CAG apunguza hati chafu hadi moja, akagua hesabu za Umoja wa Afrika

Muktasari:

  • Wakati hati chafu zimepungua toka sita miaka iliyopita hati moja, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) sasa inakagua hesabu katika ngazi ya kimataifa zikiwamo za Mahakama Maalumu ya watuhumiwa wa vita vya Sierra Leone iliyopo The Hague nchini Uholanzi, hesabu za Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dodoma. Wakati Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ikienda kimataifa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere amesema kwenye ukaguzi wa hesabu za mwaka 2022/2023 hati chafu imepatikana moja tofauti na miaka iliyopita.

Kichere amesema hayo leo Alhamisi, Machi 28, 2024  wakati akikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na ukaguzi wa ufanisi ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa mujibu wa Katiba. Ripoti hiyo inatakiwa kukabidhiwa kwa Rais kabla ya Machi 30 kila mwaka na Rais ndani ya siku saba za kazi anatakiwa kuiwasilisha bungeni.

“Mwenendo wa hati za ukaguzi nimetoa jumla ya hati 1,209 za ukaguzi kati ya hizo hati 222 zinahusu Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hati 215 zinahusu mashirika ya umma, hati 475 zinahusu Serikali Kuu na hati 19 za vyama vya siasa, hati 296 zinahusu miradi ya maendeleo.

“Katika hati hizo zinazoridhisha ni 1,197, sawa na asilimia 99, hati zenye shaka ni tisa sawa na asilimia 0.7, hati mbaya ni moja sawa na asilimia 0.1 na nilitoa hati mbili za kushindwa kutoa maoni ambayo ni sawa na asilimia 0.2,” amesema.

Amesema kwa ujumla hati za ukaguzi wa hesabu zinazounyesha utayarishaji unaoridhisha wa hesabu unaozingatia kwa kiasi kikubwa taratibu na kanuni za uandaaji wa hesabu akisema utayarishaji wa hesabu unazingatia viwango vinavyotakiwa kimataifa.


Mapendekezo yake

Kichere pia amesema katika ripoti za ukaguzi wa hesabu za miaka iliyopita alitoa mapendekezo kadhaa yanayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma, kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuongeza tija katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.

“Natambua juhudi kubwa za Serikali yako katika kuyafanyia kazi mapendekezo ninayotoa kwenye ripoti zangu za ukaguzi, hii ni pamoja na ofisi yako kutoa miongozo mbalimbali juu ya kushughulikia mapendekeao ya ripoti zangu.

“Hata naendelea kuweka msisitizo kwamba mapendekezo haya yatekelezwe kwa ukamilifu ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha na rasilimali zingine zinazotumika katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Serikali zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema.


Mafanikio ya NAOT

Kichere pia amesema Januari 6, 2024, ofisi yake ilifanikiwa kupata cheti cha kutambulika kimataifa kwa mfumo wa usimamizi wa ubora, kinahotolewa na taasi ya kimataifa ya viwango vya ubora.

“Ofisi yangu imeendelea kukagua kamisheni ya usimamizi wa Anga ya Afrika, yenye  makao makuu yake mjini Dakar nchini Senegal, kwa mkabata wa miaka mitatu utakaokamilika mwaka kesho wa 2025.

“Pia, tunaendelea na mkataba wa kukagua hesabu za Umoja wa Afrika (AU), wenye makao makuu yake mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, mkataba ambao utakamilika mwaka huu,” amesema.

Kichere pia amesema wanakagua hesabu za Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zake. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Tanzania, Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda.

 “Naomba kutumia fursa kukujulisha kuwa tumepata mkataba mwingine wa miaka sita wa kukagua Mahakama Maalumu inayoshughulikia kesi za waliohusika na uhalifu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone iliyopo The Hague nchini Uholanzi,” amesema.

Mahakama hiyo ndiyo iliyomuhukumu kifungo cha miaka 50 jela Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor ambaye alikutwa na hatia ya kutenda makosa 11 ya uhalifu wa kivita nchini Sierra Leone. Taylor amefungwa jela nchini Uingereza.