Jaji asema weledi na uadilifu unahitajika mashauri ya wanyamapori

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Imeelezwa kuwa, kutokana na uzito wa uendeshaji wa mashauri ya ujangili wa wanyamapori, majaji, mahakimu na waendesha mashitaka wametakiwa kuwa waadilifu na weledi

Lushoto. Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) cha Lushoto mkoani Tanga, Dk Paul Kihwelo amesema weledi na uadilifu unahitajika katika kushughulikia mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ukiwemo ujangili.

Jaji Kihwelo amesema hayo Aprili 22, 2024 wakati akifungua mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ukiwamo ujangili yakihusisha wadau wa haki jinai 160 chuoni hapo.

Mafunzo hayo yatakayochukua wiki mbili mpaka Mei 5, 2024 yanaendeshwa na IJA kwa ufadhili wa taasisi isiyo ya kiserikali ya PAMS Foundation inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori.

Wengine waliopo kwenye mafunzo hayo ni majaji wa Mahakama Kuu, mahakimu, waendesha mashtaka  na wapelelezi wa ngazi mbalimbali kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Tanga.

 “Mashauri ya makosa dhidi ya ujangili na misitu yana changamoto kubwa sana, kwa sababu haya makosa yanagusa uchumi wa Taifa na ni makosa ya kimataifa, hivyo ili watu waweze kuamua mashauri hayo kwa wakati na inavyostahili, ni vema wawe na uelewa wa kutosha.

“Ni matarajio yetu baada ya mafunzo haya kutakuwa na uboreshaji mkubwa katika kukabiliana na makosa haya,” amesema Dk Kihwelo.

Pia, Jaji Kihwelo ametoa wito maofisa wote wanaopatiwa mafunzo hayo na wengineo kushughulikia mashauri ya makosa ya wanyamapori kwa weledi na uadilifu pamoja na kuongozwa na dhamira zinazojali masilahi mapana ya Taifa.

Samson Kasaala ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa PAMS Foundation, amesema wamefadhili mafunzo hayo ili kuhakikisha wadau hao wanaboresha uweledi katika utendaji kazi na kukabiliana na makosa ya mashauri ya wanyamapori.

“Niwaombe wadau hao wawe na weledi na kutenda haki, kuhakikisha kesi zote zinasikilizwa kwa haki na hukumu zinakuwa za haki, kwa sababu wao wana wajibu wa kulinda mali zetu ambazo ni sehemu muhimu ya uchumi kama utalii,” amesema. 

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni majaji wa Mahakama Kuu, waendesha mashita kutoka Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, maofisa kutoka Jeshi la Polisi na mnamlaka mbalimbali zinazojihusisha na upelelezi pamoja na uhifadhi wa maliasili.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwamo Ofisa Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa) Kanda ya Arusha, Matika Chacha amesema mafunzo hayo yatasaidia kuboresha upelelezi hivyo kupatikana kwa ushahidi mzuri utakaowezesha kuwajibishwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi ya Wanyamapori na makosa ya misitu.

 Ofisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kaskazini, Zayana Mrisho amesema kuwa mafunzo hayo yatawasadia kupata uelewa mpana juu ya taratibu bora za ukamataji wa wahalifu na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani bila kuathiri mwenendo mzima wa tukio zima.

Tayari makundi matatu ya mafunzo hayo yamekwishafanyika katika mikoa ya Morogoro, Katavi na Iringa huku awamu ya tano ikitarajiwa kufanyika wilayani Tarime Mkoa wa Mara Mei mwaka huu.

Hadi kumalizika kwa mafunzo, jumla ya washiriki 785 watakuwa wamepatiwa elimu hiyo.