Mbivu, mbichi suala la kikokotoo kujulikana Mei Mosi

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akizungumza wakati wa uhitimishaji wa hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali imeanza kuchukua hatua za kuyafanyia kazi malalamiko dhidi ya kanuni mpya ya kikokotoo cha pensheni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo mara mbili.

Dodoma. Serikali imesema suala la kanuni mpya ya kikokotoo cha pensheni ya wastaafu lina maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na limeanza kufanyiwa kazi, majibu yatajulikana kwenye sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, jijini Arusha.

Hayo yamesema leo Ijumaa Aprili 19, 2024 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi bungeni, alipojibu hoja za wabunge kuhusu suala la kikokotoo.

Wabunge kadhaa leo wameendelea kulalamikia suala la kikokotoo akiwamo mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliyesema kikokotoo ni bomu.

“Nataka nikushauri, jambo la kikokotoo ni bomu, ulipokee kwa heshima na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) naomba unisikilize hapa. Pokea jambo la kikokotoo na Naibu Waziri Mkuu (Dk Doto Biteko) na Naibu Spika (Mussa Azzan Zungu) na Spika (Dk Tulia Ackson), mpelekeeni Mheshimiwa Rais ushauri wa kitaalamu atoe ‘statement’ (tamko) kwa Watanzania, hilo ni bomu,” ni kauli ya Waitara.

Wabunge wengine waliozungumzia suala la kikokotoo ni mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma ambaye alisema matumizi ya kikokotoo kipya yanaenda kutengeneza Taifa lenye watumishi wezi.

Wengine waliochangia ni Ester Bulaya (Viti Maalumu), Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Kasalali Mageni (Sumve) na Florent Kyombo (Nkenge) ambao wote waliitaka Serikali kukaa na wafanyakazi na kuirejesha sheria hiyo bungeni.

Mbunge wa Viti Maalumu anayetokana na vyama vya Wafanyakazi, Jane Jerry ametaka elimu itolewe kwa wafanyakazi.

Hata hivyo, Neema Mwandabila, mbunge wa viti maalumu amesema fedha za mkupuo za asilimia 33 kutoka asilimia 25, zinatosha kwa kuwa ni ongezeko la asilimia nane.

Katambi leo ameliambia Bunge kuwa hatua ni nzuri kwani wameanza kulifanyia kazi kutokana na maelekezo ya Rais Samia na ya Bunge.

“Kwa sasa hatua ni nzuri, Rais aliishatoa maelekezo zaidi ya mara mbili akiwa amekutana na wastaafu wa Jeshi la Polisi, alitoa maagizo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba tufanye tathmini na kuangalia upya na kufanya mapitio kuona hiki kikokotoo cha sasa kama tunaweza kukiboresha zaidi ili wastaafu wasiweze kupata shida,” amesema.

“Tumeshaanza kazi hiyo, lakini hata sheria inatutaka tufanye tathmini kila baada ya miaka mitatu…na sasa tuko kwenye hatua hiyo na tumefanya tafiti nyingi.

“Hatuwezi hata siku moja Serikali kufumba macho wala kuziba masikio katika suala la Watanzania ambao wamefanya kazi ya heshima kwa ajili ya ujenzi wa Taifa hili,” amesema Katambi.

Amesema hilo ni la kisayansi linahitaji utafiti wa kina kuweza kujihakikishia kwanza kuwa na uendelevu wa mifuko, pili katika tija, kuangalia wastaafu waweze kupata fedha na wawe na uhakika wa kulipwa mafao pale wanapostaafu.

“Mimi mwenye nina masilahi, maana nina wazee wangu watatu wanaelekea kustaafu,” amesema Katambi.