Kortini wakidaiwa kuiba lita 400 za mafuta ya transfoma

Mshtakiwa Stephano Njau ( mwenye fulana nyeupe) akiwa na Praygod Kimaro katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shitaka la wizi wa lita 400 za  mafuta ya transfoma.

Muktasari:

  • Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Desemba Mosi, 2023 na Februari 2024 katika eneo la Ubungo Kibangu.

Dar es Salaam. Dereva wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Stephano Njau (34) na mfanyabiashara Praygod Kimaro(48), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka mawili  likiwemo la kukutwa na lita 400 za mafuta ya Transfoma, mali ya shirika hilo.

Wanadaiwa kuwa baada ya kuiba mafuta hayo, waliyaweka dukani na kuanza kuyauza, wakati wakijua ni kosa kisheria.

Washtakiwa hao, ambao wote ni wakazi wa Kimara, wamefikishwa Mahakama hapo, leo Aprili 23, 2024 na kusomewa mashitaka yao na wakili wa Serikali, Adolf Verandumi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Kabate amedai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 10558/2024.

Akiwasomea mashitaka hayo, amedai katika shitaka la kwanza, linakomkabili mshtakiwa Kimaro pekee yake, anadaiwa kukutwa na mali ya wizi, kinyume cha sheria.

Kimaro amedaiwa kati ya Desemba Mosi, 2023 na Februari 2024 katika eneo la Ubungo Kibangu, mshtakiwa alikutwa dukani kwake akiwa na lita 400 za mafuta ya Transfoma yenye thamani ya Sh4 milioni, mali ya Tanesco.

Shitaka la pili ni wizi akiwa mtumishi wa umma, linamkabili mshtakiwa Njau pekee yake, ambapo imedaiwa kati ya Desemba Mosi, 2023 na Februari 2024 katika duka lililopo Ubungo Kibangu, aliiba lita 400 za mafuta ya Transfoma.

Imedaiwa katika kipindi hicho na eneo hilo, Njau akiwa dereva wa Tanesco, aliiba lita hizo za mafuta zenye thamani ya Sh4 milioni, mali ya mwajiri wake.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashitaka hayo, walikana.

Hata hivyo, upande wa mashitaka waliifahamisha mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kupitia wakili washtakiwa  Henry Sechu, ameiomba mahakama hiyo kuwapa wateja wake dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Kabate ametoa masharti ya dhamana ambapo kila mshtakiwa alitakiwa awe na mdhamini mmoja wenye barua kutoka taasisi inayotambuliwa kisheria, awe na kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Vilevile wadhamini hao wanatakiwa kusaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 22, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana na wapo nje kwa dhamana.