JKCI kufuatilia hali za wagonjwa wa moyo kidijitali

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge akionyesha kifaa aina ya Dozee ambacho hutumika kupima kiasi cha oksijeni ya mgonjwa, shinikizo la damu kinapoweka chini ya shuka kwenye kitanda anacholalila mgonjwa.

Muktasari:

  • JKCI kwa kutumia kifaatiba inatoa huduma kwa wagonjwa wakiwa majumbani.

Dar es Salaam. Ujio wa kifaa maalumu kinachoweza kusaidia kutoa taarifa ya maendeleo ya wagonjwa wa moyo ‘dozee’ wawapo nyumbani, unatajwa kupunguza gharama za huduma na muda kwa wagonjwa wawapo hospitalini.

Kifaa hicho kinasaidia wagonjwa kupata mwendelezo wa matibabu wakiwa nyumbani, huku Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ikiweza kuwafuatilia kidijitali.

Kifaa hicho kinachouzwa Dola mbili za Marekani (Sh5,190) huwekwa chini ya shuka kwenye kitanda cha mgonjwa, kikifanya kazi ya kupima mapigo ya moyo, oksijeni ya mgonjwa, shinikizo la damu na kutoa taarifa kwa daktari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2024, Mkurugenzi JKCI, Dk Peter Kisenge amesema wanatangaza kifaa hicho baada ya wagonjwa watano kupatiwa huduma wakiwa nyumbani walipotoka hospitalini walipofanyiwa  operesheni.

Dk Kisenge amesema hayo alipotangaza huduma ya kufuatilia mwenendo wa wagonjwa wakiwa nyumbani iliyoanzishwa, ikitajwa kupunguza gharama za wagonjwa wanazotumia wanapokuwa hospitalini.

Amesema huduma hiyo itasaidia kupunguza muda kwa wagonjwa kulazwa hospitalini.

“Mtu akishafanyiwa upasuaji wakati mwingine alilazimika kukaa zaidi ya siku 10 ili tumuangalie ,lakini sasa anaweza kukaa siku nne, halafu akaendelea kufuatiliwa akiwa nyumbani ambapo  tunaweza kupata taarifa zote muhimu tunazohitaji kuzifahamu,” amesema Dk Kisenge.

Amesema kuwahi kurudi nyumbani kwa wagonjwa kutafanya taasisi hiyo kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi, hasa katika kipindi ambacho magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka.

Magonjwa ya moyo ni kati ya yale yasiyoambukiza ambayo takwimu zinatajwa kuongezeka kila mwaka.

Septemba 29, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya JKCI Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema takwimu za wizara kupitia Mtuha (DHIS -2) zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu pekee, kutoka wagonjwa milioni 2.5 mwaka 2017 hadi wagonjwa milioni 3.4 mwaka 2022.

Mbali na kuwapo kwa ongezeko hilo, Dk Kisenge amesema uwepo wa huduma hiyo utasaidia kupunguza vifo vya ghafla ambavyo vimekuwa vikiwakumba wagonjwa, kwani watakuwa na uwezo wa kuhudumiwa kwa haraka

“Mtu akiweka kifaa hiki katika kitanda anacholalia yeye peke yake, kama presha itapanda tunaweza kumwambia muuguzi au ndugu aliye karibu afanye nini ili kuishusha, kama imeshuka tunaweza kumwelekeza nini afanye ili ikae sawa,” amesema Dk Kisenge.

Amesema hilo pia linaweza kufanyika ikiwa oksijeni ya mgonjwa imeshuka, kwani pindi taarifa itakapotumwa kwao itakuwa ni rahisi hatua za haraka kuchukuliwa.

“Mgonjwa akizidiwa na kuwahi hospitalini gharama zinakuwa ndogo tofauti na akichelewa, pia akipata mshtuko wa ghafla wa moyo kadri unavyochelewa kumuhudumia moyo unachoka, ukichoka gharama kubwa zitatumika,” amesema Dk Kisenge.

Amesema katika taarifa  zinazotumwa, wakati mwingine miongoni mwa huduma zinazoweza kufanyika ni mgonjwa kutakiwa kuwahishwa hospitali kwa mujibu wa taarifa za vipimo vitakavyoonyesha, au daktari kufika kumhudumia.

“Hii ni teknolojia ambayo wenzetu India tayari wanaitumia na sisi tumeileta nchini. Tutaanza na Dar es Salaam na baadaye itakwenda maeneo tofauti nchini baada ya madaktari kufundishwa kwa mujibu wa taratibu ili kusaidia kuona wagonjwa sehemu zote,” amesema.

Ni ahueni

Ibrahim Timane, aliyewahi kusumbuliwa na tatizo la moyo na kulazimika kuhudhuria kliniki kila mwezi amesema: "Haikuwa rahisi, kila mapigo ya moyo yalipokuwa yanaenda kwa haraka nilihisi kuna shida imeibuka tena."

Timane mkazi wa Tabata, Dar es Salaam amesema miaka kama sita nyuma akiwa mkoani Dodoma kikazi alihisi mwili uko tofauti, mapigo ya moyo yanaenda kasi hivyo akalazimika kwenda hospitali kupimwa na kubainika ni kweli moyo wake una shida.

"Nilianzishiwa dozi ya mwezi mzima, kwa kuwa Dodoma nilikuwa kikazi, daktari aliyenihudumia aliniambia nikirudi Dar es Salaam, baada ya kuwa nimemaliza dozi niende kliniki JKCI.”

"Katika kipindi chote cha dozi sikuwa sawa kiakili, nikihisi mapigo kwenda kasi basi mawazo yananijia tofauti. Huwezi kurudi hospitali kwa kuwa niliambiwa hadi mwezi nikimaliza dozi, baada ya dozi na kufanyiwa vipimo nikabainika nimepona," amesema Timane.

Timane amesema kifaa hicho kitakuwa msaada kwa wagonjwa.

Mbali na wagonjwa kuona ahueni, baadhi ya waliowahi kuhudumia wagonjwa hospitalini hapo wakiwa hawana ndugu ndani ya Jiji la Dar es Salaam wameeleza unafuu wake.

“Ninachotamani huduma ianze kutolewa hadi mikoani, nilimuuguza mdogo wangu hapo hospitalini, Dar es Salaam sina ndugu, mwanzoni nilikuwa nalala nyumba za wageni hela ikaisha gharama zikaongezeka mara mbili.”

“Ni tofauti na angekuwa nyumbani, gharama ingekuwa ndogo, kama ni kitanda ni cha nyumbani, kula tunakula kama kawaida, labda tutalipia tu muuguzi au daktari atakapokuja,” amesema Annastazia.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI, Smita Bhalia amesema huduma hiyo inalenga kutoa mwendelezo kwa wagonjwa waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Amesema itawasaidia kupata wauguzi au madaktari watakaokuwa wakifuatilia hali zao ikiwamo kufanyiwa usafi wa vidonda vyao kama wamefanyiwa upasuaji.

“Gharama zinatofautiana kulingana na hali ya mgonjwa husika kwa sababu kuna wengine wanahitaji uangalizi wa saa 24,” amesema Dk Bhalia akifafanua kwamba inaweza kufikia Sh100,000.