Hatari kwa wanandoa kufichana mali, fedha

Muktasari:

  • Kwa muktadha wa kisheria, ikitokea mhusika akipoteza maisha upo uwezekano mkubwa wa mali hizo kupotea au kuangukia kwenye mikono ya watu wasio sahihi.

Dar es Salaam. Wakati wimbi la ndoa kuvunjika likiendelea kutikisa kwenye jamii, tahadhari imetolewa kwa wanandoa wanaowaficha wenza wao kuhusu mali wanazomiliki kwa kuhofia kuachana.

Kwa muktadha wa kisheria, ikitokea mhusika akipoteza maisha upo uwezekano mkubwa wa mali hizo kupotea au kuangukia kwenye mikono ya watu wasio sahihi.

Tahadhari hii imekuja kufuatia ongezeko la migogoro dhidi ya wenza ambayo chanzo chake ni kufichana mali, huku kukiwepo na wanaotaka kuficha mali zao kwa majina ya watu wengine kwa hofu ya kugawana pale ndoa itakapovunjika.

Akizungumza na Mwananchi, wakili Bashir Yakubu amesema utamaduni huu umeanza kushika kasi nchini, huku wanawake walioko kwenye ndoa wakiongoza kwa tabia hiyo, hasa kununua mali, ikiwemo ardhi, nyumba au hata biashara bila kuwashirikisha waume zao.

“Haya mambo yanafanywa na pande zote, ila kwa upande wangu nimekutana na kesi nyingi za wanawake, kinachoonekana wengi huandika mali kwa majina ya ndugu zao na hili linafanyika ili kuondoa uwezekano wa mume wake kupata umiliki wa moja kwa moja wa mali husika.

“Wapo wengine wanaoandika hizo mali kwa majina yao, inaweza kuwa ardhi, nyumba au biashara lakini wanaficha kiasi kwamba mwenza wake au hata watoto wake inakuwa vigumu kujua au kuifikia ilipo na kwa muktadha huu kuna viwanja, nyumba hata fedha benki ambazo hazina wenyewe,” amesema Yakubu.

Wakili huyo anafafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, jina linaloandikwa kwenye mali ndilo linalotambulika kama mmiliki wa mali husika, hivyo hata ikitokea mmiliki halali amefariki ghafla bila kuweka wazi kuhusu mali hiyo, hakuna kinachoweza kubadilika isipokuwa kwa busara za aliyeandikwa.

“Ukimuandika ndugu halafu ikatokea umekufa ghafla itategemea busara za yule uliyemuandika kama ataguswa kuweka wazi kuhusu makubaliano hayo, kinyume na hapo mali inakuwa imepotea. Halafu inawezekana uliyemuandika ndiye akatangulia kufa, utawezaje kuwaaminisha watu wake wa karibu, ikiwemo familia kuwa hiyo mali ni yako wakati ipo kwenye jina lake”.

Anachoeleza Yakub ni mfano halisi wa kisa kilichomkuta Lawrence Mnubi, kijana huyu amepoteza mali za urithi alizoachiwa na baba yake kufuatia kutoweka kwa mtu mwenye taarifa za kina kuhusu mali hizo.

Amesimulia, “Wazazi wangu walitengana nikiwa na miaka mitatu nikawa naishi na mama, nilipofikisha miaka mitano baba alinikutanisha na mwanasheria wake ambaye anafahamu kwa kina kuhusu mali zake ambazo hakuzifahamu mama yangu wala mwanamke mwingine aliyemuoa.

“Wakati baba yuko hai kuna wakati aliniambia kwamba kwa kuwa mimi ni mtoto wake wa kiume pekee ameniandikisha kwenye nyumba mbili na taarifa zote anazo huyo mwanasheria na hakuwahi kumueleza chochote mke aliyekuwa akiishi naye,” amesema na kuongeza

“Miaka mingi ikapita, baba yangu amefariki dunia mwaka jana, yule mtu alikuja msibani na kunikumbusha kwamba ana taarifa ya mali za baba hivyo nimtafute baada ya kumaliza msiba, nilifanya hivyo, lakini hadi sasa ni zaidi ya miezi 10 sijampata. Namba za simu alizonipa hazipatikani na amehamisha ofisi, naona wazi nimezipoteza hizo mali”.

Anasema baada ya kufuatilia kwa kina ndani ya familia akagundua hakuna mtu mwingine yeyote anayefahamu kuhusu mali hizo zaidi ya mwanasheria huyo ambaye hadi sasa hajui atampata vipi.


