Ajali yaua watatu familia moja Mbwewe

Muktasari:

  • Watu watatu wanahofiwa kufariki baada ya ajali ya gari aina ya Toyota Alphard kuligonga lori kwa nyuma eneo la Mbwewe wilayani Bagamoyo.

Pwani/ Tanga. Watu watatu wanahofiwa kufariki kwenye ajali ya gari iliyotokea leo Alhamisi Desemba 28, 2023 eneo la Mbwewe wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital, Diwani wa Kata ya Mbwewe,   Omary Msonde  amesema kuwa ajali hiyo imetokea saa 12 alfajiri leo kwenye eneo hilo.

‘Waliofariki walikuwa wanaelekea mkoani Tanga wakitumia gari dogo aina ya Toyota Alphard lililogonga kwa nyuma lori la mizigo lililokuwa limeharibika kwenye eneo hilo,”amesema

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amekiri kuwa na taarifa za ajali hiyo na amesema alikuwa njiani kuelekea eneo la tukio huku akiahidi kulizungumzia kwa kina baadaye.

“Nimesikia hivyo niko njiani naelekea huko kwenye tukio,”amesema RPC Lutumo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 28, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando kwenye mtandao wa kijamii amesema kuwa waliofariki ni familia ya Diwani wa Kata ya Kabuku Halmashauri ya Wilaya Handeni mkoani Tanga, Nurudin Semnangwa.

"Semnangwa amefiwa na mke wake pamoja na mtoto kutokana na ajali ya gari iliyotokea asubuhi hii eneo la Mbwewe, Pwani. Kwenye ajali hiyo pia dada wa kazi amefariki, dereva na mtoto mwingine wamejeruhiwa. Taarifa zaidi itatolewa.",imesema taarifa hiyo ya Mkuu wa Wilaya Albert Msando.