Dk Salim afichua ndoto zake UN zilivyokatishwa

Katika moja ya shajara ya Dk Salim Ahmed Salim ya Ijumaa, Desemba 06, 1996, aliandika: “Leo imekuwa siku ya pekee kuhusu uwezekano wa kuwania kwangu nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNSG).

“Siku hii imeniletea mshangao wa ghafla pale nilipoangalia kupitia CNN, takriban saa 11 jioni, kwamba Makamu wa Rais (wa Afrika Kusini) Thabo Mbeki alitangaza hadharani huko New Delhi (India) kuunga mkono uwezekano wa kuwania kwangu nafasi ya UNSG.

“Tangazo hili lilikuja bila taarifa yoyote kwangu na katika muktadha wa matukio ya leo ambayo yalionyesha wazi upinzani wa Ufaransa kwa sababu za lugha, jambo ambalo halina msingi ikizingatiwa kuwa Ufaransa iliunga mkono azma yangu ya mwaka 1981.

“Matukio yafuatayo kuhusiana na suala la UNSG yanastahili kuzingatiwa:
“(i) Saa 11:15 asubuhi, Rais Benjamin Mkapa alinipigia simu kutoka Iringa, Tanzania kuulizia hali ilivyo na hasa kama Mkutano wa Ouagadougou umetoa msimamo wowote thabiti kuhusu suala hilo.

“Nilimweleza Rais (Mkapa) kuhusu mashauriano yangu na Rais (Blaise) Compaore (wa Burkina Faso) na Jenerali Sani Abacha (Rais wa Nigeria). Nilimalizia kwa kumwambia Rais kwamba, kwa kuzingatia hali ilivyo, haingekuwa busara kuwasilisha jina langu. Badala yake, mashauriano yanapaswa kuimarishwa ili kubaini msimamo wa mwisho wa Ufaransa na katika mchakato huo kujaribu kuwashawishi kuonyesha unyumbufu.

“(ii) Saa 12:15 na baadaye saa tatu asubuhi, Anne (Makinda) alinipigia simu kutoka Addis Ababa. Katika nyakati zote mbili, tulijadili suala la UNSG na nilimweleza kwamba msimamo wangu thabiti ni kwamba, isipokuwa msimamo wa Ufaransa utafafanuliwa kwa njia inayoonyesha unyumbufu zaidi, hakuna haja ya kuwasilisha jina langu kwenye Baraza la Usalama. Anne alikubaliana kabisa na msimamo huu.

“(iii) Saa 3:15 asubuhi, wakati bado najaribu kulala ingawa nilienda kitandani saa kumi usiku, nimekuwa nikiamshwa mara kwa mara na simu. Hakika ni simu muhimu na zinazohusiana. Mtu aliyetambulisha kuwa ni Balozi wa Ufaransa anayeratibu Mkutano wa Ufaransa-Afrika alinipigia simu.

“Alisema kuwa aliarifiwa na Balozi wa Ufaransa huko Pretoria kwamba napaswa kumpigia simu Rais Nelson Mandela saa 11 asubuhi kwa saa za Afrika Kusini kwenye namba 27-11-4831227 (nilipochunguza, niligundua kuwa hiyo ni namba ya makazi ya Rais huko Johannesburg) au saa moja usiku kwa saa za Afrika Kusini kwenye namba (27-21)6899121 (Cape Town).

“Kwa kuwa wakati huyo mtu alinipigia tayari ilikuwa imepita saa kumi na moja asubuhi kwa saa za Afrika Kusini, nilimpigia Rais simu saa kumi na moja jioni (ambayo ilikuwa saa moja usiku kwa saa za Afrika Kusini) tu kugundua kuwa hakuwepo. Niliambiwa kuwa alikuwa anashiriki chakula cha jioni lakini watanipigia Rais atakaporudi.

“Baada ya kupata simu kutoka Cape Town (Afrika Kusini), niliona habari kwenye CNN kuhusu Afrika Kusini kuniunga mkono kuwania nafasi ya UNSG.

“Suala la UNSG lilikuwa moja ya mada zilizojadiliwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje Jakaya Kikwete akiandamana na Balozi Kibello waliponitembelea kwenye chumba changu cha hoteli saa 6:15 mchana...”

“Baada ya mashauriano kati ya Rais Mandela na Makamu wa Rais Thabo Mbeki na wengine, Rais Mandela ameamua si tu kwa Afrika Kusini kuniunga mkono bali pia kuwasilisha rasmi uwezekano wa kuwania kwangu nafasi hiyo kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Wako tayari kufanya hivyo mara moja lakini walitaka kwanza kupata ridhaa yangu.
“Walikuwa wanatambua msimamo wa Ufaransa juu ya suala la lugha lakini hawaamini kwamba hilo linatosha kufanya Ufaransa ipige kura ya veto dhidi ya uwezekano wa kuwania kwangu nafasi hiyo.

