Baba atiwa mbaroni akidaiwa kumnajisi mtoto wake

Kamanda wa Polisi Nkoa wa Njombe, Mahamoud Banga

Muktasari:

  • Baba alienda kumripoti Polisi kijana mmoja aliyemuhisi kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na binti yake, mtoto naye akadai kuwa baba yake ndiye anayembaka.

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Barnabas Ndelwa (32) mkazi wa Mtaa wa Kitisi kwa tuhuma za kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka 13.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatano Aprili 17, 2024, Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Mahamoud Banga amesema tukio hilo limetokea Aprili 14, 2024 katika Wilaya ya kipolisi Makambako.

Kamanda huyo amesema mtoto huyo alienda kituoni hapo akiambatana na baba yake aliyekuwa na lengo la kwenda kumshtaki kijana, aliyedai ana uhusiano wa kimapenzi na binti yake huyo.

Hata hivyo, wakati baba akitoa maelezo, ndipo binti yake akawaeleza polisi kuwa baba yake ndiye huwa anamnajisi.

Amesema mtoto huyo amedai kuwa mtuhumiwa amekuwa akimfanyia kitendo hicho tangu mwaka 2022.

"Binti alipofika kituo cha polisi kwa ajili ya kupata huduma ya PF3, ndipo aliwaeleza maofisa wa dawati la jinsia la polisi Wilaya ya Makambako kuwa licha ya kuletwa na baba yake kwa ajili ya kumshtaki kijana anayetuhumiwa kutembea naye, lakini baba yake ndiye anamuingilia,” amedai Kamanda Banga.

Kamanda Banga amesema baada ya maelezo ya mtoto huyo, baba huyo alikamatwa na bado anashikiliwa na polisi hadi uchunguzi utakapokamilika.

Amesema ikibainika baba huyo anahusika na tuhuma hizo, atafikishwa mahakamani mara moja.

Akizungumzia hilo, mkazi wa Makambako, Paschal Matimbwi amesema hali ni mbaya kwenye maeneo mengi mjini humo.

“Tuhuma za wazazi kuwaingilia watoto wao yanazidi kuongezeka tu, wazazi inabidi tujitathimini,” amesema matimbwi.

Amesema inafikia wakati wazazi wenyewe kwa wenyewe wanashindwa kuaminiana ndani ya nyumba, hivyo hadhani kama wanaweza kuwalinda watoto na vitendo vya ukatili.

Merygoreth Richard mkazi wa Njombe mjini amesema kwa Makambako tukio hilo si la kwanza kuripotiwa yamekuwa yakijirudia mara kwa mara, wananchi wasiiachie Serikali pekee kupambana na tatizo hilo.

“Wananchi tuingilie kati, tusiseme huyu sio mtoto wangu muache aharibikiwe, bali tuungane kuwasaka wahalifu tuwaripoti na tutoe ushirikiano pale panapohitajika kutoa ushahidi kwa mamlaka husika,” amesema Richard.

Na ametoa rai kwa Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaojihusisha na matukio ya aina hiyo ili kuwa fundisho kwa wengine.

"Baba anambaka mtoto wake tunakwenda wapi na ni nani wa kumlinda mtoto kama siyo mzazi, ndiye anatakiwa kuwa wa kwanza kumlinda mwanawe,” Richard