Kesi ya meno ya tembo: Mke afungwa miaka 20, kulipa faini ya Sh22 bilioni

Vipande wa meno ya tembo. Picha na maktaba

Muktasari:

  • Leonida, ambaye ni mkazi wa Kimara Stop Over, Dar es Salaam anatumikia adhabu hiyo pamoja na mumewe, Peter Kabi baada ya kutiwa hatiani kwa kukutwa na meno ya tembo 210 sawa na wastani wa tembo 93 waliouawa.

Dar es Salaam. Siku ya kufa nyani miti yote huteleza, usemi huu unaweza kutumika kuelezea harakati za Leonida Kabi kujinasua na kifungo cha miaka 20 na faini ya Sh22 bilioni kwa makosa ya ujangili kufika mwisho katika milango ya Mahakama.

Juni 27,2012, Leonida na mumewe Peter Kabi waliokuwa wakiishi Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam walikamatwa na meno ya tembo 210 na vipande vitano vya mifupa ya tembo yenye uzito wa kilo 450, nyara zote hizo zikiwa na thamani ya Sh2.2 bilioni, ambapo Mahakama imeongeza thamani yake mara 10 na kufikia Sh22 bilioni.

Kulingana na ushahidi uliotolewa idadi hiyo ya meno ni sawa na tembo 93 waliuawa.

Mwaka 2017, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikawahukumu Leonida na mumewe Peter Kabi, kutumikia kifungo cha miaka 15 kila mmoja kwa kosa la kwanza na miaka 20 jela kwa kosa la pili na la tatu, ambapo  adhabu hizo ziliamriwa zitumike kwa pamoja.

Hawakuridhika na hukumu hiyo na wakakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo ilitoa hukumu yake Julai 13,2018 na kubariki kutiwa kwao hatiani, isipokuwa ikabadili kifungo kwa kosa la pili na tatu kutoka miaka 20 jela hadi kuwa miaka 25 jela.

Halikadhalika katika kupigania haki yao, walikata tena rufaa Mahakama ya rufaa ambayo Januari 26, 2022, kupitia kwa jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Barke Sehel na Zephrine Galeba, walifuta adhabu ya miaka 15 waliyopewa kwa kosa la kwanza.

Hata hivyo, jopo hilo la majaji lilishusha kifungo cha miaka 25 kwa kosa la pili na la tatu na kurudisha kifungo cha miaka 20 jela lakini, ikaamuru pia walipe faini ambayo ni mara 10 ya thamani ya nyara za Serikali ambazo walikutwa nazo Oktoba 27,2012.

Inaonekana baada ya hukumu hiyo, mumewe alikata tamaa lakini Leonida akaamua kubisha tena hodi Mahakama ya rufaa na safari hii si kwa rufaa tena kwani alishafika mwisho kisheria, bali safari hii akiiomba ipitie upya maamuzi yake ya Januari 26, 2022.

Hata hivyo, mbele ya jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Abraham Mwampashi na Zainab Muruke, Mahakama ya rufani katika uamuzi wake iliyoutoa Mei 7,2024, imetupilia mbali maombi hayo ya marejeo ikisema sababu zake hazina mashiko.

Maelezo ya kosa lilivyotendeka

Ushahidi wa upande wa mashitaka unaeleza kuwa siku ya tukio Oktoba 27,2012, polisi walipokea taarifa fiche kwamba wawili hao walikuwa wameficha mali za wizi nyumbani kwao, ambapo walikwenda nyumbani kwao Kimara Stop Over kufuatilia.

Shahidi wa kwanza, Inspekta Emael Shilla akiwa na polisi wenzake, walipofika nyumbani hapo walimkuta Leonida na baada ya kufanya upekuzi katika nyumba ya mbele, walifanikiwa kupata mali hizo zilizodhaniwa kuwa zilipatikana kwa njia ya wizi.

Polisi walienda katika nyumba ya wafanyakazi (servant quarter) ambapo walibaini chumba kimoja kikiwa kimefungwa na walipomtaka Leonida awape funguo, aliwaambia kuwa alikuwa nazo mumewe ambaye hakuwepo nyumbani.

Baadaye polisi walifanikiwa kupata funguo na kukifungua na katika kupekua chumba hicho, timu hiyo ya upekuzi ilibaini meno ya tembo na mifupa kwenye  mifuko ya sandarusi ikiwa imefunikwa na bendera ya Taifa na hapo Leonida alipoteza fahamu.

Baada ya kuhesabu na kupata idadi ya meno hayo, walijaza hati ya utaifishaji (seizure note) ambayo ilitiwa saini na mashahidi wote akiwemo shahidi wa tatu, Happiness Nshunju na Leonida na baadaye Leonida alipelekwa kituo cha Polisi Mbezi.

Kipindi hicho kutoka hapo nyumbani na wakiwa kituo cha Polisi Mbezi, Leonida alikuwa akiendelea kuwasiliana na mumewe, lakini baadaye alijitokeza aliyekuwa mshitakiwa wa tatu kituoni hapo na kukamatwa ingawa hata hivyo aliachiwa na Mahakama.

