Daraja Mto Luipa kunusuru maisha ya wananchi Mlimba

Mwonekano wa daraja linalojenga kwenye Mto Luipa.

Muktasari:

  •  Mwenge wa Uhuru  umezindua miradi saba yenye thamani ya Sh2.361 bilioni kwenye halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ikijumuisha ya elimu, maji, afya, kilimo, mifugo, maliasili, mazingira na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mlimba. Wakazi wa vijiji vya Kisegese, Chiwachiwa na Lavina katika Kata ya Namawala wataepuka hatari ya kupoteza maisha baada ya daraja jipya kuanza kujengwa katika Mto Lupa.

Daraja linalotumika sasa ni la mbao linalodaiwa kukatika mara kwa mara na kusababisha vifo na majeruhi kwa watumiaji wake.

Leo Jumanne Aprili 23, 2024, Mwenge wa Uhuru umezindua ujenzi wa daraja hilo utakaogharimu Sh1.926 bilioni za Halmashauri ya wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Kisegese Wilayani Mlimba, Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi amesema wananchi wa vijiji hivyo wanapata  madhara mbalimbali ikiwemo kutumbukia mtoni na kupoteza maisha, kujeruhiwa na wengine hupoteza mifugo na mazao mtoni hapo.

Mbunge huyo amesema kukamilika kwa ujenzi wake kutaleta faraja zaidi kwa wananchi kwa kuwa linaunganisha pia vijiji vya Mbingu Chini, Kisegese, Chiwachiwa na Lavina.

Mkazi wa Kijiji cha Kisegese, Scola Andrea (32) amesema mto Luipa una tabia ya kujaa kipindi cha masika na hakuna mtu anayeweza kuuvuka.

“Wanaopata shida zaidi wale wanaokaa Chiwawachiwa, maji yakijaa hapa huwezi kuvuka na kama ndiyo mama mwenye mimba anataka kwenda kule ng’ambo hawezi kujifungua, atazalia hapahapa mtoni,” amesema Andrea.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Mhandisi Sadiki Karume amesema ujenzi wa daraja la Luipa ulianza Mei 26, mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Novemba 17, mwaka huu.

Amesema mpaka sasa ujenzi wake umegharimu Sh1.336 bilioni kati ya Sh1.926 bilioni zitakazotumika kuukamilisha.

Karume amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya Nabawy Construction Ltd ya Morogoro.

“Kukamilikia kwa daraja hili kutaleta nafuu kwa wananchi wa Kata ya Namawala na Mbungu,” amesema mhandisi huyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mnzava ameipongeza halmashauri hiyo  kufuata taratibu za zabuni kwa kumpata mkandarasi aliyekidhi vigezo na kuondoa manung’uniko.

“Serikali ilitunga sheria za usimamizi wa fedha za umma kwamba kuwe na utaratibu wa matumizi wa fedha na wazabuni wanaopata wapite kwa sifa walizonazo. Hii inaondoa manung’uniko na tumejiridhisha baada ya kukagua nyaraka za utekelezaji wa mradi huu , itaondoa madhara ambayo wananchi walikuwa wakipata katika daraja la mbao la mto Luipa,” amesema Mnzava.