Miili ya wanajeshi wa Tanzania waliofia Congo kuwasili nchini

Muktasari:

  • Wanajeshi waliopoteza maisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itawasili nchini siku chache zijazo, Msemaji wa Serikali Mobhare Matinyi ameeleza.

Dar es Salaam. Miili ya wanajeshi watatu raia wa Tanzania waliopoteza maisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), itawasili nchini hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania,  Mobhare Matinyi amethibitisha.

 Wanajeshi hao watatu ni miongoni mwa waliotumwa katika operesheni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenda nchini DRC kwa ajili ya kulinda amani. Katika tukio hilo wanajeshi wengine watatu wamejeruhiwa.

Taarifa ya kifo na majeruhi ya wanajeshi hao SADC ilitolewa kwa umma Aprili 8, 2024 ikisema, tukio hilo limesababishwa na kombora lililoangukia karibu na kambi ya wanajeshi hao.

Leo Aprili 12, 2024 Matinyi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ametoa taarifa ya majeruhi na miili ya wanajeshi waliofariki dunia.

“Wanajeshi wanaendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa wanajeshi waliopo kule ambao wana utaratibu wa kuangalia majeruhi, Pia miili inafanyiwa taratibu itawasili sina tarehe kamili ya lini miili itawasili, lakini miili ya mashujaa wetu hao itawasili nchini kwa siku chache zijazo,” amesema.

Juzi, SADC kupitia taarifa yake iliandika kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea baada ya kombora kuangukia karibu na kambi waliyokuwa wakiishi wanajeshi hao.

“SAMIDRC inasikitika kutangaza kifo cha mwanajeshi wa Afrika Kusini aliyefariki wakati akipatiwa matibabu kutokana na changamoto za kiafya katika Hospitali ya Goma, DRC,” iliandikwa kwenye taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Familia ya SADC inatoa salamu za rambirambi kwa familia wapendwa hao  Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msiba  huo na wakati huohuo, tunawatakia ahueni ya haraka askari watatu waliojeruhiwa,” iliandikwa kwenye taarifa hiyo ya SADC.

Kufuatia taarifa hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Dk Stergomena Tax ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda.

Pia amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda amani katika mipaka na nje ya mipaka yetu kulingana na makubaliano na Itifaki za kikanda na kimataifa.