Maadhimisho siku ya wakunga duniani: Wakunga waainisha mapendekezo saba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wakunga wawili waliopewa vyeti vya pongezi kutokana na  huduma walizozitoa wakati wa maafa, ambao ni  Anenyise Makyao kutoka Rufiji   na Theodora Nakei kutoka Hanang mkoani Manyara (walioshika vyeti).

Muktasari:

  • Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wakunga, Chama cha Wakunga Tanzania (Tama) kimekuja na mapendekezo saba ili kuboresha fani hiyo ikiwemo kutambuliwa rasmi.

Dar es Salaam. Chama cha Wakunga Tanzania (Tama) kimetoa mapendekezo saba kwa Serikali ili kuboresha fani hiyo.

Miongoni mwa mapendekezo waliyotoa ni kuwezesha wakunga kutoa huduma wakati wa maafa, ukunga kutambuliwa rasmi katika utumishi, kuongeza idadi ya wakunga katika vituo vya afya hasa zahanati na kutoa elimu ya mabadiliko tabianchi.

Wameyasema hayo leo Mei 5, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Wakunga Duniani yaliyoratibiwa na Tama kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) yaliyobebwa na kauli mbiu isemayo ‘wakunga ni suluhisho muhimu kwa mabadiliko ya tabianchi’.

Akisoma salamu za Tama, Rais Mteule Dk Beatrice Mwilike amesema umefika wakati sasa Serikali kutengeneza mfumo maalumu, utakaowawezesha wakunga kuhudumia wakina mama na watoto wachanga wakati wa maafa.

“Ni muhimu kuwa na mikakati endelevu na madhubuti kuwawezesha wakunga kuwafikia waathirika pindi inapohitajika na kukabiliana na hali, mikakati hiyo inawezekana kupitia elimu, kuwa na mifumo ya tahadhari na kuwalinda watoa huduma na wapokea huduma,” amesema Dk Beatrice.

Hilo litawezekana kupitia kuwajengea uelewa wakunga kuhusu suala zima la mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwenye afya ya uzazi, jinsi ya kuwahudumia waathirika na kuzuia matatizo yatokanayo na athari hizo.

Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa kufuatia mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na ongezeko kubwa la joto nchini, huku tafiti mbalimbali zilizofanyika zikionyesha kuwa linaweza kuathiri kusababisha mimba kuharibika au mama kujifungua kabla ya wakati na hivyo kuathiri mtoto atakayezaliwa.

“Hivyo kama wakunga tunapaswa kuwa na uelewa mpana wa mabadiliko ya tabianchi ili tuweze kupanga na kutoa huduma kufuatana na athari za mabadiliko hayo. Tukumbuke kuwa ujauzito, uchungu na kujifungua havijui maafa,” amesema Dk Beatrice.

Lakini ili matokeo chanya yapatikane katika kuhudumia wajawazito, chama hicho kimeomba kuongezwa idadi ya wakunga katika vituo vya kutolea huduma, kwa kutoa ajira mahususi kwa wakunga wanaomaliza mafunzo na kuhitimu. “Pia Serikali iboreshe zaidi mazingira ya kutolea huduma kwa wakunga kuwa na nyumba karibu na vituo vyao vya kazi, ikizingatiwa kuwa huduma zao zinahitajika saa 24 na wakati mwingine ni za dharura,” amesema.

Kuhusu kuzalisha wahitimu wabobezi, Rais wa Tama amesisitiza umuhimu wa kuanzisha mafunzo ya walimu wa ukunga ili kuhakikisha kuwa wahitimu wa kada hiyo wanatoka na ujuzi na stadi za kutosha.

Dk Beatrice pia amesema kutambua taaluma ya ukunga katika mfumo wa utumishi wa umma kwani wakunga wakihitimu bado wanaajiriwa kwa cheo cha Ofisa Muuguzi ambayo inapunguza morali ya kufanya kazi.

“Pia walipwe mishahara na marupurupu mengine kulingana na ngazi zao za elimu hasa kuanzia ngazi ya wakunga wabobezi,” amesema Dk Beatrice.

Akijibia hoja hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mapendekezo yaliyotolewa na Tama yatafanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa, ili kuboresha utendaji kazi wa wakunga ambao alibainisha kuwa ni watu muhimu nchini.

“Serikali imeweka juhudi katika kuwanunulia vifaa vyote vitakavyowawekea urahisi, katika kufanya kazi ikiwemo magari ya kubebea wagonjwa na nyie mnapata nafasi ya kwenda na wagonjwa sehemu ambazo amepata rufaa,” amesema Majaliwa.

Katika kukabiliana na ufinyu wa wakunga, Majaliwa amesema anatambua changamoto ya upungufu wa watumishi hao kwenye vituo vya afya jambo ambalo linafanya mkunga mmoja kuhudumia wagonjwa 20 na zaidi, ikilinganishwa na kiwango cha Shirika la Afya Duniani (WHO) la wagonjwa wanne kwa mtumishi mmoja.

“Serikali inatambua kuwa wakunga wanatoa huduma nyingi zaidi ya kuhudumia wajawazito, ambao wamejifungua na watoto wachanga, lakini pia wamekuwa wakishiriki katika chanjo, kliniki za watoto wa miaka mitano, Serikali inaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha inakabiliana na suala hili ikiwemo kutoa ajira kwa watumishi wa afya,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ametumia nafasi hiyo kuitaka Wizara ya Afya kufuatilia kwa karibu kukamilisha muundo wa utumishi ili kada ya ukunga wapate stahiki zao na kunufaika.  

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wanakwenda kuangalia namna ya kuanzisha stashahada za ukunga, ili kuwawezesha wahitimu kufanya kazi yao iliyokusudiwa ya kuhudumia   wajawazito pekee.

“Kama Serikali tunakubaliana na nyie kuwa ipo haja ya kuongeza idadi ya wakunga, si kusema muuguzi mkunga hapana, kama ni mkunga ni mkunga, kama ni muuguzi ni muuguzi ili kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuimarisha uzazi salama,” amesema Ummy.

Kwa upande wake, Mwakilishi mkaazi wa UNFPA Tanzania, Melissa McNeil-Barrett amesema wataendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha kila ujauzito unathaminiwa, kila uzazi ni salama na kila malengo ya kijana yanafikiwa.