Alichosema Makalla mkoani kwa Chongolo

Muktasari:

  • Asema mkoa huo, ambao kwa sasa unaongozwa na Daniel Chongolo, umepiga hatua ya maendeleo kwa haraka kutokana na Serikali kupeleka fedha.

Songwe. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema Mkoa wa Songwe umepiga hatua za kimaendeleo kwa kiasi kikubwa.

Makalla aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, amesema hayo mkoani Songwe akiwa ziarani pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na wajumbe wengine wa sekretarieti ya chama hicho.

“Songwe naijua, mimi nilikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati inaanzishwa, na niliwahi kukaimu ukuu wa mkoa huku kwa wiki mbili, hivyo nina historia nayo,” amesema.

“Nataka nikiri kwamba kwa miaka minane tangu umekuwa mkoa rasmi, Songwe imepiga kasi kubwa ya maendeleo na hakuna haja ya mkoa huu kuitwa kitindamimba kutokana na kazi kubwa ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameifanya,” amesema Makalla.

Amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi za maendeleo katika mkoa huo, ikilinganisha na miaka ya nyuma, hivyo ana kila sababu ya kupongezwa.

Mkoa wa Songwe ulimegwa kutoka Mkoa wa Mbeya, baada ya Rais wa nne, Jakaya Kikwete kutangaza kuanza kwa mchakato wa kuanzisha mkoa na wilaya mpya  Oktoba 18, 2015; na, mrithi wake Dk John Magufuli akatangaza uanzishwaji wake kwenye Gazeti la Serikali (GN) Namba 461 Januari 29, 2016.

Kwa sasa mkoa huo, unaongozwa na Daniel Chongolo, aliyekuwa katibu mkuu wa CCM hadi Novemba mwaka jana, kabla ya kuteuliwa na Rais Samia kuwa mkuu wa mkoa Machi 9, 2024.


Lengo la ziara

Makalla amesema lengo la ziara ni kuangalia uhai wa chama hicho, maandalizi ya uchaguzi, kuona utekelezaji wa ilani ya CCM na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi.

Mbali ya hilo, amesema kila mwana-CCM kuanza ngazi ya mtaa hadi ngazi za juu atembee kifua mbele kuonyesha na kueleza mafanikio yaliyofanywa na chama hicho bila aibu.

Amesema kama kuna mtu anasema CCM haijajenga zahanati, basi wamwonyeshe ilipo.

Makalla amesema kuna sehemu kunaweza kuwa na changamoto ya maji lakini kuna kisima kimechimbwa, wawaonyeshe kisima hicho.

 “Ukweli ni kwamba kila kijiji kuna alama ya jambo fulani ambalo limefanyika, kwa hiyo wana-CCM kwa kila ngazi tuonyeshe mafanikio yaliyofanywa na Serikali ya CCM bila kuona aibu,” amesema.