GGM kutumia Sh19 bilioni miradi ya maendeleo Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella (katikati) akishuhudia utiaji saini Mpango wa utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) iliyofanyika katika mgodi wa GGM na kuhusisha viongozi wa mgodi, halmashauri na madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita

Muktasari:

  • Katika fedha hizo, halmashauri za Geita, Mbogwe na Chato zitapata mgawo wa Sh200 milioni kila moja na fedha nyingine zitaelekezwa kwenye huduma za maji, afya na elimu.

Geita. Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) umepanga kutumia Sh19 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kipindi cha mwaka 2023.

Fedha hizo ni za kipindi cha miaka miwili ya 2022 na 2023 ambapo halmashauri ya Geita itatekeleza miradi yenye thamani ya Sh8.6 bilioni, huku halmashauri ya mji ikitekeleza miradi ya Sh9.8 bilioni.

Akizungumza leo Machi 21,2023 wakati wa hafla utiaji saini mpango wa utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti, Simon Shayo amesema halmashauri tatu za Bukombe, Mbogwe na Chato kila moja itapata Sh200 milioni za maendeleo.

Shayo amesema mbali na miradi ya elimu, afya na maji, pia wamekua wakiteketeza miradi ya kimkakati ikiwemo ya kilimo, miundombinu ya barabara pamoja na miradi ya kuwezesha wananchi kiuchumi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Geita, Constantine Morandi amesema 1/3 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na halmashauri hiyo yanatoka kwenye mgodi wa GGM na yamewezesha kujenga zahanati zaidi ya 20 pamoja na miradi mingine ya elimu, uwanja wa mpira na barabara.

Amesema mbali na mapato pia vijana kutoka kwenye mitaa inayozunguka mgodi hunufaika ma ajira kila mwaka kwenye mgodi huo.