Hapi: Usipoteuliwa acha nongwa, saidia ushindi wa chama

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ally Hapi amewataka wana CCM ambao wataanguka kwenye kura za maoni na kushindwa kuteuliwa kwenye nafasi walizoomba kuacha nongwa na badala yake watulie.

Iringa.  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi amewataka wanaCCM ambao hawatateuliwa kwenye chaguzi zijazo kuacha nongwa na badala yake, watulie huku wakielekeza nguvu zao kusaidia ushindi wa chama hicho.

Amesema wapo baadhi ya watu ambao huwa wanakosa uvumilivu wasipoteuliwa, hivyo wanaanzisha fitina, jambo ambalo halina uhai kwa chama hicho.

Akizungumza na wakazi wa Iringa mjini, leo Mei 5, 2024, Hapi amesema subira katika kipindi ambacho umeachwa ni jambo la msingi na hakuna anayejua kesho utapewa nafasi gani.

“Uongozi unatoka kwa Mungu, wale wote watakaochukua fomu kwenye chaguzi zijazo, ikiwa hawatateuliwa wajue wakati haujafika. Usifanye nongwa wala kutengeneza fitina, kuwa na subira,” amesema Hapi.

Amesema maeneo mengi ambayo CCM huwa inashindwa ni kutokana na migawanyiko ya ndani ya chama hicho, baada ya wale wasioteuliwa kuamua kuweka makundi yao.

“Usipoteuliwa ungana na wenzako kuiletea ushindi CCM, kuna watu bila nongwa hawawezi, sasa hawa wasiwashawishi muache kukipigania chama, huwezi kujua unaepushwa na nini,” amesisitiza.

Hapi amekumbushia namna alivyotulia akiendelea na kilimo shambani huku akiunga mkono kazi za CCM kutokana na namna alivyolelewa.

“Ulipotoka mkeka nakumbuka ilikuwa alfajiri, nikaona simo. Nikaangalie tena na tena, simo. Nikamshukuru Mungu nikaenda kwenye kilimo,” amesema na kuongeza:

“Aliyeniteua tena ni mama, imani yangu kwa nchi na chama ni kuwa mwadilifu. Tuache nongwa, tuchape kazi na tumsaidie Mwenyekiti wa CCM Taifa kuimarisha chama, hatimaye tushinde chaguzi,” amesema Hapi.

Hapi amesema ataendelea na ziara nchi nzima kuhakikisha anawakumbusha viongozi wote wajibu wao katika kuhakikisha jumuiya inakuwa hai na wanashinda katika chaguzi kuanzia wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, mwakani.

Hapi amesema hakuna ubishi kwamba chini ya Rais, Dk Samia Suluhu Hassan, zipo kazi nyingi zimefanyika katika sekta mbalimbali ikiwamo ya afya, miundombinu, elimu, kilimo na nyinginezo.

“Mama anayo imani kubwa na sisi, amefanya kazi na tunaona, lazima tumsaidie kwa kuhakikisha tunakuwa hai,” amesema Hapi.

Hapi amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha Jumuiya ya Wazazi kuelekea uchaguzi mkuu wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Amezitaka jumuiya zote kufanya kazi kwa ushirikiano ili CCM inufaike na matunda yake.

“Tushirikiane, tuchape kazi na kufikie malengo kwa pamoja,” amesema Hapi.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi, George Kavenuke amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kuiga mfano wa Hapi, kwa kufanya ziara kwenye maeneo yao katika kukijenga chama.

“Akiondoka kiongozi na sisi tuendelee na kazi, ziara isiishie leo peke yake, tuchape kazi, tufanye kazi na tufikie malengo yetu pamoja,” amesisitiza Kavenuke.