Chanzo ajali ya basi, treni iliyoua 13 chatajwa

Muktasari:

  • Wakati watu 13 wakipoteza maisha kutokana na ajali ya basi linalomilikiwa na Kampuni ya Ally's kugonga treni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limeweka wazi chanzo cha ajali.

Singida. Jeshi la Polisi mkoani Singida, limesema chanzo cha ajali ya basi la Ally’s, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza na kusababisha vifo vya watu 13 baada kugonga kichwa cha treni katika makutano ya reli na barabara wilayani Manyoni ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo.

Hata hivyo, katika ajali hiyo kumekuwa na idadi tofauti ya majeruhi kutoka vyanzo vitatu tofauti ambapo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ataja idadi ya majeruhi 32, Jeshi la Polisi limesema wapo 34, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC) likitangaza majeruhi ni 25.

Akizungumza leo, Jumatano Novemba 29, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa amesema kichwa cha treni kiliacha njia yake na kwenda pembeni mwa reli.

Kamanda Mutabihirwa amewataka madereva wote wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani zinawaongoza ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha TRC, Jamila Mbarouk basi hilo liligonga kichwa cha treni chenye namba V9519006 kilichokuwa kinatokea stesheni ya Aghondi kuelekea Manyoni.

Amesema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 13, kati yao, wanawake wakiwa sita na wanaume saba na kujeruhi 25, ambao ni wanawake ni saba na wanaume 18.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema hakuna majeruhi yoyote aliyesalia ndani ya basi hilo baada ya kuliinua.

Awali Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Dk Furaha Mwakafwila amesema wamepokea miili ya watu 13 na majeruhi 32.