Makalla kama Makonda, naye ataka mdahalo

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Amosi Makalla (katikati) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda (kulia) katika ofisi ndogo za CCM jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Asema sharti uwe unalenga kujadili kwa hoja kuhusu utendaji wa Serikali na mafanikio ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wapinzani wamjibu wakisema isiwe tu kusema bali auitishe.


Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema atakuwa tayari kushiriki mdahalo wowote nchini unaolenga kujadili kwa hoja kuhusu utendaji wa Serikali na mafanikio ya Chama cha Mapinduzi (CCM).


Kauli kama hiyo imewahi kutolewa na mtangulizi wa Makalla katika nafasi hiyo, Paul Makonda ambaye Machi 31, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Januari 14, 2024  Makonda akiwa Unguja Zanzibar, alitaka kufanyike mdahalo wa wazi kati yake na viongozi wa Chadema ili Watanzania wachague ikiwa wataendelea na maandamano au kuchagua maridhiano.

Makalla ametoa kauli hiyo alipokuwa anawatoa hofu wenye wasiwasi na uwezo wake, akisisitiza anaweza kujenga hoja katika mdahalo wowote.

Wenziwe watatu walioteuliwa pamoja naye ni John Mongella, Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Jokate Mwegelo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) na Ally Hapi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Makalla imejibiwa na Mkurugenzi wa Habari, Uhusiano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema akimtaka asiishie kujinadi kuhusu mdahalo, bali auitishe ili wakutane ajenge hizo hoja.

Makalla alieleza hayo jijini Dar es Salaam jana, alipohutubia katika hafla ya mapokezi yake na wajumbe wenzake watatu wa sekretarieti ya CCM walioteuliwa jana na NEC.


Nipo tayari kwa mdahalo

"Nataka niwaeleze nayaelewa majukumu ya nafasi yangu ya mwenezi, maana ninasoma mitandaoni baadhi wananikumbusha majukumu ya mwenezi. Nayaelewa yapo katika Katiba ya CCM,” amesema na kuongeza:

"Nipo tayari kwa mdahalo wa aina yoyote wa kujibu hoja na katika hilo upele umepata mkunaji."


Chadema wamjibu

Wakati Makalla akionyesha utayari huo, Mrema alimtaka mwanasiasa huyo aandae hicho anachokiita mdahalo kisha amwite wajenge hoja.

Alisema kabla hajafikiria kuomba mdahalo na mtu, anapaswa kujua historia yake, akisema yupo tayari hata kesho (leo), iwapo Makalla atauitisha.

“Anataka mdahalo kuhusu nini, anapaswa ajue historia ya mtu anayeomba kufanya naye mdahalo, nipo tayari hata kesho aitishe twende tukashindane kwa hoja,” alisema Mrema.


Kauli ya CUF

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa alieleza kiu yake ya mdahalo huo, akisema unapaswa kuanza na waenezi wa vyama.

Hata hivyo, alisema jambo hilo litawezekana iwapo kutakuwa na ulinzi kwa wanamdahalo ili yasijirudie yaliyomkuta Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

“Warioba aliwahi kupigwa kofi katika mdahalo na mtu huyo aliyempiga hadi leo CCM inamuona anafaa kuwa kiongozi, kwa hiyo mjadala uhusishe ulinzi pia,” alisema.

ACT-Wazalendo

Katibu wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani alisema chama chake kimejipambanua katika siasa za midahalo.

Alieleza wakati wowote kipo tayari kufanya aina hiyo ya siasa kwa kuwa ndiyo msingi wake na ndizo zinazojenga demokrasia ya kweli na ushindani wa hoja.

Alisema kama maneno ya CCM ni uhalisia, Makalla anapaswa kuandaa huo mdahalo kwamba yupo tayari kusimama naye.

“Nipo tayari kushiriki katika mdahalo wowote, asiishie kusema, aandae nitasimama kupambana naye kwa hoja,” alisema Bimani.

Katika hotuba wakati wa mapokezi, Makalla alisema atayatekeleza majukumu yake kwa kuanzia ulipo msingi wa chama hicho, kwa maana kuanzia ngazi ya mashina ili kuwaelimisha wananchi juu ya kuichagua CCM katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo, alisisitiza kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake, Makonda na kuwa atautekeleza wajibu huo ipasavyo.

"Mimi Amos Makalla nimerudi nyumbani mna shaka juu ya hilo, mna shaka na historia yangu? Nimerudi nyumbani mara nyingi nimekuwa nikiwaeleza, nimetokana na CCM," alisema.

Alisema uteuzi wa wajumbe hao uliofanywa na NEC umekamilisha kile alichokiita timu, huku akisisitiza wote wanajuana kutokana na historia zao ndani ya CCM.

Alishauri zifanyike siasa za kistaarabu kwa kuwa ndiyo mwenendo wa Rais Samia.


