Baba adaiwa kumuua mtoto wake kisa achangiwe fedha alipe madeni

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera

Muktasari:

  • Mtuhumiwa anadaiwa kumziba pua na mdomo mtoto wake wa miezi minne, kisha kutumbukiza mwili kwenye jaba lenye maji.

Tarime. Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya inamshikilia Marwa Meng'anyi (40), mkazi wa kijiji cha Keroti wilayani Tarime kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa miezi minne, ili apate fedha kutoka kwenye kikundi cha kusaidiana, kisha alipe madeni.

 Akizungumza kwa simu leo Jumapili Machi 31, 2024, Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Mark Njera amesema inadaiwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo kwa kumziba pua na mdomo mtoto huyo.

Amesema baada ya kufariki dunia kwa kukosa pumzi, alimtumbukiza kwenye jaba lenye maji.

"Tukio lilitokea Machi 21, 2024, tunaendelea na uchunguzi kujua ukweli juu ya tukio hili, baada ya hapo hatua nyingine zitafuata. Uchunguzi wa awali wa daktari unaonyesha mtoto alikufa kwa kukosa hewa baada ya kuzibwa pumzi mdomoni na puani, baba bado tunaye mahabusu," amesema.

Amemtaja mtoto huyo kuwa Selina Marwa ambaye mwili wake ulikutwa ndani ya jaba.

Akieleza tukio hilo, mama wa marehemu, Bageni Marwa amesema siku hiyo alimuacha mumewe na watoto wao wawili, alipokwenda mtoni kufua.

Amesema akiwa anamalizia kufua, ghafla mtoto wao mkubwa alimfuata mtoni akimtaka waende nyumbani kumuangalia mtoto.

"Nilipofika nyumbani mtoto alinielekeza moja kwa moja kwenye ndoo ya maji, nilimkuta mtoto wangu akiwa ametumbukizwa mle kichwa chini miguu juu wakati huo mume wangu hakuwepo nyumbani.

“Nilipiga kelele kuomba msaada ndipo watu wakaja, baadaye mume wangu naye akaja, kisha mwenyekiti akasema mazingira ya kufa yana utata, hivyo ni lazima polisi waje kufanya uchunguzi kwanza," amesema.

Bageni amesema mume wake alikataa wazo la polisi kwenda kufanya uchunguzi akidai yeye ndiye aliyepata hasara ya kufiwa na mtoto na kutaka kumzika bila uchunguzi.

"Alikataa akasema yeye ndiye amepata hasara, hivyo hataki mambo ya polisi hapo ndipo nami nikapata wasiwasi kwa nini akatae uchunguzi? Nikaanza kuamini kuwa huenda yeye ndiye aliyemuua mtoto wangu," amesema.

"Ni kweli mume wangu alikuwa na madeni mengi sana, watu walikuwa wanapishana hapa kumdai yawezekana kweli alimuua mtoto ili achangiwe na kikundi kwa sababu miongoni mwa waliokuwa wanamdai ni kikundi chake pia," amefafanua Bageni.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Keroti, Marwa Mwita amesema baada ya kufika eneo la tukio na kukuta mazingira ya kutatanisha aliamua kulishirikisha Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi.

Amesema madai ya baba huyo kumuua mtoto wake ili achangiwe yalitolewa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakiwepo wana kikundi wenzake na kwamba kitendo cha baba huyo kukataa polisi kufanya uchunguzi pia kinaashiria huenda madai hayo yakawa na ukweli.

"Huwa kuna utaratibu wa mwanakikundi akipata msiba anachangiwa pesa, kwa hiyo huyu kutokana na madeni yanayomkabali yawezekana aliona njia pekee ya kupata pesa ni kufiwa, hivyo akaamua kujitengenezea  msiba kwa kumuua mtoto wake mchanga," amedai.