Mikakati mitatu ya Rais Samia kwenye kilimo kwa vijana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mjadala wa masuala ya kilimo na vijana wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Septemba 7, 2023. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Huenda kilio cha masoko ya mazao kwa wakulima ikabaki kuwa historia nchini, hii ni baada ya mikakati ya Serikali kwa kutengeneza muunganiko wa moja kwa moja kati ya mkulima na soko, kujenga miundombinu bora kwa ajili ya wakulima na kuendelea na mkakati wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT).

Mikakati hiyo imetajwa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliposhiriki moja ya mijadala katika mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF), unakuja kipindi ambacho, baadhi hukitazama kilimo kama shughuli isiyo na matumaini.

Akizungumza katika jukwaa hilo, leo Septemba 7, 2023, Rais Samia amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kutaja mambo mawili yanayofanyiwa kazi baada ya utafiti uliofanywa kusaka muarobaini wa masoko hayo.

“La kwanza ni kujua bidhaa gani inatakiwa wapi ndani na nje ya nchi, tukijua hilo tutajua hasa wapi nini kinazalishwa na kinatakiwa kwenda wapi, lakini la pili ni muunganiko wa mkulima na soko lenyewe, hatujaifanya sawa sawa,” amesema.

Ingawa juhudi zimefanyika katika baadhi ya mazao, mkuu huyo wa nchi amesema yapo mengine ambayo hadi sasa wakulima wanakabiliwa na changamoto ya kupata masoko yake.

Miongoni mwa mazao aliyoyataja kuwa na ufumbuzi wa masoko, ni korosho, ufuta na mbaazi, kwani yanauzwa kwa wanunuzi kushindana kupitia mfumo wa mauzo ya stakabadhi ghalani.

Pamoja na juhudi hizo, kuunganisha miji na nchi kwa kujenga miundombinu ya barabara, ameitaja kuwa hatua nyingine muhimu inayochukuliwa na Serikali yake kufuta machozi ya wakulima kuhusu masoko.

“Sio barabara pekee tunatengeneza bandari za Mikoa mbalimbali ziwe na uwezo wa kupokea meli kushusha malighafi na kupokea bidhaa kwa ajili ya kusafirisha,” amesema.

Kwa upande mwingine, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imejidhatiti kuiendeleza sekta ya kilimo siyo tu kwa manufaa yake, bali kwa manufaa ya bara zima la Afrika na dunia kwa ujumla.

Mkuu huyo wa nchi amesema Tanzania iliweka mkakati wa kuifanya sekta ya kilimo ichangie asilimia 10 kwenye pato la taifa ifikapo mwaka 2030. Ili kutekeleza ajenda hiyo, tulianzisha mpango wa kujenga kesho iliyo bora (BBT) kwa vijana wa Tanzania.

“Lengo kuu la BBT ni kuwezesha ushiriki wa vijana kwenye sekta ya kilimo kuinua maisha yao na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema malengo ya kimkakati ya BBT ni pamoja na kuwavutia vijana kushiriki kwenye miradi ya kilimo chenye faida, ufugaji na uvuvi na kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo.

Malengo mengine ni kuwashirikisha vijana kwenye biashara ya kilimo na pia kuwaongoza vijana kwenye kampuni za ujasiriamali na kuboresha mazingira ya biashara.

Amebainisha kwamba mpango huo unalenga kutengeneza ajira milioni tatu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kufikia mwaka 2030. Vilevile, amesema BBT inakusudia kuanzisha kampuni za vijana 12,000.

“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, BBT imefanikiwa kuwachukua vijana na wanawake 1,252 na hadi sasa, vijana 812 wamejiandikisha kupata mafunzo ya miezi mine ya biashara ya kilimo katika atamizi 13.

“Sh10.7 bilioni zimetengwa na serikali kwa ajili ya kuwapatia vijana misaada na mikopo nafuu. Dalili njema zinaonekana kwamba vijana wanaweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo,” ameeleza kiongozi huyo.