Wasemavyo watu

Nestory Masawe, mkazi wa Buza amesema wanaume hufikia hatua hiyo kama hawana imani na wake zao, hivyo kwao uamuzi sahihi ni kutoweka wazi baadhi ya vitu wanavyovimiliki.

“Haya mambo ni kutokana na kushuhudia mikasa ya aina hii kwenye jamii, hawa wanawake zetu wengine wapo kwa ajili ya maslahi na unaona kabisa mawazo yake ni kwenye mali. Anakuta umeshajitafuta unamuoa mnaishi kidogo, mkiachana anataka mgawo sawa, sasa ili kuepusha hasara unaona bora vitu vyako vingine asivifahamu,” ameeleza  Masawe.

Wakati Masawe akieleza hayo, Regina Mshana, mkazi wa Vikindu amesema kuna muda mwanamke inamlazimu kujiongeza, hasa anapoona mienendo ya mume wake haieleweki.

“Si kwamba unakuwa na lengo la kuficha ila kuna wakati kwenye ndoa unakutana na mazingira yanayokufanya ufikirie kujipanga kimaisha, tunashuhudia ndoa zikivunjika na mara nyingi wanaopata shida ni wanawake, sasa ili kujiwekeza salama mtu anaona ni heri awe na kitegauchumi au hata mali ambayo inaweza kumfaa baadaye.

“Ni kweli kabisa katika mazingira hayo unaona ni heri uwashirikishe ndugu zako au marafiki zako, ingawa sina uhakika kama wengine wanafikia hatua ya kuandika majina ya ndugu ili kuficha mali,” amesema Regina.


Nini kinasababisha hali hii?

Wakili Yakub anasema mara nyingi haya yanafanywa na wanandoa wanaoishi kwa kuviziana, kila mmoja akiwa na mawazo kuwa muda wowote ndoa itavunjika, hivyo hapaswi kufanya uwekezaji mkubwa ndani ya taasisi hiyo.

“Changamoto tuliyonayo sasa ni wanandoa kuviziana, kila mmoja anakuwa tayari kusubiri lolote litokee, ndiyo maana mtu anaona nikiweka mali hapa ikitokea la kutokea itatambulika ya pamoja hivyo lazima kuwepo mgawo.

“Kingine ni kutoaminiana, halafu pia wanawake wengi huwa wanaamini waume zao hawana haki ya kumiliki mali zao iwe wakiwa hai au hata ikitokea wamekufa, yaani mwanamke anaona ni heri mali aiandike jina la mama, kaka au dada yake, lakini sio kuiweka katika mazingira ambayo yanaweza kumnufaisha mume wake.”

Mhadhiri wa saikolojia Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Christian Bwaya amesema kwa kiasi kikubwa tabia hii inachangiwa na malezi aliyolelewa mtu, anakuwa katika msingi unaoamini kwamba usalama wake ni kuficha alichonacho.

Amesema wazazi wenye misimamo mikali kupindukia, wanaowatisha watoto kwa kufikiri tofauti, wanaoadhibu watoto kwa kuwa wakweli, wanatengeneza tatizo la mtoto kujijengea ukuta na kuona ni salama kuishi maisha yake.

Kwa mujibu wa Bwaya, mtoto wa aina hii akifikia umri wa kuingia kwenye uhusiano na hatimaye ndoa anaweza kupata wakati mgumu kuweka wazi mambo yake.

Sababu nyingine inayochangia usiri wa aina hii ni tabia ya mwenza ambapo mwanasaikolojia huyu anabainisha kuwa kuna uwezekano mtu akalazimika kumficha mwenza wake kutokana na mwenendo wake.

“Kabla hujalalamika kuwa unafichwa, jiulize unaaminika? Unapoona mwenzako anakuficha sana, inawezekana tatizo likawa kwako. Hujamfanya ajisikie salama vya kutosha, aone hata akiwa wazi kwako hatakuwa amejiweka kwenye hatari. Huwa inaanza na vitu vidogo vidogo.

“Unaambiwa kitu unawaka na kumshambulia mwenzako. Unashirikishwa kitu husikilizi, unakosoa na kuonesha mwenzako hajui. Ukiendelea na tabia hiyo unashangaa mwenzako anaanza kujitenga na wewe na kufanya vitu vyake kimyakimya. Pia kuna zile tabia za upendeleo,” amesema.

