Viongozi wadaiwa kukacha mkutano wa diwani Simanjiro

Diwani wa Loiborsiret wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Ezekiel Lesenga (kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Loiborsiret na  kusikiliza kero na changamoto zao pamoja na kuwasomea taarifa ya miradi ya maendeleo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  •  Wanakijiji wamedai kuwa viongozi wa kata na kijiji hawajashiriki mkutano wa Diwani wa Loiborsiret wilayani Simanjiro wakihofia kuulizwa maswali

Simanjiro. Wakazi wa Kijiji cha Loiborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamewashukia mwenyekiti wa kijiji hicho  Kimaai Saruni na mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Aloyce Teme kwa kutoshiriki mkutano wa Diwani wa Loiborsiret, Ezekiel Lesenga maarufu Maridadi.

Wananchi wamedai viongozi hao wamegoma kushiriki mkutano wa diwani wao uliokuwa na agenda ya kusoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kuhofia kuulizwa maswali magumu juu ya uuzwaji wa ardhi ya kijiji hicho.


Hata hivyo, Mwananchi Digital imezungumza na viongozi hao ambao wamesema kinachozungumzwa hakina ukweli.

Mwenyekiti wa kijiji, Saruni amesema hakuwa na taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo.

"Kuhusu uuzaji ardhi, hakuna hata nusu heka niliyouza wala Serikali ya kijiji hakuna waliyouza hizo ni siasa, waliouza mashamba yao wanajulikana ni watu binafsi tena waliuza bila kushirikisha Serikali ya kijiji," amesema Saruni.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Loiborsiret, Teme amesema hakupata mwaliko wala  taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo.

"Suala la kuuza ardhi ya kijiji anayetakiwa kuulizwa ni mwenyekiti wa kijiji, mimi nilishindwa kufika kwa sababu sikualikwa," amesema Teme.

Mmoja kati ya wakazi hao, Lazaro Lambagi akizungumza katika mkutana leo Jumamosi Mei 4, 2024, amesema hofu ya kuulizwa maswali magumu kutokana na kuuza ardhi kumesababisha viongozi hao kutohudhuria mkutano.

"Aliyekuwa DC Simanjiro, Dk Suleiman Serera aliagiza viongozi kusimamisha uuzaji ardhi hadi uchaguzi wa Serikali za mitaa upite, ila hawa wameendelea kuuza kwa kificho," amedai Lambagi.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la  Kalai Mollel amedai kuwa viongozi hao wameshiriki kuuza eneo la ardhi ya Kitongoji cha Oltepelek na wameng'oa vibao vya eneo la malisho na kuviweka ofisi ya Kijiji cha Loiborsiret.

"Tumelalamikia suala hili la uuzwaji ardhi kwa muda mrefu ila viongozi hawa wabishi, ila mwisho wao umefika," amedai Mollel.

Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Mary Chisoji amesema wenyeviti walishapewa onyo la kutouza ardhi hadi uchaguzi wa Serikali za mitaa utakapofanyika na kupatikana viongozi.

"Hili la kurejeshwa kwa vibao vilivyong'olewa vya malisho Kitongoji cha Oltepelek, tutavirejesha baada ya wiki moja wananchi wasijali kuhusu hilo," amesema Chisoji.

Hata hivyo, diwani wa kata hiyo, Lesenga amesema kitendo cha viongozi hao kususia ziara na mkutano wake kimemkwaza.

Amesema hiyo ni dalili ya kufanyika kwa siasa chafu zisizo na tija kwa maendeleo ya wananchi.

"Nimekuja kuelezea utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kupitia mikutano ili tuone mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na kusikiliza kero na changamoto za watu ila viongozi hao wamegoma hawajafika," amesema Lesenga.

Amesema suala la kung'olewa vibao vya eneo la malisho atalisimamia mpaka virejeshwe huku akisema alikuwepo wakati wanapanga matumizi bora ya ardhi kupitia mkutano wa kijiji.

"Kwa sababu mliamua wenyewe eneo hilo liwe la malisho nitaweka miguu yangu hapo kutetea hilo na kama viongozi hao wameshiriki ardhi ile watakuwa wamejiharibia," amesema Lesenga.