Jafo: Hoja ya kuingia Zanzibar kwa pasipoti ni kurudi nyuma

Wabunge wakimpongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo, baada ya bajeti ya wizara yake kupitishwa na Bunge.

Muktasari:

  • Bunge lapitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Dodoma.  Bunge limepitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Waziri mwenye dhamana, Dk Selemani Jafo akisema hoja ya kutaka kurejesha utaratibu wa watu wa Tanzania Bara kuingia Zanzibar kwa pasipoti ni kujirudisha nyuma.

Jafo amesema hayo leo Jumanne Aprili 23, 2024 akitoa majumuisho ya jumla kuhusu hoja za wabunge zilizotokana na mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

“Kaka yangu pale alipozungumza kwamba, kwa nini watu wasiingie na pasipoti Zanzibar, nikasema aah! kaka wazo zuri lakini unataka kuturudisha nyuma.”

“Katika mchakato huu Serikali ya awamu ya pili chini ya hayati Mzee Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) wakati kule Serikali iliyokuwa chini ya Rais Dk Salmin Amour, kipindi kile walikuwa wanajadili, jambo hili lilitoka kipindi hicho likaonekana linaleta usumbufu,” amesema Dk Jafo.

“Hivi mtu leo mtani wangu Gwajima (mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima) atoke Kawe akienda kule Zanzibar atafute pasipoti, tutarudi nyuma sana, na hii si makusudio ya Muungano wetu,” amesema.

Hoja ya kurejesha pasipoti Zanzibar ilitolewa na  mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa aliyesema Rais wa kwanza hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa ana akili sana na kwamba haamini kama alizidiwa maarifa na Rais Sheikh Abeid Amani Karume kwa kusema Zanzibar watu waingie kwa utaratibu.

“Kwa nini waliweka pasipoti visiwa vile vinahitaji kulindwa, mimi sikubaliani na suala la kutovilinda visiwa. Sasa hivi Zanzibar imejaa watu na tunavyoendelea hawatakuwa na sehemu ya kuishi,” amesema.

Amesema anahitaji hati za kusafiria zirudi ili kuwe na ulindaji wa watu wanaoingia Zanzibar.

“Sasa hivi ukienda pale Zanzibar utakuta viwanja vimechukuliwa, miti imekatwa, kulikuwa na zao la mikarafuu haliko tena, imebakia Pemba tu na kule Pemba linaenda kuisha, minazi hakuna sasa hivi tunaagiza nazi kutoka Mafia,” amesema.

Chupa za rangi

Kuhusu chupa za rangi za viwandani Jafo amesema:  “Tumefanya kikao na wadu wote kuhusu chupa zile za rangi, wazalishaji wote wa vinywaji viwandani wamekubali kila mzalishaji wa kiwandani kanuni tumetengeneza pamoja, kanuni hiyo itakuwa kwenye gazeti la Serikali muda si mrefu.”

“Mchakato wake unaendelea kila mwenye kiwanda mwenye chupa ya plastiki ana jukumu la kuhakikisha haionekani kwa mujibu wa kanuni na sheria,” amesema.

Jafo amesema suala la usafi ni jambo linalokera, akitoa mfano wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kwenye barabara ya mabasi yaendayo haraka licha ya kujengwa vizuri, kuna takataka nyingi zimetupwa.

Amesema suala la usafi ni jukumu la Serikali za mitaa na wameelekezwa wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kwenye maeneo yao.

Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ililiomba Bunge kuidhinisha Sh62.67 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/2025, fedha ambazo zimeidhinishwa.