Karatu wahamisha wanaoishi mabondeni

Mwonekano wa baadhi ya nyumba zikiwa zimezingirwa na kujaa maji katika eneo la Gyekrum lililopo Kata ya Qurus, wilayani Karatu Mkoa wa Arusha kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Muktasari:

  • Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali wilayani Karatu Mkoa wa Arusha, nyumba nyingi zimezingirwa na maji na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa kazi.

Arusha. Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha imeendelea kuwahamisha wananchi wanaoishi mabondeni na kuwapeleka maeneo maalumu yaliyotengwa, ili kuepukana na athari za maafa ya mafuriko.

 Jana, halmashauri hiyo ilifanya vikao vya Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC) katika kata zote wilayani humo, ili kutambua maeneo yaliyoathirika na mvua zinzoendelea kunyesha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Aprili 20, 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Dk John Lucian amesema wanaendelea kuwaondoa wananchi wanaoishi mabondeni, ili wasikumbe na athari za mafuriko.

“Kwa sasa tuko kwenye hatua ya kuwatambua waathirika wa mafuriko katika kata zote na kupitia vikao vya dharura vya WDC vilivyofanyika maeneo yote jana, tumetaka tupate taarifa ya jumla, kisha tutaipeleka kwa mkuu wa wilaya ambaye ataiwasilisha kwa mkuu wa mkoa,” amesema.

“Tumewaondoa watu wanaoishi maeneo ya mabondeni na kuwapeleka sehemu maalumu, ikiwemo Shule ya Msingi Bwawani, wengine wameenda kwa ndugu na jamaa zao, tuliona kama halmshauri tuanze kwa kutambua walioathirika,” amesema na kuongeza;

“Karatu mjini ambayo baadhi ya nyumba zao zimejaa maji, tumewatengea maeneo ya kuhamia kwa muda, ila vijijini kuna nafuu kidogo.”

Mvua hizo zilizonyesha tangu wiki iliyopita zimeathiri maeneo mbalimbali wilayani humo, ikiwemo Kata ya Qurus na Karatu.

Awali, wakizungumza na Mwananchi Digital Aprili 16, 2024, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kwa haraka, kabla madhara hayajawa makubwa.

Jeneth Mfanga, mkazi wa Bwawani amesema amelazimika kwenda kupanga kutokana na nyumba yake kujaa maji.

Amesema mvua hiyo iliyoanza kunyesha tangu wiki iliyopita imeleta athari kubwa kwao, kwani mbali na nyumba yake kujaa maji, pia saluni aliyokuwa anaitegemea kama kitega uchumi nayo imejaa maji na amefanikiwa kuokoa vifaa vichache.

Maeneo mengine mkoani Arusha tangu wiki iliyopita yaliyopata chanagmoto ya mafuriko ni pamoja na lile la Kisongo ambalo mali ziliharibika ikiwemo mazao, maeneo ya biashara kujaa maji na matope yaliingia kwenye nyumba na kusababisha familia nyingi kukosa makazi.

Pia Wilaya ya Arusha ilipata athari baada ya gari la Shule ya Msingi ya Ghati Memorial kutumbukia kwenye korongo na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane na msamaria mwema mmoja aliyekuwa akijaribu kuwaokoa wanafunzi hao.