DC Muheza awapa mabinti wa chuo siri ya kufanikiwa

Mkuu wa Wilaya ya Muheza Zainab Abdallah.

Muktasari:

  •  Mabinti wameelezwa kuwa ili kufikia ndoto zao wanapaswa kutokata tamaa jambo ambalo litawaweka katika mlango wa kufanikiwa kimaisha

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Muheza Zainab Abdallah amesema mabinti wanapaswa kuwa na ndoto kubwa zisizoweza kufikika ili kuwapa chachu ya kujituma zaidi katika masomo na shughuli wanazozifanya.

Amesema ili kufikia ndoto zao wanapaswa kutokata tamaa jambo ambalo litawaweka katika mlango wa kufanikiwa kimaisha.

 Zainab amesema hayo leo alipohudhuria hafla fupi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) jijini Dar es Salaam.

“Wewe unayependa urembo, upishi au mavazi basi jitume ili uje uwe msusi au mpishi wa Rais ili ukatengeneze jina watu wakufahamu duniani ukaingize pesa,” amesema.

Ameongeza kuwa hata wanapokuwa wanasoma wanaweza kufanya mambo makubwa akitolea mfano kuwa washoni au wabunifu wa mavazi nje ya kusoma na wakafanikiwa kimaisha.

“Hapa chuoni kuna watu wanafanya sherehe za kuzaliwa kila siku unaweza ukawa unatengeneza keki ukawa unauza kila siku, nawaambia hamjachelewa lazima ujue ndoto yako uweze kufanikiwa,” amesema Zainab.

Aidha, amesema lazima waweke mikakati ya kuzifikia ndoto zao  kuanzia chini na mikakati lazima ifanane na ndoto. Amesema lazima waepuke vitu kama kashfa ili wajiandae kuwa viongozi safi.

Akijitolea mfano yeye mwenyewe kuteuliwa kuwa DC mdogo akiwa na umri wa miaka 23 pekee amesema yeye kwao ndio wa kwanza kuteuliwa kwenye wadhifa huo kwa kuwa alijiandaa yeye binafsi kuanzia kifikra na kuwa kioo kwenye jamii.

“Kiongozi lazima uwe msaada kwenye watu wanaokuzunguka, lazima kuacha ubinafsi, uwashike mikono wenzako waweze kufanikiwa sasa ili yote yatimie pia kuwa na ndoto nyingi, mimi mnavyoniona ni kiongozi nina ndoto nyingi nasoma pia namiliki kampuni nafanya na biashara,” amebainisha.

Amesema lazima wajitoe kwakuwa wanawake Mungu amewapa uwezo wakufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, hivyo wanapaswa kufanya kile kilicho sahihi huku wakiwa na watu sahihi.

Mwisho amewataka kuwa watu wenye nidhamu kuanzia wanavyosuka, kutembea na katika matumizi ya pesa.

Mkurugenzi wa Taasisi  ya Mwanamke na Uongozi, Shamira Mshangama amesema wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza ili kutimiza ndoto zao za kuwa viongozi.

Amesema jambo kubwa ni kuondoa hofu mioyoni mwao na kujiamini akimtolea mfano mkuu wa wilaya Zainab kuwa miongoni mwa viongozi mdogo nchini akisema hayo yote yanawezekana.

Mshangama amesema wanapaswa kujenga mtandao kwa kuwa hakuna mtu aliyeweza kufanikiwa peke yake akiwataka kuwa na uhusiano mzuri na kila mtu kuanzia marafiki.

Aidha, amewataka mabinti kujitokeza na kujitosa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi nchini ili kufanikisha ndoto zao.

Mmoja ya mabinti waliohudhuria hafla hiyo, Nafhat Abdallah amesema kitendo cha binti kuwa na malengo makubwa na ya muda mrefu kinaleta chachu katika maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.

“Japokuwa changamoto ni nyingi katika safari ya maisha ya binti lakini kinachopaswa ni kusimama na kuendelea kusonga mbele,” amesema Nafhat.