Shahidi wa nne ambaye ni Ofisa wanyamapori kutoka kikosi cha kupambana na ujangili Mkoa wa Pwani, alieleza alivyokwenda kituo cha Polisi Oysterbay ambako nyara hizo zilihamishiwa na katika kuhesabu walipata meno 210 na vipande vitano vya mifupa.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, nyara hizo zilikuwa na thamani ya Dola 365,000 za Marekani ambazo ni sawa na Sh2,206,610,000 na ripoti yake ilipokelewa kama kielelezo.

Utetezi wao kortini ulivyokuwa

Katika utetezi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, washtakiwa wote walikana mashitaka ambapo Peter Kabi alikana kufahamu lolote kuhusiana na meno hayo licha ya kwamba yalipatikana nyumbani kwake wakati akiwa hayupo.

Kuhusiana na mali za wizi zilizopatikana nyumbani kwake, Kabi alijitetea kuwa zilihifadhiwa nyumbani kwake kama dhamana ya fedha ambazo alikuwa amemkopesha mmiliki wa mali hizo ili aweze kununua dawa kwa ajili ya baba yake mgonjwa.

Kwa upande wake, Leonida alikiri kweli kuwapo nyumbani Oktoba 27,2012 wakati maofisa wa Polisi walipofika nyumbani kwao na pia alikiri ni kweli kuwa baada ya upekuzi wa polisi kulipatikana mali hizo zilizokuwa zinadaiwa kuwa ni za wizi.

Baada ya mali hizo kupatikana, zilijazwa katika karatasi na maofisa wa polisi na kushuhudiwa na majirani zake waliokuwepo na akaeleza kuwa mmoja wa maofisa wa polisi aitwaye Ndege alimdhalilisha kwa kumuita kuwa ni mwizi huku akimpiga.

Alieleza kuwa ni kutokana na hilo, alidondoka chini na kupoteza fahamu na alipopata fahamu alisaini karatasi na kupelekwa kituo cha Polisi Mbezi na kuwekwa mahabusu hadi Oktoba 28,2012 alipopelekwa kituo cha Oysterbay na baadaye mahakamani.

Katika utetezi wake huo, alisema kabla ya kupelekwa mahakamani, Oktoba 29,2012 alitolewa mahabusu na kupandishwa  katika gari aina ya Landcruicer lililokuwa na meno ya tembo na kupelekwa mbele ya Kamanda wa Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova.

RPC Kova alimuonyesha mbele ya wanahabari ambao walimpiga picha akiwa na meno hayo na akatoa kipande cha gazeti la Habari Leo na Nipashe vilivyokuwa na picha yake kuhusiana na tukio hilo, ikimuonyesha akiwa na shehena hiyo ya meno ya tembo.

Pamoja na utetezi wao huo, mahakama iliwatia hatiani na kumwachia mshtakiwa wa tatu kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Kizingiti cha mwisho kortini

Baada ya rufaa yao katika Mahakama ya rufani ambayo ndio ya juu na ya mwisho kugonga mwamba na kuongezewa faini mara 10 ya thamani ya nyara za Serikali walizokutwa nazo, Leonida alijaribu tena kupigania haki kwa mlango mwingine.

Safari hii alifungua maoni ya jinai akiomba mahakama hiyo ya rufaa iifanyie marejeo hukumu yao akiegemea sababu mbili kuu, moja hukumu yao ilifikiwa kwa kuegemea makosa ya wazi kwa sura ya kisheria, kwani kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni.

Leonida alisema kama mahakama ya rufani ingekuwa imeona makosa hayo ya upande wa mashitaka, basi ingempa faida yeye na hoja ya pili ni kuwa alinyimwa kimakosa haki ya kusikilizwa kwa utetezi wake, kwani haukuzingatiwa na mahakama.

Hata hivyo, mbele ya jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Abraham Mwampashi na Zainab Muruke, mahakama ya rufani katika uamuzi wake iliyoutoa Mei 7,2024, imetupilia mbali maombi hayo ya marejeo ikisema sababu zake hazina mashiko.

Majaji hao walisema kwa kupitia kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo, wameridhika kuwa ushahidi wa utetezi wa Leonida ulizingatiwa na kukataliwa kwa utetezi wake hakumaanishi kwamba mahakama haikuzingatia katika kutoa hukumu.

Kutokana na hukumu hiyo sasa ukizingatia katika Mahakama ya Rufani ilishasikiliza rufaa yake na kuitupa kabla ya Leonida kufungua maombi ya marejeo ambayo nayo yametupwa, anasubiri huruma ya Rais kutokana na mamlaka ya kikatiba aliyonayo.

Madaraka ya Rais ya kumsamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia ya kosa lolote lile, la jinai yamo katika ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005.

Ibara hiyo inatamka kuwa: ”bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yeyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.