Mvua yatibua shughuli ya Muungano Musoma

Baadhi ya watu waliojitokeza kushiriki shughuli ya usafi katika Soko la Kwasanane Manispaa ya Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Ofisa Habari wa Mkoa wa Mara,  Ranfrida Ngatunga amesema mkuu wa mkoa ameamua kuahirisha shughuli hiyo kutokana na hali ya hewa

Musoma. Mvua zilizoanza kunyesha tangu usiku wa kuamkia  leo Aprili 26,2024 zimezuia ufanyaji wa usafi uliokuwa umepangwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Evans Mtambi kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Usafi huo ulitarajiwa kufanyika katika Soko la Kwasanane lililopo Kata ya Nyakato, Manispaa ya Musoma.

Ofisa Habari wa Mkoa wa Mara,  Ranfrida Ngatunga amesema mkuu huyo wa mkoa ameamua kuahirisha shughuli hiyo kutokana na hali ya hewa.

Mbali na usafi, pia mkoa ulipanga kusherehekea maadhamisho hayo kwa kufanya mkutano Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma na kungekuwa na shughuli mbalimali zikiwamo hotuba kutoka kwa viongozi na burudani.

Kuahirishwa huko kumefanyika ikiwa baadhi ya watumishi wakiwa wameishafika eneo la tukio huku wengi wao wakishindwa kushuka kwenye magari kutokana na mvua.

 “Tuliambiwa watumishi wote tushiriki kwenye usafi na baadaye tungejumuika kule Bweri kwa ajili ya hotuba na burudani," amesema mtumishi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Amesema mvua hiyo imesababisha watumishi wengi kushindwa kufika eneo la usafi kwa wakati uliopangwa hivyo ingekuwa vigumu shughuli hiyo kufanyika kama ilivyokuwa imekusudiwa.

"Unaweza kuona hapa wapo watumishi wengi ila wengi zaidi bado wameshindwa kufika hapa kwa sababu ya hali ya hewa na naamini wengi wao wanasubiri mvua iishe ndipo waje," ameongeza.

Tayari watumishi waliokuwa wamefika katika eneo hilo kwa ajili ya usafi wameanza kuondoka kurejea makwao baada ya kupewa taarifa juu ya shughuli hiyo kuahirishwa na mkuu wa mkoa.

Baadhi ya wakazi wa Nyakato wamesema kulingana na hali ya hewa hata ushiriki wa wananchi ungekuwa hafifu.

"Tuliambiwa usafi unafanyika kuanzia saa 12 asubuhi, lakini mpaka saa tatu ndio kama hivi unaona wengi wameshindwa kwa sababu ya hali ya hewa," amesema John Manyama.

“Hii mvua imetuharibia pamoja na kutaka kushiriki kufanya usafi lakini tulikuwa na kero zetu ambazo tulitaka kumfikishia mkuu wetu wa mkoa hasa ukizingatia ni mgeni na hajawahi kufika hapa sokoni kwetu," amesema Joyce Kitengule.

"Hapa hata wakisema wasubiri hadi mvua ikatike kwa vyovyote shughuli imeharibika maana itakapokatika muda utakuwa umeenda na watu watakuwa wako kwenye shughuli zao za kujiingizia kipato," ameongeza Michael Mtatiro.