RC Chalamila asisitiza mshikamano msibani kwa Gardner

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Media, Gardner Habash.

Muktasari:

  • Wananchi wajitokeza kuuaga mwili wa  aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM Gadner Habash

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wasanii, wanahabari na watu wengine kuoa taarifa pindi mwenzao anapopata tatizo akiwa hai.

Amesema wanatakiwa kutoa taarifa ili angalau watu waweze kushiriki kutoa michango kwa ajili ya kuokoa maisha wakati wa uhai wake.

Hayo amesema leo Aprili 22, 2024 katika viwanja vya Leaders Club wakati wa kumuaga aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM katika kipindi cha Jahazi Gardner Habash

"Wakati fulani tunapokutana kwenye misiba kama hii tungekuwa tunakutana wakati mwenzetu akiwa anaugua hospitali kwa kuchanga michango ingekuwa na tija zaidi," amesema Chalamila.

Amesema wingi wa watu waliojitokeza angekuwa anaona kwa macho yake angemshukuru Mungu aliyemleta duniani kuliko alivyofunga macho na huku watu wakiongea mambo mengi akiwa amenyamaza.

Chalamila amewataka wananchi kuendeleza mshikamano na si kusubiri roho kuacha mwili kwa kutoa michango ya kuhudumia wakiwa hai sio hadi atakapofariki dunia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu ambaye ameungana na viongozi wengine wa Clouds Media nchini kwa ajili ya kutoa salamu za rambirambi, amesema Gardner aliifanya kazi ya utangazaji kuwa rahisi kwa kueleza mambo magumu kwa njia ya burudani.

"Tuna kazi moja ya kutoa taarifa lakini taarifa tunazozitoa kwa jamii ambayo inabadilika kwa jinsi inavyotumia ile taarifa kumbe basi ‘innovation’ (ubunifu) ni muhimu sana hivyo Gardner alitumia hiyo nafasi kwa kutoa mambo magumu kuwa burudani," amesema Machumu.

Amesema vipindi walivyokuwa wanafanya walikuwa wanatumia mfumo wa edu-tainment kwa kutoa mambo magumu kwa burudani ambayo “wakati watu wanajadili mambo magumu wao walifanya kuwa burudani.”

Awali, akisoma wasifu wa marehemu mdogo wake Dk Seline Mandala amesema Gardner alikuwa akisaidia watu bila kuwa na ubaguzi na hakusubiri malipo.

"Alikuwa anatusaidia ndugu na jamaa kila tulipokuwa tunahitaji msaada na hakusubiri malipo kwa kuwa alikuwa mwepesi wa kusamehe pale anapomkopesha mtu," amesema Dk Seline.

Gadner alifariki saa 11 alfajiri Aprili 20, 2024 akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao kata ya Tarakea, wilayani Rombo mkoa wa Kilimanjaro Aprili 23, 2024.