Serikali kutoa mwongozo mahudhurio shuleni wakati wa mvua

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Yazitaka shule kuchukua tahadhari inapowezekana, ikiwamo kutowalazimisha wanafunzi kuhudhuria shule kama hali ya hewa ni mbaya.

Dar es Salaam. Serikali imezisihi shule kuchukua hatua za tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ikiwamo kutowalazimisha watoto kwenda shule kama hali imeonekana kuwa mbaya kwa siku husika.

Imesema wazazi wana haki ya kutoruhusu watoto kwenda shule endapo watakuwa na wasiwasi na hali ya hewa ya siku husika.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Aprili 24, 2024 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika utoaji huduma ya elimu kutokana na athari za mafuriko.

Profesa Mkenda amesema tangu mvua zianze kunyesha kumekuwa na changamoto ya wanafunzi kufika shule, hali iliyozilazimu baadhi ya shule kuwapumzisha watoto kwa muda.

Amesema Serikali inaendelea kuwasiliana na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kueleza iwapo hali itazidi kuwa mbaya watalazimika kusitisha masomo.

"Tunatoa wito wakati hali ya hewa ikiwa si nzuri, wazazi wana haki ya kuwazuia watoto kwenda shule.  Kwani kitu cha kwanza ni usalama wa watoto wetu, hivyo shule zina wajibu wa kufidia vipindi inapotokea hali mbaya ya hewa na wanafunzi kushindwa kufika shule,” amesema.

Hata hivyo, amesema tatizo wanaliona zaidi katika shule binafsi ambako watoto wanasoma mbali na maeneo wanayoishi.

TMA katika taarifa imetoa angalizo la uwapo wa mvua katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikihimiza tahadhari kuchukuliwa.

Profesa Mkenda amesema Kamishna wa Elimu hivi karibuni atatoa mwongozo, ikiwemo mabadiliko kidogo ya ufundishaji.

Kwa magari yanayobeba wanafunzi Profesa Mkenda ameagiza tahadhari kuchukuliwa kwa sababu Serikali haitaki kusikia imepoteza watoto kwa sababu tu magari yalikuwa yakiwapeleka shule.

Alfajiri ya Aprili 12, 2024 gari la Shule ya Msingi Ghati Memorial, jijini Arusha lilipata ajali baada ya kuanguka kwenye korongo la Sinoni lililojaa maji eneo la Dampo.

Katika ajali hiyo wanafunzi wanane walifariki dunia pamoja na msamaria mwema aliyeshiriki kazi ya uokoaji.

Gari hilo lilikuwa na jumla ya watu 13, wakiwemo wanafunzi 11, matroni na dereva.

Kuhusu shule za Serikali ambazo zimeathiriwa na mafuriko, Profesa Mkenda amesema wamejipanga kuzifanyia ukarabati na zile ambazo zipo katika maeneo hatarishi watatafuta maeneo mengine ya kuzijenga.

Kwa shule zilizoathiriwa na mafuriko wilayani Rufiji mkoani Pwani, amesema Serikali imeruhusu wazazi kuchagua shule zingine ambazo wangependa watoto wao wakasome.

Amesema kazi hiyo wataifanya kwa kushirikiana na maofisa elimu kata.

"Tumetoa nafasi ya watoto wetu kuendelea na masomo katika shule nyingine tatizo la mafuriko likiisha kama mzazi ataridhia mtoto kubaki katika shule aliyohamia uwanja upo wazi," amesema Profesa Mkenda.