Makamba: Tumetafiti asilimia 30 eneo linalosadikika kuwa na gesi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Serikali imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/23 itachochea shughuli za utafiti wa gesi asilia katika asilimia 70 ya eneo ambalo bado halijafanyiwa tafiti ya rasilimali hiyo. 

Dar es Salaam. Serikali imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/23 itachochea shughuli za utafiti wa gesi asilia katika asilimia 70 ya eneo ambalo bado halijafanyiwa tafiti ya rasilimali hiyo. 

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 11, 2022 mjini Dodoma na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati wa kutia saini makubaliano ya awali katika Mkataba Hodhi (HGA), kati ya Serikali na Kampuni za Shell na Equinor.

Kilichosainiwa ni baadhi ya vipengere vinavyoweka msingi katika maandalizi ya HGA ambayo bado yanaendelea ili kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG).

“Tumegundua futi za ujazo trilioni 57, ni kingi lakini ukilinganisha na nyingine kiwango hiki ni kidogo, Msumbiji jirani zetu wana utajiri wa futi za ujazo trilioni 200, sisi bado kidogo, sababu ni kwamba sisi tumetafiti asilimia 30 tu ya eneo linalosadikika kuwa na gesi,”amesema na kuongeza:


“Kwa maana hiyo tukifufua na kuendeleza shughuli za utafutaji tutapata gesi nyingi zaidi, moja ya malengo ya wizara yetu ni kuanza shughuli hizo katika mwaka ujao wa fedha 2022/23.”

Makamba amesema Tanzania ina jumla ya vitalu 34, vitalu 22 viko tupu huku 12 tu ndio vilivyopo hai na shughuli zinaendelea.

“Kwa hiyo tunaamini mwaka ujao wa fedha na mwaka unaofuatia, pia kutokana na hamasa ya shughuli hii tunaamini tutaongeza hamasa ya wawekezaji kuja kuendelea na tafiti na tutaongeza kiwango cha gesi nchini na uchumi wa gesi utaongezeka,”amesema.