Ally Hapi

Katibu Mkuu wa Wazazi wa CCM, Ally Hapi alianza kwa kufananisha mabadiliko ya sekretarieti yaliyofanyika na mabadiliko yanayofanywa dakika za mwisho katika mchezo wa soka.

"Sisi wachezaji tunaoingia dakika za majeruhi huwa ni 'super sub', Rais Samia ni kama vile kocha, anapopanga safu ya kwanza inaweka msingi, anapohitaji kiungo mtoa mipira amemwingiza Dk Emmanuel Nchimbi, kuna wale wakumaliza mchezo, ndiyo sisi tulioingia dakika za mwisho," alisema.

Alisema chama hicho hakitakuwa na huruma ya kumwachia yeyote ushindi katika uchaguzi, badala yake kitasimama kuhakikisha kinatafuta na kupata kura za kushinda maeneo yote.

Katika hotuba yake, hakuacha kutupa kijembe kwa vyama vya upinzani, akisema vimekosa shukurani licha ya kuruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara na kupewa ruzuku.

"Wale jamaa wa upande wa pili ambao kazi yao ni kulialia, Rais amewatengenezea mazingira mazuri wanafanya mikutano na wamepata ruzuku, shukurani hawana, niwaambie katika uchaguzi huu CCM haitakuwa na huruma," alisema.

Akijibu hoja hiyo, Mrema alisema kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya wateule wa NEC ya CCM awamu hii wanaishia kuzungumza yasiyoeleweka hivyo  wanapayuka.

Alisisitiza Chadema hakitarajii huruma ya yeyote katika uchaguzi na ushindi wowote utatokana na juhudi zake, kama kinavyoendelea kufanya.

“Kama wanataka kuona kivumbi wasubiri Aprili 20, 2024 ratiba tulishaitangaza tulipotoa Azimio la Mtwara, kwa hiyo wakae tayari kusubiri maandamano mwezi huu. Tulisema tunasimama kupisha wenzetu wa mfungo wa Ramadhani na Kwaresima,” alisema.

Hapi akizungumzia nafasi yake, alisema yeye ndio mlezi wa makundi yote, hivyo atafanya kazi hiyo kuhakikisha anawaandaa vijana na wanawake.

Akijenga hoja hiyo alisisitiza kuwa, hana ugeni katika uongozi ndani ya chama hicho kwa kuwa amewahi kutumika nafasi mbalimbali katika UVCCM.

"Lakini mimi si mgeni, nilikuwa vijana nikaazimwa na Serikali na sasa nimerudi, Waswahili wanasema kisu kimerudi katika ala," amesema.

Amesema utayari wake wa kukitumikia chama hicho na Serikali hauna shaka hata kidogo.

Jambo lingine, amesema anaenda kufanya kazi usiku na mchana na kushirikiana na watendaji wote ili kuifanya jumuiya ya Wazazi isadifu ukubwa wake.

Jokate Mwegelo

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo alisema uteuzi huo umempa fursa ya kuweka historia ndani ya Umoja huo kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya mtendaji mkuu wa jumuiya hiyo.

Ameeleza alikuwa katika viwanja hivyo hivi karibuni chini ya UWT na kwamba anaweka historia nyingine ya kuwa mtendaji pekee aliyetumikia jumuiya mbili za chama hicho.

Jokate amesema vijana wako timamu na wanajua nafasi yao kama walinzi wa viongozi wote na wasaka kura wa CCM.

"Tunatuma salamu kwa wanaowatazama vijana wa CCM wanaosubiri wakosee, vijana wa CCM hatutakosea na hatutafanya makosa, tutashambulia kila kona kuzisaka kura za chama," amesema.

Ameeleza vijana hawatakuwa nyuma katika kushiriki kuwania nafasi za uongozi ndani ya uchaguzi kuanzia wa serikali za mitaa.


John Mongella

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella alisema kwa kuwa Rais Samia ameonyesha uvumilivu katika siasa, ni muhimu nao wakafuata mwendo huo.

Lakini, alisema iwapo atatokea atakayefanya siasa kinyume cha mwendo huo, CCM kuna wataalamu wa kutosha wa mambo hayo.

Alisema asitarajiwe kuonekana zaidi kwenye majukwaa kwa kuwa nafasi yake ni kusimamia utendaji ndani ya chama hicho.

"Kama mtu ana akili timamu baada ya kumsikia Jokate, Hapi, Gavu na Makalla maana yake muziki umeanza. Kama kuna mtu alikuwa hamwelewi Rais Samia hii safu ni ujumbe tosha," amesema.

Amewakabidhi jukumu vijana wa chama hicho, kuhakikisha viongozi wa Serikali wanalindwa.

"Mimi nakumbuka enzi zetu vijana tulipiga marufuku watu kutishwa, vijana ndiyo walinzi wa chama," alisema.