Magufuli aikagua ndege ya Serikali, atoa agizo kwa bosi wa ATCL

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkurugenzi wa ATCL Ladislaus Matindi wakati wa Ukaguzi wa ndege hiyo aina ya Foker 50

Muktasari:

  • Leo Alhamis, Rais wa Tanzania, John Magufuli ametembelea hanga la matengenezo ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo kwa mkurugenzi mkuu wa ATCL

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi kuhakikisha fedha zote zilizoanza kutolewa kwa ajili ya kuipeleka ndege ya Serikali nje ya nchi kuipaka rangi zinarejeshwa haraka.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Alhamisi Machi 28, 2019 alipotembelea hanga la matengenezo ya ndege la ATCL katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukagua marekebisho ya ndege ya Serikali aina ya Foker 50 ambayo inabadilishwa matumizi ili itumike kusafirisha abiria kama zinavyotumika ndege nyingine za ATCL.

Taarifa  iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema katika ziara hiyo ya kushtukiza, Rais Magufuli ameshuhudia kazi ya ufungaji wa viti 48 vya abiria ukiwa umekamilika na mafundi wa kupaka rangi wakiwa wanakamilisha kuchora picha ya mnyama Twiga anayetumiwa kama nembo ya ndege za ATCL.

“Rais Magufuli ameelezwa kuwa kazi ya marekebisho ya ndege hiyo imechukua siku saba na mafundi wanakabidhi ndege leo, tayari kwa matumizi,” imeeleza taarifa hiyo.

“Pia, Rais Magufuli ameagiza mafundi sita  waliofanya kazi ya upakaji rangi ya ndege hiyo kwa makubaliano ya kulipwa Sh2 milioni waongezwe fedha nyingine Sh10 milioni kama motisha ya kuonyesha moyo wa uzalendo, kufanya kazi kwa wakati na kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetoa kwa ajili ya kupeleka ndege Afrika Kusini,” taarifa imemnukuu Rais.

Mapema leo asubuhi akipokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha viongozi na watendaji wa Serikali kutaka kupeleka ndege hiyo Afrika Kusini ili ikabadilishwe rangi ambako ingegharimu zaidi ya Sh328 milioni badala ya kazi hiyo kufanyika nchini.

Rais Magufuli amesema alilazimika kuingilia kati mchakato huo na kuagiza marekebisho hayo ikiwamo kupaka rangi za ATCL yafanyike nchini, kazi hiyo imefanikiwa kwa gharama ya Sh7 milioni ikilinganishwa na Sh328 milioni iwapo ingepelekwa Afrika Kusini.

Akitoa maelezo kwa Rais Magufuli, Matindi amekiri iwapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini marekebisho yangegharimu muda usiopungua siku 14 na gharama zingekuwa siyo chini ya Sh328 milioni na amemhakikishia fedha zilizotolewa zimerejeshwa.

Mkurugenzi mkuu huyo ameongeza baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo ATCL inatarajia kuwa ndege hiyo itaanza mara moja kutoa huduma za usafiri wa anga katika kituo cha Mtwara na kufuatiwa na Iringa, Mpanda na baadaye Songea, Pemba na Tanga.

Desemba 23, 2018 wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya ATCL aina ya Airbus A220-300 jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliagiza ndege mbili za Serikali (Foker 50 na Foker 28) zilizokuwa zikitumiwa na viongozi zibadilishwe matumizi ikiwamo kupakwa rangi ya shirika hilo ili zitumiwe na Watanzania wote.