CCM yajinasibu kwa kuwa na hazina ya wazee

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, akisalimiana na aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Salum Juma Tindwa nyumbani kwake Kwa Mchina, Unguja alipofanya ziara ya kuwatembelea viongozi wastaafu wa chama hicho na Serikali.

Muktasari:

  • CCM Zanzibar imesema wazee wenye uzoefu na upeo mkubwa wa maarifa hukishauri mambo yenye kuleta tija.

Unguja. Chama cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimesema kinazidi kuimarika kutokana na hazina ya wazee waliopo, hivyo kitaendelea kutunza, kuthamini na kuwaenzi wazee waliohudumu kwa uadilifu katika nafasi mbalimbali za utumishi ndani ya chama na serikalini kwa ujumla.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema hayo  Aprili 22, 2024 akiwa ziarani  kuwatembelea wazee wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya Unguja.

Amesema maendeleo yaliyopatikana nchini yalijengewa misingi imara na wazee hao enzi za utumishi wao, hivyo wana mchango mkubwa katika mafanikio yaliyofikiwa.

Amesema chama hicho kinajivunia kuwa na wazee  wenye uzoefu na upeo mkubwa wa maarifa ya kushauri mambo yenye kuleta tija.

“Watu wengi wanajiuliza kwa nini CCM kila siku inazidi kuimarika ni kutokana na uwepo wa wazee hawa ambao wengi wao walifanya kazi kubwa ya utumishi katika maeneo mbalimbali ya chama na Serikali, na wanaendelea kutushauri mambo mema yanayoleta ufanisi ndani ya taasisi yetu,” amesema Dk Dimwa.

Kupitia ziara hiyo amewasisitiza viongozi na watendaji wa chama hicho na Jumuiya zake kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea wazee na makundi mengine yenye mahitaji maalumu, ili nao wajione bado wanakumbukwa na kuthaminiwa juu ya kazi kubwa walizofanya.

Wazee waliotembelewa ni Kadhi mkuu mstaafu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji Khamis,  kada wa CCM,   Waalidi Psinarie Kavishe, aliyekuwa mkuu wa mkoa kusini Pemba, Salum Juma Tindwa na aliyekuwa katibu mkuu wizara ya wanawake na watoto Zanzibar, Msham Abdallah Khamis.

Kavishe amesema hatua hiyo inajenga matumaini mapya kwao kuonekana wanakumbukwa, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuendelea kutoa ushauri wao.

Ametoa wito kwa viongozi, watendaji na wanachama wa CCM nchini kuhakikisha wanakipigania chama hicho kiendelee kushika dola mwaka 2025.