Hidaya chapoteza nguvu baada ya kuingia Mafia

Muktasari:

  • TMA imesema kimbunga hicho kimekosa nguvu, mabaki ya mawingu yaliyokuwa yameambatana na kimbunga hicho yamesambaratika.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia mwendelezo wa taarifa zake kuhusu kimbunga Hidaya imesema kimekosa nguvu baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia.

Taarifa hiyo imetolewa jana Jumamosi Mei 4, 2024 saa 5.59 usiku.

"Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa wa kilichokuwa kimbunga Hidaya zilizokuwa zikitolewa na TMA tangu Mei 1, 2024, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita, kimbunga Hidaya kimepoteza kabisa nguvu baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia," imesema taarifa hiyo.

Pia, taarifa imesema mabaki ya mawingu yaliyokuwa yameambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo mbalimbali ukanda wa kusini hususani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro, hivyo hakuna tena tishio la kimbunga Hidaya.

TMA ilianza kutoa tahadhari ya kimbunga hicho tangu Mei 1, 2024 kilikuwa na mwendokasi wa kilomita 130 kwa saa kabla hakijapungua nguvu.

Hii ni mara ya pili ndani ya miaka minne vimbunga kupungua nguvu vikiwa vinaingia nchini.


 Aprili 25, 2021 kimbunga Jobo kilipoingia Pwani ya Bahari ya Hindi kilipungua nguvu na kutoweka.

Kuhusu kimbunga Hidaya

Taarifa ya TMA iliyotolewa Ijumaa Mei 3, 2024 iliitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua kubwa na kimbunga hicho kuwa ni Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Unguja.

Huku mikoa mingine ya Ruvuma, Kigoma, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simuyu, Mara, Arusha, Manyara Kilimanjaro, Pwani, Morogoro, Tanga na mikoa ya Pemba ikitarajiwa kupata mvua kubwa kama athari ya kimbunga hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 3, 2024 Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema kimbunga hicho kiliendelea kupungua kasi na huenda ndani ya saa 12 zijazo kitakuwa kimepungua zaidi, huku akiitaja mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa imekwishaanza kupata athari.

“Lakini pia madhara ya kimbunga hicho yameanza kuonekana kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kwani kumekuwepo na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali unaovuma kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa,” alisema Matinyi.