“Rais Mandela amezungumza kwa nyakati tofauti na marais (Bill) Clinton (wa Marekani) na (Jacques) Chirac (wa Ufaransa) na atanijulisha ipasavyo. Lakini ni hisia zao kwamba hatupaswi kuruhusu msimamo wa Ufaransa kuzuia jina langu kuwasilishwa. Ikiwa Ufaransa itapiga kura ya veto dhidi ya uwezekano wa kuwania kwangu nafasi hiyo, watakuwa wanatafuta mgongano na maslahi yao barani Afrika yataathirika.
 

Kuwania ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa

Mwaka 1981, Dk Salim alionyesha nia ya kugombea nafasi ya katibu mkuu. Hakufanikiwa pamoja na kwamba aliungwa mkono na nchi za Afrika, Asia, Kilatini.

Marekani na China, katika nafasi zao kama wanachama wa kudumu, walitumia mamlaka yao ya kura ya turufu dhidi ya wagombea ambao wao hawakuwataka.
Marekani ilimpendelea mgombea wa Austria, Kurt Waldheim, lakini China na Ufaransa zilimuunga mkono Dk Salim. Uingereza na Urusi hazikupiga kura.

Mchakato wa kupiga kura kumpata katibu mkuu unahitaji kuungwa mkono, au angalau kusiwe na upinzani miongoni mwa wanachama wote wa kudumu wa Baraza la Usalama na kura nyingi kutoka kwa UNGA.

Mchakato huo wa muda mrefu wa uchaguzi ulirudiwa mara 16 katika kipindi cha wiki tano, Salim alimtaka Rais wa Baraza la Usalama la wakati huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda, Balozi Olara Otunnu, kuwasiliana na Baraza la Usalama kuwaambia hataki jina lake lirudishwe kwenye upigaji kura uliofuata baadaye.

Ilidhihirika kuwa Marekani haikukata tamaa ya kumzuia Dk Salim kugombea, hivyo alijitoa kuruhusu wagombea wengine wa Afrika wanaotaka kugombea nafasi hiyo. Hatimaye, mwanadiplomasia wa Amerika ya Kusini kutoka Peru Javier Perez de Cuellar alichaguliwa.


Baadhi ya nyadhifa katika Umoja wa Mataifa (UN)

Akiwa mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kuondoa Ukoloni, alifanya ziara za kibalozi katika nchi za Uingereza, Tanzania, Zambia, Botswana, Msumbiji na Ethiopia.

Anabainisha tofauti kati ya nafasi hii na ile ya Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kwamba Kamati Maalumu ya Kuondoa Ukoloni ilitoa mapendekezo, wakati Baraza la Usalama lilikuwa na uwezo wa kufanya uamuzi.

Aprili na Mei 1976, Salim aliongoza kikosi cha wajumbe sita kutoka Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuondoa Ukoloni.

Kikosi hicho kilisafiri hadi Lusaka, Zambia; Dar es Salaam, Tanzania; Addis Ababa, Ethiopia; Maputo, Msumbiji; Gaborone, Botswana na London, Uingereza kushauriana juu ya juhudi za kuondoa ukoloni katika nchi za Rhodesia na Namibia.

Mashauriano haya, yaliwashirikisha wakuu wa nchi na maofisa wa Serikali, wawakilishi kutoka kwa watendaji wakuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na Kamati yake ya Ukombozi, na wanachama wa vuguvugu mbalimbali za ukombozi, yalikuwa hatua muhimu ya kuboresha ushirikiano kati ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa kuhusu ya kuondoa ukoloni katika Afrika.

Kipindi cha Salim kama mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vikwazo dhidi ya Rhodesia mwaka 1975 na kipindi chake cha mwaka 1976 kama Rais wa Baraza la Usalama kilisaidia sana kufanikisha kupitishwa kwa Azimio 386 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono kupatikana kwa uhuru wa Msumbiji na nchi nyingine kadhaa ikiwamo Namibia.

Kipindi ambacho Dk Salim alifanya kazi katika Umoja wa Mataifa kiliinua hadhi ya Afrika na ile ya mataifa mengine yanayoendelea.

Mwaka 1980 alirejea nyumbani kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania hadi 1984 kilipotukia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine, ndipo alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Salim aliongoza Kamati ya Ukombozi ya OAU mwaka 1983. Mwaka 1988 alimshinda Ide Oumarou, wanadiplomasia wa Nigeria, katika nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU, wadhifa alioshikilia hadi Julai 2001.