Bashe ataja mikakati nane kukuza uzalishaji mazao ya bustani

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Muktasari:

  • Wizara ya Kilimo imeeleza mkakati nane ya kukuza na kuimarisha mazao ya bustani ili kuuza mazao hayo kwa tija kimataifa.

Dodoma. Wizara ya Kilimo imeeleza mkakati nane ya kukuza na kuimarisha mazao ya bustani ili kuuza mazao hayo kwa tija kimataifa.

Mazao hayo yaliyowekewa mkakati ni mazao ya matunda, mboga, maua na viungo.

Mikakati hiyo imeelezwa leo Jumanne, Oktoba 25, 2022 na Waziri wa kilimo, Hussein Bashe wakati akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa mikakati wa Taifa wa kuendeleza mazao ya bustani katika kipindi cha miaka 10 ambapo Sh4.7 trilioni zitatumika kwenye utekelezaji wake.

Bashe amesema vipaumbele vya wizara hiyo ni kuhakikisha mnyororo wa thamani wa mazao hayo kuanzia kwenye mbegu, uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa mazao hayo ndani na nje ya nchi.

Akieleza mikakati mingine, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Andrew Massawe amesema wamejikita katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani kwa kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mazao ya asili ya mbogamboga.

Amesema mkakati mwingine ni kuboresha miundombinu ya ufungaji, uhifadhi na usafirishaji wa mazao hayo baada ya kuvuna.

Aidha amesema mikakati hiyo imejielekeza katika maeneo makuu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani na bidhaa zilizosindikwa kwa asilimia 40, kuimarisha tafiti, uratibu na uwezo wa wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani Ili kuwezesha uwekezaji katika tasnia hiyo.

"Mkakati huu utafanya mabadiliko katika kilimo cha mazao ya bustani kwa kuongeza uwezo wa wakulima wadogo, wawekezaji na watoa huduma katika mnyororo wa thamani wa matunda, mboga, viungo, mimea tiba, mapambo na vikolezo"amesema.

Mkakati huo unalenga mazao yenye fursa za biashara na kuimarisha lishe yakiwemo zabibu, parachichi, nyanya, pilipili manga, mdalasini, karafuu, vanilla, embe, nanasi, viazi mviringo, vitunguu, tangawizi na mboga za asili zenye viini lishe.