Mbunge ataja mbinu kunusuru wanafunzi kuchezea kondomu

Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula akizungumza wakati akiuliza swali kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo Jumanne, Aprili 23, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Swai la Dk Mabula limekuja kutokana na eneo la shule hiyo kutumiwa na dada poa nyakati za usiku hivyo kuacha zana wanazozitumia ambazo ni mipira (kondomu). 

Dodoma. Mbunge wa Ilemela, Dk Angelina Mabula ameitaka Serikali kujenga uzio katika Shule ya Msingi Kitangili  iliyopo mkoani Mwanza ili kuokoa maisha ya watoto wanaochezea  kondomu katika uwanja wa mpira.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo Jumanne Aprili 23, 2024, Dk Mabula  amesema eneo hilo lenye shule mbili nyakati za usiku limekuwa likitumiwa na dada poa na  lipo katika uwanja wa CCM wa Kirumba.

“Ni lini Serikali itaweka uzio ili kuokoa maisha ya watoto ambao wanachezea mipira (kondomu), “amehoji Dk Mabula.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala Bora na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba amemkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilemela kwenda katika shule hiyo na kufanya tathmini.

“Kama alivyozungumza mheshimiwa mbunge kuna kila sababu ya halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kutenga fedha ili kunusuru na kutengeneza mazingira bora ya wanafunzi hao,” amesema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Bunda Mjini Robert Maboto amehoji ni lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi, Bunda Mjini.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali ilipeleka fedha Halmashauri ya Mji wa Bunda Sh288 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma matano ya sekondari (vyumba vya madarasa manne na maabara moja) na maboma ya shule za msingi ya madarasa 13 na matundu ya vyoo 21, ambayo ujenzi wake umekamilika.

Amesema mwaka 2024/2025, Serikali imetenga fedha Sh125 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya vyumba vya madarasa 10 yaliyopo katika shule za msingi mbalimbali.

Amezitaja shule hizo ni Rubana, Mbugani, Mlimani, Shule shikizi Sazira Mbugani, Butakale, Nyasana, Shule shikizi Ruselu, na Kinyambwiga B, ambapo maboma yatakayosalia yatakuwa 14.

Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha za ukamilishaji wa maboma 14 yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kadri ya upatikanaji wa fedha.