Mama lishe Arusha wapewa mbinu kukabiliana na majanga ya moto

Ofisa mwandamizi wa masuala ya jamii na maendeleo ya kiuchumi kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML), Ruth Mharagi akizungumza na  mama lishe kuwaeleza namna ya kukabiliana na majanga ya moto.

Muktasari:

  •  Maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanaendelea jijini Arusha yaliyoanza Aprili 23 yatahitimishwa Mei 1, 2024 siku ya Wafanyakazi Dunia

Arusha. Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), imetoa mafunzo maalumu kwa kinamama lishe wa Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuwaelimisha namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto.

Mafunzo hayo yametolewa juzi Jumatano, Aprili 24, 2024 na Osha katika maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yatakayohitimishwa Mei 1, 2024. Osha ilishirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).

Pia, mama lishe hao walipewa mitungi ya gesi ya kupikia kwa ajili ya kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kisha kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.

 Mkaguzi wa afya ya mazingira ya kazi kutoka Osha, Elizabeth Mtile amewasisitiza kina mama kuzingatia umuhimu wa kufuata sheria na miongozo mbalimbali ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.


“Kauli mbiu yetu inayosema athari za mabadiliko ya tabianchi katika usalama na afya kazini, inalenga kudhibiti majanga na mabadiliko haya ya tabianchi kwa kushirikisha kila kundi kwenye jamii kwani athari hizi zinatugusa sisi sote,” alisema.

 Mmoja wa kina mama lishe hao, Prinsila Kwai aliwashukuru kwa kupatia mafunzo hayo kwa kuwa yanaenda kuwa chachu ya mabadiliko kwao na kwa wale wanaowazunguka.

 “Kwa kweli tunashukuru sana kwa shughuli zetu za kila siku zinahusiana na moto hivyo mafunzo haya yatatusaidia sana namna ya kukabiliana na mlipuko labda wa gesi,” amesema.

Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi amesema wamemua kutoa elimu kwa kina mama hao ili watambue namna ya kupambana na moto majumbani na kuzingatia usalama kwenye maeneo yao ya biashara hasa ikizingatiwa wao ni chanzo kikubwa cha kukutana na watu wengi.

 “Tunawafundisha namna ya kupambana na majanga ya moto kwani shughuli zao za kila siku zinahusiana na masuala ya moto na matumizi ya mkaa na gesi.

 “Lakini pia ni vema kutambua namna gani mabadiliko ya tabianchi yanaathiri watu pia namna tabia zetu binafsi zinavyoweza kuchangia kuachana na ukataji hovyo wa miti,” alisema.

 Amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi, zinamuathiri kila mmoja bila kujali, cheo, mkubwa au mdogo hivyo ni vema kila mmoja kuzingatia matumizi ya nishati safi ili kuondokana na majanga yatokanayo na mabadiliko hayo.

 “Tumeandaa elimu hii kuona namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa sababu ukataji wa miti ukikithiri unasababisha mmonyoko wa ardhi, mafuriko na ongezeko la joto duniani.

 “Matumizi ya mkaa au kuharibu vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kusabababisha athari kwenye mazingira na kusababisha mafuriko hata kwenye maeneo yetu ya uchimbaji,” amesema.

 Ofisa mwandamizi wa masuala ya jamii na maendeleo ya kiuchumi kutoka GGML, Ruth Mharagi amesema katika mafunzo hayo, wamewafundisha kinamama namna salama ya kutumia nishati ya gesi na kuwasisitiza kuondokana na matumizi ya mkaa.

 “Lakini pia kwenye banda letu tumeendelea kupokea wageni wanaopenda kujifunza namna ya kupambana na majanga ya moto kwa sababu asilimia kubwa wanauelewa mdogo namna ya kukabiliana na majanga ya moto majumbani.

 “Watu wengi hawajui njia za awali za kupata msaada wa kuzima moto, sisi tunatoa mafunzo hayo, kuna vifaa vya kawaida ambavyo mama yeyote anavyo nyumbani, mfano ndoo ya maji, taulo, kanga au kitenge vilivyolowekwa kwenye maji, ni vifaa vya kawaida ambavyo unaweza kutumia kuzima moto hivyo tunaendelea kuwaribisha kwenye mabanda yetu,” amesema.