimika kuwaondoa wapangaji wake wawili baada ya kupigana kwa madai ya kuchukuliana wanaume.

“Migogoro kwenye nyumba za kupanga haiwezi kukosa kwa sababu watu wana tabia tofauti, hivyo wapo wanaofuatilia maisha ya wengine na suala la usafi na kuchangishana fedha lazima lilete migogoro,” amesema.


Matukio polisi

Mwaka 2023 Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, lilitangaza kumshikilia Blandina Fred mkazi wa Kijiji cha IIkirev, Kata ya Olturoto wilayani Arumeru, kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma kisu mpangaji mwenzake, Erick Adam kutokana mchango wa Sh1, 000 za ununuzi wa umeme.

Taarifa ya Polisi ilisema tukio hilo lilitokea baada ya ugomvi baina ya wapangaji hao wawili, Adam ikielezwa aligoma kulipia umeme.

Mwaka 2017 mwanamke mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam alichomwa kwa kisu usoni na kifuani na jirani yake baada ya mgeni wake kuvaa kandambili za mwenzake.

Baada ya mwenye kandambili kuuliza akaambiwa zimevaliwa na mgeni wa mpangaji, akasema hataki mazoea na watu ndipo ukazuka ugomvi.


Utafiti wa upangaji

Ripoti ya utafiti uliopewa jina Mikopo ya Makazi (HMF) uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Makazi (HFHI) na Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) na kutolewa mwaka 2023 unaonyesha, asilimia 70 ya Watanzania wanaishi katika nyumba za kupanga, huku wanaojenga wakichukua muda mrefu zaidi ya miaka 18.

Utafiti huo ulifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma kwa wananchi wenye umri wa miaka 25 hadi 50 wakiangaliwa hali ya vipato vyao.