Majaliwa ataka wateule wa Rais kusimamia haki

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya kuandaa mikakati na  utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande.

Muktasari:

Waziri mkuu amesisitiza kwamba utashi wa Rais katika kuboresha mfumo wa utoaji wa haki jinai, lazima udhihirike kwa viongozi hao walioko karibu na wananchi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  amewataka wakuu wa mikoa kuyasimamia na kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.

Aidha,  amesisitiza kwamba ni lazima viongozi na watendaji wa Serikali wawe na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na kuyatekeleza mapendekezo hayo.

Waziri Mkuu amebainisha hayo leo Mei 6, 2024 wakati akifungua warsha ya kuwajengea uelewa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhusu maboresho kwenye mfumo wa haki jinai na utoaji wa haki nchini.

Amesema malalamiko ya wananchi katika masuala kadhaa ndiyo yaliyoweka msukumo kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Haki Jinai na kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo na hatimaye kuigeuza kuwa kamati ya kuandaa mikakati utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Miongoni mwa malalamiko hayo ni utungaji wa baadhi ya sheria ndogo katika mamlaka za mikoa ambazo aghalabu hukinzana na sheria mama.

“Mfano ni tozo zinazoanzishwa na halmashauri kama vile ushuru wa mabango, kodi za maegesho na usimamizi wa matumizi ya maeneo ya barabara zinasababisha mkanganyiko kwa wananchi kwa kuwajibishwa na chombo zaidi ya kimoja,” amesema Waziri Mkuu,

Masuala mengine yaliyolalamikiwa ni migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya madaraka ya ukamataji pamoja na utamaduni wa wakuu wa mikoa na wilaya kuambatana na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama katika ziara mbalimbali hata zile zisizohitaji uwepo wa vyombo hivyo.

Jambo hilo limeelezwa kuwa limekuwa likisababisha hofu kwa wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa viongozi hao.

"Kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wa Rais katika maeneo yenu ya utawala, ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa azma yake (Rais) inatimia kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai,” amesisitiza.

Waziri mkuu amesisitiza kwamba utashi wa Rais katika kuboresha mfumo wa utoaji wa Haki Jinai lazima udhihirike kwa viongozi hao walioko karibu na wananchi.

"Hata hivyo, utashi huo hauwezi kudhihirika kwenu iwapo hamtakuwa na nia ya dhati ya kubadilika na kisha kuongoza mabadiliko kwenye maeneo mnayomwakilisha Rais hususan katika kuwahudumia wananchi,” amesema.

Waziri mkuu amesisitiza kuwa ni lazima viongozi na watendaji wa Serikali kuwa na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na kuyatekeleza mapendekezo hayo.

Pia ametaka viongozi hao wa mikoa wazingatie uwepo wa majengo na miundombinu muhimu kwa ajili ya taasisi za Haki Jinai katika maeneo mapya ya utawala  yaliyoanzishwa.

“Kuna maeneo mengi mapya ya utawala ambayo bado huduma za Haki Jinai kama vile vituo vya Polisi na magereza hazijafika na wananchi wanapata tabu sana kuzifikia huduma hizo katika wilaya mama ikiwemo kutembea au kusafiri kwa muda mrefu,” amesisitiza.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi, Dk Festo Dugange,  amesema watasimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yatakayotolewa katika warsha hiyo ili dhamira ya Rais ya kutaka kuona wananchi wanapata haki zao inatimia.

Kwa upande Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema kamati yao iliundwa ili kufanyia kazi ripoti ya tume iliyokuwa na mapendekezo 333 ya maboresho ya utendaji kazi wa taasisi za haki jinai katika maeneo mbalimbali.

Amesema takwimu zinaonesha matukio ya uhalifu nchini yanaongezeka kila mwaka huku juhudi kubwa zinaelekezwa kupambana na uhalifu badala ya kubaini na kuuzuia.

“Moja ya majukumu tuliyopewa kwenye kamati hii ni kuandaa mkakati wa kitaifa wa kubaini na kuzuia uhalifu unaotarajiwa kuwa nyenzo ya utekelezaji wa taasisi na mamlaka zote zinazohusika ili kukabiliana na janga la uhalifu nchini,”amesemaa.