Fursa ya miaka mitano kwa wanafunzi wa UDSM hii hapa

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala, Profesa Bernadeta Killian akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Advent Construction Limited Dhruv Jog jana Aprili 25,2024 chuoni hapo baada ya kuingia makubaliano ya Kampuni hiyo kutoa ufadhili wa wanafunzi chuoni hapo

Muktasari:

  • Sifa ya mwanafunzi atakayenufaika na ufadhili huo lazima awe na ufaulu wa juu na anapohitimu chuo atajiunga na mafunzo kwa vitendo

Dar es Salaam. Ni matumaini kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wa fani ya uhandisi wasiomudu gharama za masomo baada ya Kampuni ya Advent Construction Limited kuingia makubaliano na chuo hicho kufadhili wanafunzi watano kila mwaka.

Makubaliano hayo yaliyosainiwa jana Alhamisi Aprili 25,2024 baina ya UDSM na kampuni hiyo itawanufaisha wanafunzi kwa kipindi cha miaka mitano, ufadhili unahusisha ada, gharama za kula na nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo ndani ya kampuni ya Advent.

Sifa ya mwanafunzi atakayenufaika na ufadhili huo lazima awe na ufaulu wa juu na anapohitimu chuo atajiunga na mafunzo kwa vitendo ndani ya Kampuni ya Advent.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ujenzi Advent, Dhruv Jog amesema lengo la kutoa ufadhili huo ni kuionyesha jamii kampuni za wazawa zina uwezo mkubwa wa kusaidia jamii na Taifa kuwa na maendeleo kiuchumi.

"Tumeingia makubaliano ya miaka mitano kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani ya ujenzi lakini mipango yetu ni kuhakikisha ufadhili huu unadumu kwa miaka zaidi ya 100, hivyo tumeanza miaka mitano lakini ni ufadhili ni endelevu,"amesema.

Akitaja sifa za wanafunzi hitajika, Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu Kampuni ya Ujenzi Advent, Rose Kimambo amesema mwanafunzi atakayepata ufadhili huo lazima awe amepata daraja A kwenye mitihani yake ya mwisho.

Sifa nyingine lazima mwanafunzi awe anapendelea masomo ya uhandisi na awe amehitimu shule ndani ya Tanzania.

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM hicho anayeshughulikia fedha, mipango na utawala, Profesa Bernadeta Killian amesema wanafunzi kukosa fedha za kulipia ada ndani ya vyuo vya elimu ni tatizo kubwa hivyo ufadhili huo utatoa fursa kwa wanafunzi wenye kipato kidogo.

"Makubaliano haya ni miaka mitano lakini tumetanua zaidi kwa kushirikiana kwenye utafiti na ubunifu, wanafunzi watakaonufaika ni wa fani ya uhandisi na sayansi ambayo wanafunzi wa kike ni wachache,” amesema.

Profesa Bernadeta amesema:“Asilimia 47 ya wanafunzi wanaosoma chuo hiki ni wanawake lakini ni asilimia 26 ya wanawake wanachukua fani ya uhandisi,ufadhili huu utaleta uwiano wa kijinsia kwenye uhandisi na Sayansi," amesema.

Profesa Bernadeta amesema kwa mwaka chuo hicho hutoa wahitimu 100 ngazi ya uzamivu na shahada ya uzamili kila mwaka wanahitimu wanafunzi 800.

Mwakilishi wa wanafunzi fani ya uhandisi chuoni hapo, David Daniel ameomba wadau wengi kujitokeza kuwafadhili wanafunzi wa fani hiyo.

"Programu hii ni nzuri kwasababu mwanafunzi anasoma huku akijifunza kwa vitendo naamini wanafunzi wengi watanufaika," amesema.