Anafafanua kuwa upendeleo huu ni ile hali ya kuwapa kipaumbele ndugu zako kuliko mweza wako, hili likifanyika kwa uwazi ni mwanzo wa kutengeneza tatizo kubwa.

“Mwenzako anaanza kuona usalama wake ni kukuficha vitu vya muhimu ili usivipeleke kwa ndugu zako. Inaanza hivyo, baadaye unashangaa mtu anafanya vitu vikubwa bila kukuambia. Bahati mbaya huwa tunalalamikia matokeo na hatujiulizi tumechangiaje mtu kutuficha”.

Bwaya anaeleza kuwa sababu nyingine ya usiri ni matokeo ya makosa ambayo mwenza mmoja amewahi kuyafanya kwa mwenzie na hakutafuta njia zozote za kupata suluhu, inaweza kumfanya ajihami kwa kufanya vitu kivyake vyake.

“Uliwahi kumfanyia mwenzako kitu na hukuonesha majuto wala kuchukua hatua za kujirekebisha. Hamkuongea mkamaliza na ukaona yameisha kumbe mwenzako bado alihitaji mfikie mahali ajihakikishie kuwa umebadilika. Huyu anaweza kuwa msiri kujihami na uwezekano wa wewe kurudia tabia zako”.

Athari za kisaikolojia

Mwanasaikolojia huyo anabainisha kuwa usiri unazorotesha ukaribu kwenye uhusiano, kwa kile anachoeleza kuwa ni vigumu kuwa karibu na mtu unayejua anakuficha vitu.

Usiri pia unapunguza kuaminiana na kuna namna mnakuwa hamfikii kwenye ule ukaribu unaohitajika kustawisha mahusiano yenu.

“Hali hii ikiendelea mnakuwa mnatengeneza mzunguko wa kutokuaminiana, usiri zaidi na kadhalika. Migogoro mingi kwenye ndoa inakuwa kwenye mzunguko huo.

“Matokeo yake ni watu kuwa kwenye ndoa, wanazungumza, lakini hawana mahusiano ya kina. Kila mtu ana maisha yake ya siri na watu wengine. Kilele chake ni mtu kuwa na siri na wazazi wake, rafiki zake ambazo mwenzake wa ndoa hazijui.”


Suluhisho ni lipi?

Kuhusu nini kifanyike kukabiliana na hali hii endapo itajitokeza kwa wanandoa, Bwaya anasema inategemea na hatua ya siri yenyewe.

Amesema kama ipo kwenye hatua za awali, ikiwemo kufichana vitu vidogo vidogo, wenza wanapaswa kubadili mwenendo na kila mmoja kuwajibika kumfanya mwenzie ajihisi yuko salama kumuelezea vitu vyake.

“Usiwe mtu wa kumshambulia kwa sababu tu amekuambia kitu usichokipenda. Pia, anza wewe kuwa wazi. Kama unataka akuambie kipato chake, mwambie kipato chako. Ukitaka akushirikishe mipango yake, anza kumshirikisha mipango yako kidogo kidogo.

“Wengine ni wasiri kama namna ya kulipiza kisasi. Omba msamaha na mtengeneze mambo yenu. Kwa hatua ya juu kabisa ya usiri, mnahitaji mtu wa tatu asiye na maslahi na uhusiano wenu, awasikilize na kuwatazamisha mapungufu ya kila upande na kuwasaidie kutengeneza imani inayoongeza ushirikiano,”

Akizungumzia hilo, Sheikh Khamis Mataka amesema ni tatizo ambalo linazidi kuota mizizi kwenye jamii, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa dini kuhubiri kuhusu maana halisi ya ndoa na misingi yake.

Anasema viongozi wa dini wakitekeleza kwa ufanisi jukumu hilo huenda ikasaidia kwa wanajamii kuelewa maana halisi ya ndoa ambayo ni kuaminiana, kupendana, kuhurumiana na kusaidiana.

“Hizi kesi tunazipata nyingi mno kwa sasa, inaonekana ndoa nyingi zinazofungwa miaka hii ni za malengo, watu wanatafuta mali au kipato na ndiyo sababu mivurugano imekuwa mingi baina ya wanandoa.

“Wengine wanakuwa watumwa wa hizo ndoa hata kama wanapitia changamoto, mtu anaona huyu mwenzangu anafanya haya ili tuachane halafu mali zigawanywe, anaamua kukomaa sio kwa upendo, bali kuhofia mali,” amesema Sheikh Mataka.