Maofisa wanne TFS mbaroni tuhuma mauaji ya mwananchi

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyamigota Wilayani Geita wakiwa kwenye maziko ya Semeni Hamis aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Geita (TFS), baada ya kukutwa akiokota kuni katika hifadhi ya msitu wa Samina bila kuwa na kibali. Na mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Maofisa wanne wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Geita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mwananchi mmoja kwa kumpiga risasi wakati akiokota kuni bila kibali katika msitu wa Samina uliopo Wilayani humo.

Geita.  Mkazi wa Kijiji cha Nyamigota Wilaya ya Geita, Semeni Hamis (34) amepoteza maisha baada ya kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa askari wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) baada ya kukutwa ndani ya msitu wa Samina akiokota kuni bila kuwa na kibali.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Wilaya ya Geita linawashikilia maofisa maliasili wanne wa TFS kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga risasi mwananchi huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Januari 6, 2024 katika Msitu wa hifadhi wa Samina.

Magembe amesema maofisa hao wanashikiliwa kwa uchunguzi kutokana na kutuhumiwa kujichukulia sheria mkononi kinyume na sheria, sera, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.

Amesema yeye kama kiongozi anayesimamia Serikali na watumsihi waliopo ngazi ya Wilaya hajafurahishwa na kitendo kilichofanywa na kamwe hawezi kufumbia macho jambo hilo.

“Hawa ni watumsihi wenzetu, huyu aliyefanya jambo hili hajatumwa ameamua kujichukilia sheria mkononi, sisi kama viongozi tumekuwa tukiwaelekeza watumishi wote hata kama mtu amekiuka sheria vipo vyombo vya dola vinavyohusika,” amesema.

Diwani wa Kata hiyo, Khadija Said akizungumzia tukio hilo amesema pamoja na kitendo kilichofanywa na mwananchi huyo kuingia hifadhini bila kibali ni kukiuka sharia, lakini sio halali kwa maofisa wa TFS kujichukulia sheria mkononi.

 “Nalaani kitendo kilichofanyika kwa maana siyo kizuri.

“Aliyefanya haya Serikali haijamuagiza ayafanye ingawa kijana huyu aliingia kwenye hifadhi akijua ni kosa, lakini askari alitumia nguvu kubwa kupita kiasi, naungana na wananchi kulaani mauaji haya na nawasihi watii sheria,” amesema Diwani Khadija.

Aidha amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati huu ambao taratibu za kisheria kwa wahusika waliofanya ukatili huo zikiendelea.