Majaliwa awapigia debe wazawa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), kuwapa zabuni wahandisi wazawa katika miradi ya ujenzi wa barabara ili kuongeza ufanisi wao.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), kuwapa zabuni wahandisi wazawa katika miradi ya ujenzi wa barabara ili kuongeza ufanisi wao.

Kauli hiyo ya Majaliwa inalenga kuimarisha uwezo wa wahandisi wazawa nchini kusimamia miradi na kadri watakavyoimarika, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) nayo itajenga imani na kuwapa zabuni kubwa.

Maelekezo ya Majaliwa yalitokana na kauli ya Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandatasi, Wakili Menye Manga aliyesema bado kuna ushiriki mdogo wa wahandisi wa ndani katika miradi nchini.

Majaliwa alitoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam jana, alipohutubia ufunguzi wa mkutano wa 20 wa Maadhimishi ya Siku ya Wahandisi nchini.

"Tarura mnapaswa kuanza kuwapa wahandisi wa Tanzania kazi ya ujenzi wa barabara kilometa chache na baadaye watahamia kwenye zile kubwa, hili litawezekana hebu tuanze," alisema.

Pamoja na hayo, Majaliwa aliitaka ufanisi wa wahandisi wa Tanzania wanapoaminiwa kutekeleza mradi mbalimbali.
Alisisitiza kauli yake hiyo akitolea mfano mmoja wa miradi waliyopewa Watanzania ambao baadaye waliishia kusambaratika.

"Wameanza vizuri kazi lakini baadaye wakasambaratika na ukiangalia nini kimewasambaratisha ni yale malipo ya awali," alisema.

Kitendo kama hicho, Majaliwa alisema kinaashiria uwezo duni wa wahandisi wa Tanzania katika kusimamia miradi, akisisitiza wanapaswa kubadilika.

Katika hotuba yake hiyo, aliitaka Wizara ya Ujenzi kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miradi inayoendelea.

Pia Majaliwa alitaka wahandisi wanawake waandaliwe mafunzo ya kuendelezwa huku Wizara ya Ujenzi ikiagizwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwaendeleza wahandisi wahitimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Wakili Manga alisema ushiriki wa wahandisi wa Tanzania pamoja na kampuni zao katika miradi nchini ni mdogo licha ya kuwa kinara katika ukuaji wa maendeleo hasa ya miundombinu.

Hata hivyo, alisema ipo miradi ambayo ingeweza kusimamiwa na kampuni za ndani, lakini wanapewa wahandisi wa nje licha ya kuwa na uwezo sawa na wazawa.

"Mikakati ya kufikia shabaha hiyo ni kuongeza ujuzi wa kitaaluma na tunaendelea kufanya hivyo kujenga uwezo na ukuaji wa teknolojia," alisema.

Kuhusu mkutano huo, alisema matarajio ni kutoka na maazimio yatakayowasilishwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

"Tutakuwa na mabadiliko katika sheria na kanuni zetu ili kuongeza usajili zaidi wa wahandisi," alisema Manga.

Katika hafla hiyo jumla ya wahandisi 200 walitarajiwa kula kiapo cha kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na kuzingatia maadili ya kazi ya uhandisi.

"Kiapo watakachokula leo ni cha maisha anaapa kutekeleza majukumu yake ya kihandisi kwa maadili muda wote," alisema.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema Tanzania ina wahandisi 36,709 kati yao wanawake ni 4,653 sawa na asilimia 13.

Alisema kunahitajika kuwa na wahandisi wengi zaidi na mafundi sanifu.

Kwa kutambua shughuli za kihandisi, alisema katika mwaka wa fedha 2002/03 Serikali ilianzisha programu ya kuwashikiza wahandisi wahitimu kwenye miradi.

Kila mwaka wizara ya ujenzi hutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza hilo.