Matibabu ya figo pigo kwa wagonjwa

Muktasari:

  • Kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa figo kukosa huduma, Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo Tanzania (Nesot), kimependekeza kwa Serikali kuongeza vifaa tiba na unafuu wa gharama katika hospitali za awali ili wananchi kupima afya zao na kutibiwa kwa haraka.

Dodoma. Kati ya wagonjwa 8800 waliogundulika kuwa na ugonjwa wa figo nchini, wagonjwa 3800 ndio wanapata huduma ya kusafisha damu ‘dialysis’ huku 5000 wakikosa huduma hiyo kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Hata hivyo, Serikali imesema imeendelea kuongeza afua za matibabu zikiwemo kusomesha wataalamu, kuboresha huduma za upandikizaji ambayo awali ilikuwa hadi Sh25 milioni lakini sasa inapatikana hadi kwa Sh20 milioni kwa mgonjwa mmoja.

Kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa hao kukosa huduma Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Figo Tanzania (Nesot), kimependekeza kwa Serikali kuongeza vifaa tiba na unafuu wa gharama katika hospitali za awali ili wananchi kupima afya zao na kutibiwa kwa haraka.

Akizungumza katika Kongamano la tisa la chama hicho lililofanyika jana Ijumaa, Novemba 23, 2023 Dodoma, rais wa Nesot, Dk Onesmo Kisanga alisema licha ya kuwepo kwa idadi hiyo ya wagonjwa bado wataalam hawatoshi na kwamba kwa sasa kada hiyo ina madaktari 39, wauguzi 20 huku 10 wakiwa wanaendelea na masomo.

“Sio changamoto ya wataalam tu bali kuna changamoto ya upungufu wa miongozo na sera, kwahiyo kazi yetu ni kuwaunganisha wataalam kujadili na kuja na jibu la pamoja la kuboresha ili kuondoa changamoto kwenye matibabu,” alisema Dk Onesmo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Pascal Ruggajo alisema katika kila wananchi 100, saba wana ugonjwa sugu wa figo.

Profesa Ruggajo alisema ugonjwa wa figo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la juu la damu ambayo nayo yanatajwa kuongezeka.

Hata hivyo, alisema Tanzania ni nchi pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ina programu mbili za upandikizaji figo yaani Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH).

“Tangu kuanzishwa kwa huduma hizo hospitali ya Muhimbili imepandikiza figo kwa wagonjwa 85 kuanzia mwaka 2017 na wagonjwa 35 katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa na kufanya wagonjwa hao kufikia 120,” alisema

Aidha alisema asilimia 85.5 ya wananchi wanatibiwa katika hatua za awali hali inayoashiria kuwa wapo wasiofika ngazi za juu na kwamba hata wale wanaofika ngazi hizo za juu, asilimia 80 ya wagonjwa hao, huwa katika hatua za mwisho za kuhitaji ‘dialysis.’

Ili kuzuia ugonjwa huo mtaalam wa lishe kutoka BMH, Yasinta Luambano alisema ni muhimu kuzingatia ulaji unaofaa na kuacha tabia bwete.

Kwa mujibu wa Yasinta, wananchi wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara, kuepuka kula vyakula vyenye kemikali na kula kiasi ili kuepuka uzito uliopitiliza.

Utafiti huo ulionyesha kuwapo kwa kati ya asilimia nane mpaka 16 ya waathirika wa figo duniani. Utafiti huo unabainisha Tanzania kwenye nafasi ya 54 katika nchi zilizoongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, huku asilimia 1.03 ya wananchi wake, hufariki kila mwaka.