Masaibu ya waokota chupa za plastiki

Muktasari:

  • Shughuli ya kuokota chupa za plastiki imezidi kukua miaka ya hivi karibuni ambapo watu rika tofauti, hasa vijana, wamejiajiri kwenye shughuli hiyo ambayo zamani ilizoeleka kwamba inafanywa na mateja. Hata hivyo, licha ya wengi kujiajiri huko, bado mtazamo wa jamii haujabadilika, jambo linalowaweka hatarini wanaofanya kazi hiyo.

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya watu, njia zao za kutafuta mkate wa kila siku zinaweza pia kuwa za kwenda kaburini.

Simulizi za waokota taka za plastiki zinafichua maisha yao yalivyo hatarini wanapopigania kujipatia riziki kupitia kukusanya taka hizo katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam.

Hakuna anayewaamini. Wanachukuliwa kama wezi waliojificha chini ya mwavuli wa kukusanya taka. Hata hivyo, wanakiri kwamba wanawahitajika kuweka maeneo yao safi.

Baadhi yao wamekumbana na vipigo kutoka kwa watu wanaodai kuibiwa mali zao, hata wakiwa hawana uhakika na madai hayo.

Baadhi yao wameuawa, wengine wamebaki na majeraha makubwa kwa sababu tu ya kuonekana wachafu na kufanya kazi ya kuokota makopo.

Hamis Chinongo, mwokota taka za plastiki huko Kimara Temboni, anasema hakuna mtu anayewaamini popote wanapopita. Anasema watu hawako tayari kukubali kwamba wanafanya kazi zao kama watu wengine.

Anaeleza kuwa siku moja alipigwa mtaani kwa sababu mwanamke alimtuhumu kuwa alimwibia ndoo yake iliyotoweka muda mfupi kabla yeye hajapita. Alijaribu kuthibitisha kuwa hana hatia lakini alinyimwa nafasi hiyo.

“Tunakabiliwa na matatizo makubwa katika kazi hii. Nilikaribia kuuawa kama si mtu mmoja aliyewazuia watu kunipiga. Kusema kweli, sikumuibia ndoo yake, lakini mtu aliyepita kabla yangu huenda aliiba, niliishia kuadhibiwa,” anasema.

Omary Yasin anasema baadhi ya watu wanaamini kwamba mtu yeyote anayekusanya takataka ni mwizi kwa kumtazama tu. Kwa bahati mbaya, anasema, baadhi ya viongozi katika serikali za mitaa hawashughulikii kwa haki masuala hayo yanapowasilishwa kwao.

“Ninakiri kuwa baadhi yetu ni wezi na tunawafahamu. Na hawa hawabebi lundo kubwa la chupa za plastiki kama sisi, wanabeba chache tu kudanganya watu lakini wanatumia mfuko huo kuficha mali za watu.

“Kwa kawaida tunaweka chupa za plastiki kwenye vyandarua kwa sababu vinaonyesha, chochote ndani kinaweza kuonekana kuondoa wasiwasi,” anasema Yasin akiongeza kwamba wanahitaji kutambuliwa katika kile wanachofanya.

Kwa upande wake, Gabriel Mpela anasema kuna baadhi ya mitaa hawapiti kabisa kwa sababu ya matukio ya zamani ya kuteswa na kuuawa kwa marafiki zao. Anaongeza kuwa wanachagua kukusanya chupa za plastiki kando ya barabara ili kuwa salama.

“Nilishuhudia kifo cha rafiki yangu mmoja ambaye alipigwa na kufariki siku moja baadaye. Alikuwa akikusanya taka za plastiki, mwanamke mmoja akapiga mayowe kwamba aliiba nguo zake. Walitafuta hawakuwapata, lakini wakaendelea kumpiga hadi kumuua,” anasimulia.

Wanawake pia hawako salama katika kazi hiyo, wanakabiliwa na changamoto zinazotishia maisha yao kama wanaume. Wanapigwa na kunyanyaswa wanapofanya kazi yao, hata pale ambapo hawakufanya kosa lolote.

“Niliwahi kupita mtaa mmoja hapa Ubungo, akaja mwanamke akanifukuza kwa matusi akilalamika kuwa mali zao zinaibiwa sana, hawatuamini hata kidogo,” anasema Sarah Lyimo, mkusanya taka za plastiki Ubungo.

Hata hivyo, Maryprisca Zephania, mkazi wa Mtaa wa Golani, Kimara anasema waokota makopo wengi ni wezi, wanajifanya wanakusanya chupa lakini wanaficha vitu kwenye viloba vyao wanavyobeba kila wanakokwenda.

“Wengi wa vijana hawa ni watumiaji wa dawa za kulevya, hawajali mali za watu. Wanaiba na kuziuza hata kwa bei nafuu. Hakuna mtu ambaye angependa kuona watu hawa karibu naye,” anafafanua.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Mtaa wa Tabata, Peter Joachim anasema kuokota chupa za plastiki ni kazi kama kazi nyingine yoyote, wanawafahamu watu wanaozikusanya mtaani kwake. Anasema wengi wao si wezi bali ni wachache wanaopita na kuiba.

“Kuna visa vichache vya wizi tunapovikea kwa hawa wakusanya makopo na wanaoiba ni wale watumia dawa za kulevya. Tunawafahamu wakusanya taka hapa Tabata, ni watu wazuri na tunathamini kazi yao,” anasema.