Timu ya mawaziri kuongeza nguvu mafuriko ya Rufiji, Kibiti

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Abdulrahman Kinana akiwa kwenye boti alipoenda kuangalia maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika Kijiji Cha Muhoro, leo  Aprili 9, 2024 na kuwapa pole wakazi wa Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani waliokumbwa na mafuriko hayo. Picha na CCM

Muktasari:

 Majaliwa ametoa kauli hiyo jana usiku Jumanne Aprili 09, 2024 wakati wa hafla ya futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema timu ya mawaziri itakwenda wilaya za Rufiji na Kibiti Mkoa wa Pwani kuungana na timu za watalaamu ili kufanya tathimini ya pamoja kutokana na athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokea wilayani humo.

Majaliwa ametoa kauli hiyo jana usiku Jumanne Aprili 09, 2024 wakati wa hafla ya futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati wa hafla ya iftari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma Aprili 09, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Sisi ndio tunaratibu Idara ya Maafa kitaifa, hapa tunapozungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama pamoja na Katibu Mkuu, Dk Jim Yonaz wako njiani wanaelekea mkoani Pwani.

“Mto rufiji umejaa na kata nne zipo kwenye maji, mawaziri wengine wa sekta ikiwamo ya afya, kilimo na mifugo pia wanakwenda ili kuimarisha uratibu wa zoezi," amesema Majaliwa.

Katika mafuriko hayo yanayotokana na mvua za masika, yameathiri kata mbalimbali za Rufiji na kuwaacha wananchi hawana makazi, huduma za kijamii zikiathirika, vifo vya watu wawili na uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Baadhi ya maeneo yamezingirwa na maji hivyo kulazimu kutumika kwa boti kuwavusha watu kutoka eneo moja kwenda jingine.

Jana Jumanne, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana aliwatembelea waathirika wa mafuriko hayo na kuitaka Serikali kuharakisha utoaji wa misaada kwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

"Nimekuja kujionea hali halisi na kuwapa pole, najua hata nikiongea hotuba kubwa itakuwa si chochote, naenda kuongea na viongozi wa Serikali," amesema Kinana.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namna inavyodhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.

“Kamishna amefanya kazi nzuri na kuboresha kwenye sekta yake, hivi sasa taasisi yake haiishii tu Makao Makuu ya nchi, ameshusha kwenye kanda na tayari wakurugenzi wameshaenda kwenye maeneo hayo ambao watakamata wazalishaji, wasafirishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya,” amesema.

Viongozi wengine walioshiriki katika iftar hiyo ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.