Dk Nchimbi awafuta machozi waathirika wa maporomoko ya tope kwa Sh10 milioni

Katibu mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiwasalimia waathirika wa maporomo ya tope la Mlima Kawetele waliopo katika kambi ya shule ya Msingi Tambukareli lei Aprili 17 jijini Mbeya

Muktasari:

  • Maporomoko hayo yamesababisha kaya zaidi ya 50 kukosa makazi, hali iliyoilazimu Serikali kuwapa makazi ya muda katika Shule ya Msingi ya Tambukareli.

Mbeya. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, amewatembelea wananchi walioathiriwa na maporomoko ya matope kutoka kwenye Mlima Kawetere, Kata ya Itezi, jijini Mbeya na kutoa Sh10 milioni kama kifuta machozi.

Dk Nchimbi amewatembelea waathirika hao leo Jumatano Aprili 17, 2024 kwenye kambi ya muda iliyopo Shule ya Msingi Tambukareli.


Akizungumza na wananchi hao, Dk Nchimbi amesema lengo la kufika hapo ni kuwapa pole na kuwaomba waendelea kumtanguliza na  kumshukuru Mungu kwa kuwanusuru na maporomoko hayo.

"Tumshukuru Mungu wote mpo salama, tujaribu kufikiria maporomoko haya yangetokea saa nane usiku, leo tungekuwa tunazungumza nini? Tumtangulize Mungu sana. CCM inatoa shukrani kwa watu wote walioguswa na kuja kusaidia kambi hii, shukrani pia kwa Serikali, taasisi mbalimbali na mbunge wenu Dk Tulia Ackson.

“Niwaombe sana ndugu zangu, zingatieni tahadhari za Serikali wakati uchunguzi unaendelea, wananchi tuwe na subira tusiharakishe kurudi huko,” amesema Dk Nchimbi.

Akiwa kwenye kambi hiyo, Dk Nchimbi mbali na salamu za pole kutoka kwa  Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, alisema fedha hizo zitasaidia kupunguza madhila yanayowakabili.

Dk Nchimbi alikabidhi fedha hizo kwa Diwani wa Kata ya Itezi, Sambwe Shitambala ambaye pia amepatwa na maafa hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Beno Malisa amemweleza Dk Nchimbi  kuwa maporomoko ya matope kutoka mlimani yaliyotokea Jumapili Aprili 14, 2024,  yamesababisha uharibifu wa nyumba 21 na mali.

Kutokana na maporomoko hayo, kaya zaidi ya 50 hazina makazi na zimehamiwa kwa muda katika Shule ya Msingi ya Tambukareli.

Malisa amesema mpaka sasa wananchi hao wameshapewa misaada ya huduma za kibinadamu kutoka Serikali ya Mkoa wa Mbeya na wadau mbalimbali.

“Wananchi hawa wanapatiwa pia huduma za afya na msaada wa kisaikolojia kutoka kwa wataalamu,” amesema Malisa.