Matibabu ya kibingwa na bobezi kupatikana ngazi za msingi

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu,  akizungumza na wananchi waliopo katika Hospitali ya Manispaa ya Iringa (Frelimo),  wakati uzinduzi wa mpango wa  utoaji wa huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 katika ngazi za halmashauri.

Muktasari:

Hospitali za halmashauri 184 katika mikoa 26 nchini zimeanza rasmi kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na bobezi kupitia huduma mkoba za kambi za madaktari. Awali kambi hizo zilifanyika kwenye hospitali za kanda na mkoa pekee.

Iringa. Huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi sasa zimeanza kupatikana katika afya ya msingi, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mpango wa kambi za madaktari bingwa waliosambaa nchi nzima, kutoa matibabu kwenye hospitali zote 184 za halmashauri.

Kwa kawaida, kambi za huduma za madaktari bingwa, zimekuwa zikifanyika katika hospitali za rufaa za kanda au mikoa, huku magonjwa ya aina moja yakiwa ndiyo yanayopata matibabu.

Katika mpango huu, madaktari bingwa watano wa upasuaji wa afya ya uzazi, watoto na watoto wachanga, magonjwa ya ndani pamoja na wale wa ganzi na usingizi, watakuwa wakitoa huduma za kibingwa kwenye hospitali moja ya Halmashauri kwa muda wa siku tano.

Mpango huo unaosimamiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi, itasambazwa katika mikoa 26 nchini.

Akizindua huduma hiyo iitwayo Madaktari Bingwa wa Mama Samia, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema watatoa huduma kwa bei waliyoikuta kwenye hospitali husika, tofauti na madaktari hao wanapofuatwa kwenye hospitali za rufaa wanazozihudumia.

Amesema jumla ya madaktari bingwa 95 wameanza kutoa matibabu hayo leo Jumatatu, Mei 6, 2024 katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma, lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wagonjwa wanaopaswa kwenda kupata matibabu kwenye hospitali za rufaa za mikoa, kanda na Taifa.

“Kwa kila hospitali moja ya halmashauri, madaktari bingwa wa magonjwa matano wanaweka kambi kwa siku tano ili kuwahudumia wagonjwa kwa bei ileile waliyoikuta. Kitu hiki ni kikubwa na niwapongeze madaktari hawa wazalendo ambao wameamua kuwafikia wananchi,” amesema Waziri Ummy.

Amesema ni kweli Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga majengo na kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba,  lakini bila matibabu kwa wagonjwa, haitakuwa imefikia azma yake ya kutoa huduma.

“Kazi ya Rais haitakuwa na maana kama tutabaki kushabikia majengo na vifaa tiba, isipokuwa huduma bora zenye staha kwa wananchi,” amesema Waziri Ummy.

Amesema Serikali ina mpango wa kushusha huduma za kibingwa kwenye hospitali za wilaya na kwa kuanzia, amezitaka Halmashauri kushusha huduma hizo kwenye zahanati na vituo vya afya.

Amesema mbali na kumpunguzia mwananchi mzigo, lengo jingine la huduma hiyo ni kuwasogezea uzoefu madaktari wa ngazi za Halmashauri katika kutoa huduma za kibingwa ili waweze kutatua baadhi ya changamoto, wanapokutana nazo.

Vilevile, amesema huduma hizo za kibingwa zitaambatana na ufunguzi wa wodi maalumu za watoto wachanga, ili kuokoa uhai wao na kupunguza vifo.

Kuhusu bima ya afya kwa wote Waziri Ummy, amesema watasimama kwenye mstari kuhakikisha sheria inafuatwa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Herry James amesema huduma hizo zitawasaidia wananchi kupata matibabu huku akiiomba Serikali isaidie kusambaza mashirika ya lishe kwenye mikoa yenye changamoto ya utapiamlo.

James, amemuomba Waziri Ummy gari kwa ajili ya wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ili iwasaidie katika kutoa huduma za afya.

Wakati huohuo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma,  Mhandisi Gilbert Simiya akizindua mpango huo mkoani humo amesema huduma za kibingwa zitakazo tolewa ni huduma za uzazi, wajawazito na magonjwa ya wanawake.

Pia amezitaja, huduma za afya kwa watoto na watoto wachanga, huduma za upasuaji na mfumo wa mkojo, huduma za usingizi na ganzi, huduma za daktari bingwa magonjwa ya ndani kama vile shinikizo la damu, kisukari na figo.