Ahukumiwa jela miaka saba kwa wizi mali ya Sh131 milioni, mlinzi asalimika

Mshtakiwa Gasper Mushi akitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela Kwa kosa la kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh131 milioni. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  imemuhukumu Gasper Mushi kwenda kifungo cha miaka saba kwa kosa la kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh131 milioni.

Dar es Salaam. Mshtakiwa Gasper Mushi amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya kuvunja ghala na kuiba vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh131 milioni mali ya Mariwa Investment Store.

Pia mahakama hiyo imemuachia huru mlinzi wa Mariwa Hardware Store, Mohamed Mapesa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka la kushindwa kutimiza majukumu yake na kuruhusu wizi huo kufanyika.

Hukumu hiyo imetokewa leo Julai 3, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio amesema kwa kuzingatia ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na upande wa mashtaka mshtakiwa amekutwa na hatia ya  kuvunja ghala na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh131.3 milioni

Mrio alisema mshtakiwa huyo aliiba mashine aina ya Desk jet HP 2050 A, kifaa cha kurekodia video pamoja na fedha taslimu ambavyo vyote vyenye thamani hiyo.

Amesema kwa upande wa mshtakiwa Mapesa mahakama hiyo imeshindwa kuthibitisha shtaka la kushindwa kutimiza majukumu yake na kuruhusu wizi huo kufanyika hivyo inamuachoa huru.

Mrio alisema mahakama hiyo imezingatia maombolezo yake ya kuomba apunguziwe adhabu, kosa lake la kwanza, anategemewa na familia yake

"Mahakama imezingatia mshtakiwa hana kumbukumbu ya makosa  ya nyuma na hili ni kosa lake la kwanza hivyo  kwa kuzingatia haya mahakama inakupunguzua adhabu,"alisema Mrio.

Kutokana na hilo mahakama hiyo  imemuhukumu mshtakiwa huyo katika kosa la kuvunja ghala la Mariwa Hardware Store kwenda jela miaka mitano huku kosa la wizi wa vitu mbalimbali akihikumiwa  kifungo cha miaka saba jela lakini vyote vimeenda pamoja ambapo atafungwa miaka saba.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa terehe isiyofahamika kati ya Juni, 2018 maeneo ya Kiungani wilaya ya Ilala mkoani Dar es salaam mshtakiwa Mushi alivunja ghala la Mariwa Investment Store na wizi wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh131 milioni.

Katika shtaka lingine ambalo lililokuwa linamkabili mshitakiwa Mapesa inadaiwa akiwa kama mlinzi wa eneo hilo alishindwa kutimiza majukumu yake ya kazi na kuruhusu mali hizo kuibiwa.