Askofu apendekeza Rais kushauriwa bila unafiki

Baadhi ya waombolezaji katika Msiba ya Mwenyekiti wa CCM mkoa Arusha, Zelothe Stephen Zelothe ambao wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdurahman Kinana. Picha Mussa Juma

Arusha. Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Massangwa amewataka wasaidizi wa Rais, Samia Suluhu Hassan kumshauri bila unafiki na kutanguliza ubinafsi.

Akiongoza Ibada katika mazishi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa Arusha, Zelothe Stephen Zelothe leo Oktoba 30, 2023 Askofu Masangwa amesema wasaidizi wa Rais waache kumpaka Rais mafuta kwa mgongo wa chupa.

"Sisi sote ni wasaidizi wa Rais lakini kuna nyie mliokaribu na Rais nawaomba mumshauri Rais wetu kwa kweli bila unafiki na bila kutanguliza ubinafsi," amesema.

Amesema katika uongozi wake wa Kanisa hakuwahi kusikia maoni ya watu ambayo yanatolewa sasa maeneo mbalimbali.

"Mwaka huu nimeisikia kuna tatizo linahitaji kutengenezwa," amesema Askofu Masangwa.

Askofu Masangwa amesema kila Mtanzania anapaswa kumsaidia Rais kufanya kazi vizuri ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Amesema hakuna ambaye alitarajia Rais Samia Suluhu Hassan angeliongoza Taifa, kwani kabla ya Rais Magufuli wengi walidhani Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa angekuwa Rais.

"Wengi tulidhani Lowassa angekuwa Rais lakini ghafla alitokea Magufuli na baada ya Magufuli akaja Rais wetu Samia Suluhu," amesema.

"Sasa tumsaidie Rais wetu aweze kuendelea kufanyakazi vizuri," alisisitiza.

Askofu Masangwa pia alizungumzia hoja za Muungano na kuwataka watanzania kushikamana na kuwa na umoja ili kutovunjwa Muungano.


"Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu tusikubali Muungano wetu kuvunjwa, kama kuna changamoto zifanyiwe kazi," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa Arusha, Mbunge wa Longido na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa amesema Arusha imempoteza kiongozi muhimu, alikuwa mshauri wao mkubwa na aliweza kuwaunganisha na kuvunja makundi.

Amesema Zelothe alikuwa mpatanishi, aliweza kuwaunganisha kwani kulikuwa na mgawanyiko ndani ya CCM.