Hatua kwa hatua 'Boni yai' na Malisa kizimbani

Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha taarufa za uongo. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob  na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X(zamani Twitter ) na Instagram, kinyume cha sheria.

Jacob maarufu kama 'Boni Yai', mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Msakuzi amefikishwa mahakamani hapo kujibu mashtaka yanayomkabili.

Mbali na Jacob, mshtakiwa wa pili ni Ofisa afya ya jamii na mwanaharakati, Godlisten Malisa mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Washtakia hao wamefikishwa Mahakamani hapo leo, Jumatatu Mei 6, 2024 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali,  Neema Moshi akishirikiana na Happy Mwakanyamale, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.

Wakili Moshi amedai kuwa washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya jinai namba 11805/2024.

Wakili huyo amedai washtakiwa wameshatakiwa makosa yao, chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Akiwasomea mashtaka yao, Moshi amedai kuwa kati ya mashtaka hayo matatu, mashtaka mawili yanamkabili Jacob peke yake huku shtaka moja ndio likimkabili Malisa.

Amedai katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuchapisha taarifa za uongo kinyume cha sheria linalomkabili mshtakiwa Jacob pekee yake, inadaiwa Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam, huku akijua na kwa nia ovu ya kuipotosha jamii, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika kama ifuatavyo

"WENYE LESENI YA KUUA WAMEUA TENA kijana wetu Robert Mlanga Mushi maarufu kama Babu G amekutwa HOSPITALI YA KILWA ROAD akiwa AMEUAWA.

Imagine tumetoa taarifa Jeshi la Polisi la kupotelewa kwa kijana wetu, cha ajabu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam likawa linatusaidia kumtafuta pia.

Kila siku Jeshi la Polisi linasema halijapata taarifa wala fununu zozote za kijana wetu na kwamba tuwe wavumilivu, wanapambana kuendelea kumtafuta. Jana machale yakawacheza ndugu wa kijana, baada ya msiri mmoja kuwatonya ndugu " nendeni hospitali ya Polisi Kilwa Road mkachungulie vyumba vya kuhifadhia maiti"

Ndugu walivyokwenda huko hospitali ya Polisi Kilwa Road wakamkuta kijana wao akiwa ameuawa, wahusika wa hospitali wanadai maiti ililetwa tangu tarehe 10 Aprili 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.

Maiti ina siku 12 hospitali ya Polisi Kilwa Road bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi waliopeleka maiti ni wa nchi gani? Walipoombwa kujua ni askari wa kituo gani na majina yao ni yapi, wahusika wa hospitali hiyo ya Polisi wanadai hawajui na wanaomba wasitajwe ... wacha wanyonge tukazike maiti yetu, sitamani kuona hata ndugu wakiomba uchunguzi dhidi ya maiti yao, kwa sababu hata mtoto mdogo anajua hapo MUUAJI NI " TAPE" ile kufunga mtu miguu, kufunga mikono kisha kumpigwa ‘tape’ ya mdomo na puani hadi kifo baada ya ile mbinu ya kupeleka msituni/ porini na kupiga risasi kujulikana Dar es Salaam ina mtu mmoja katili sana."

Shtaka la pili, ni kuchapisha taarifa za uongo kinyume cha sheria linalomkabili pia Jacob, ambapo mshtakiwa huyo anadaiwa Machi 19, 2024 katika jiji la Dar es Salaam, kwa nia ovu ya kuupotosha umma, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii  wa X  wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika  kama ifuatavyo:

"MAUAJI ARUSHA, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Omari Msamo ameuawa baada ya kusimamishwa na kushushiwa kipigo kizito kilichopelekea kutoa uhai wake na Polisi wa usalama barabarani baada kutuhumiwa kuendesha gari akiwa ametumia kilevi, Jeshi la Polisi linatumia kila jitihada kuzuia vyombo vya habari kuripoti tukio hili kama njia ya kuficha na kuwanusuru askari wake dhidhi ya mkono wa sheria".

Shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, ambapo mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.

Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, mshtakiwa alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii wa Instagram wenye jina la Malisagj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka:   " Tarehe 13 Aprili,  Meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024.

Inadaiwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa Polisi maeneo ya Kariakoo na baada ya hapo hawakuonekana tena ... leo wakaambiwa "nendeni Hospitali ya Polisi Kilwa Road, ndugu yenu amefichwa mochwari pale" wakaenda.

La haula! wakamkuta Robert akiwa kwenye jokofu la baridi. Hakuwa Robert tena bali ni mwili wake ukiwa na majeraha ya kipigo.

Ni mauaji ya kikatili Masikini Robert hajawahi kuwa na ugomvi na mtu kwa nini utendewe haya."

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, walikana kutenda makosa hayo.

Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa maelezo ya awali.

Wakili Peter Kibatala na Dickson Matata wanaowatetea washtakiwa hao, wameomba mahakama iwape dhamana wateja wao kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

"Tunaiomba mahakama yako iwape wateja wetu masharti nafuu ambayo wataweza kudhaminika kwa sababu washtakiwa hao wameonyesha uaminifu kwa kwenda kuripoti polisi bila shida" alidai Kibataka.

Pia wameomba kupatiwa nakala ya hati ya mashtaka pamoja na maelezo yao na Hakimu Swallo alikubaliana na ombi la upande wa utetezi na kueleza kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika na hivyo kutoa masharti ya dhamana.

Hakimu Swallo amesema kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao saini fungu la dhamana la Sh2milioni kila mmoja.

Pia wadhamini hao wawe na nakala ya kitambulisho cha Taifa (Nida) na wawe na barua kutoka taasisi zinazotambulika kisheria.

Hakimu Swallo baada ya kutoa masharti hayo ya dhamana.

Wakili Kibatala aliiomba mahakama iwape ahirisho fupi ili waweze kuwasiliana na wadhamini ambao hawakuwepo mahakamani hapo kwa wakati huo.

"Mheshimiwa hakimu, naomba mahakama yako itupe ahirisho fupi ili tuweze kuwasiliana na wadhamini kwa sababu hatukujua kama washtakiwa hawa wataletwa Mahakamani, kwa sababu asubuhi washtakiwa walienda kuripoti Polisi na walipofika huko ndio wakachukuliwa na kuleta hapa mahakamani hivyo hata ndugu hawana taarifa kama wameletwa mahakamani hapa " alidai Kibataka.

"Na hii tunajitahidi ndani ya muda wa mahakama tuwe tumeleta wadhamini hapa mahakamani kwa sababu hata mimi nilikiwa sijui kama wameletwa mahakamanai hawa kina Jacob" amedai Kibatala.

Hakimu Swallo alikubaliana ombi la Kibatala na kuahirisha kesi hiyo kwa muda, huku akiwaelekeza wadhamini hao wapelekwe kabla ya muda wa mahakama kuisha.

Hata hivyo, saa tisa na nusu washtakiwa hao walipandishwa tena kizimbani kwa ajili ya kupata dhamana baada ya ndugu zao kuja kuwawekea dhamana.

Baada ya kukamilisha masharti ya dhamana, mahakama hiyo imepanga kesi hiyo kuitwa Juni 6, 2024 na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.